October 17, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Samizi:Uchunguzi wa mapema wa saratani ya matiti huokoa maisha

Na Mwandishi Wetu ,TimesMajira

NAIBU Waziri wa Afya, Dkt. Florence Samizi, amewataka Watanzania kuimarisha juhudi za kujikinga na saratani ya matiti kwa kufanya uchunguzi wa afya mara kwa mara, akisisitiza kuwa utambuzi wa mapema unaweza kuokoa maisha na kupunguza gharama za matibabu.

Akizungumza wakati wa maadhimisho ya Mwezi wa Uelewa wa Saratani ya Matiti Duniani, yenye kaulimbiu “Kila simulizi ni ya kipekee, kila hatua ina thamani,” Dkt. Samizi amesema Serikali inaendelea kuwekeza katika mashine za kisasa za uchunguzi wa matiti aina ya mammography katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road ili kuboresha uwezo wa kugundua mabadiliko yanayoweza kuwa viashiria vya saratani katika hatua za awali.

Amesema kuchelewa kufika katika vituo vya afya hadi ugonjwa unapofikia hatua za juu huongeza ugumu na gharama za matibabu, hivyo wananchi wanapaswa kuchukua hatua mapema badala ya kusubiri dalili ziwe kubwa.

“Ujumbe wangu kwa Watanzania wote leo hii ni kwamba tusisubiri mpaka ugonjwa uwe mkubwa, tuchukue hatua mapema. Uchunguzi wa mapema unaweza kuokoa maisha,” amesema Dkt. Samizi.

Amerejea kauli ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, aliyoitoa Novemba 2025 kuhusu umuhimu wa kinga, akisema, “Kinga ni bora kuliko tiba.” Amesisitiza kuwa Serikali inaendelea kuweka nguvu katika kinga na utambuzi wa mapema wa magonjwa kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali.

Aidha, amezungumzia kampeni ya “Zijue Namba Zako” iliyoanzishwa na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, akiwataka wananchi kufahamu hali za miili yao kupitia vipimo muhimu vya afya, ikiwemo uzito, uwiano wa uzito na urefu, kiwango cha mafuta mwilini na kolesteroli, kwa ushauri wa wataalamu wa afya.

Dkt. Samizi amewataka wananchi kuzingatia mtindo bora wa maisha kwa kufanya mazoezi ya mwili mara kwa mara, kula lishe bora na yenye uwiano, kudumisha uzito unaofaa, kuepuka matumizi ya tumbaku na kupunguza matumizi ya pombe ili kupunguza vihatarishi vya magonjwa mbalimbali.

Katika hatua nyingine, amesema Serikali imewekeza katika mashine tatu mpya za kisasa za matibabu ya saratani, zinazolenga kuongeza uwezo wa kuhudumia wagonjwa wengi zaidi, kuboresha usahihi wa matibabu na kupunguza muda wa kusubiri huduma za mionzi.

Ameeleza kuwa uwekezaji huo unalenga kupunguza muda wa kusubiri matibabu ya mionzi kutoka takribani wiki 14 hadi wiki mbili, hatua itakayosaidia wagonjwa kuanza matibabu kwa wakati na kupunguza adha wanazopitia.

“Uwekezaji huu si suala la kuwa na mashine pekee, bali ni suala la kuokoa maisha, kupunguza mateso ya wagonjwa na kuhakikisha wananchi wanapata matibabu wanayohitaji kwa wakati,” amesema.

Dkt. Samizi amesisitiza kuwa Serikali inaendelea kuimarisha upatikanaji wa huduma za afya na mifumo ya bima ya afya ili kupunguza changamoto za gharama za matibabu kwa wananchi, pamoja na kusogeza huduma karibu na jamii.

Akizungumzia umuhimu wa uchunguzi wa saratani ya matiti, amewahimiza wanawake kuifahamu hali ya kawaida ya matiti yao na kuwahi katika vituo vya afya wanapoona mabadiliko yasiyo ya kawaida, yakiwemo uvimbe kwenye titi au kwapani, mabadiliko ya ngozi ya titi au chuchu.

Amebainisha kuwa saratani ya matiti inaweza kuwapata pia wanaume, hivyo kila mtu anapaswa kuwa makini na mabadiliko ya mwili wake na kutafuta huduma za afya mapema anapobaini dalili zinazotia shaka.

Amesema mapambano dhidi ya saratani ya matiti yanahitaji ushirikiano wa Serikali, taasisi za umma na binafsi, mashirika ya kijamii, viongozi, familia na wananchi kwa ujumla ili kuongeza uelewa, kuhimiza uchunguzi wa mapema na kuhakikisha wagonjwa wanapata matibabu kwa wakati.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Saratani ya Ocean Road, Dkt. Diwani Msemo, amesema matembezi yaliyofanyika ni fursa muhimu ya kuhamasisha jamii na kuongeza uelewa kuhusu saratani ya matiti, hususan umuhimu wa uchunguzi wa mapema na kuwahi kupata matibabu.

Dkt. Msemo amesema Rais Samia amefanya uwekezaji mkubwa katika taasisi hiyo, ikiwemo ununuzi wa vifaa tiba, ukarabati wa miundombinu na kuongeza ujuzi kwa wataalamu wa afya, hatua zinazolenga kuboresha huduma za uchunguzi na matibabu ya saratani.

Ameongeza kuwa ushirikiano kati ya Serikali, wataalamu wa afya na jamii ni muhimu katika kuimarisha elimu kuhusu saratani, kupunguza unyanyapaa na kuwasaidia wagonjwa kupata huduma kwa wakati.