December 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Samia: Tusiogope mageuzi kwenye mashirika ya umma

Asema madhumuni ya Serikali ni mashirika yafanye kazi na kuzalisha, Mwenyekiti Kamati ya Bunge ataka yasiyofanya vizuri kujitathimini, ataja sababu nne zinazoyatesa

Na Mwandishi Wetu, Arusha

RAIS Samia Suluhu Hassan amesema uamuzi wa Ofisi ya Msajili wa Hazina kufuta na kuchanganya baadhi ya mashirika ambayo hayaonekani kufanya vizuri umesababisha kelele nyingi.

Jambo hilo amesema linasababishwa na watu kuogopa mageuzi yanayofanyika katika mashirika ya umma licha ya kuonekana kufanya vizuri katika baadhi ya maeneo.

Rais Samia ametoa kauli jana jijini Arusha wakati alipofungua kikao kazi cha pili cha wenyeviti wa bodi na watendaji wakuu wa taasisi za umma kilichoandaliwa na Ofisi ya Msajili ya Hazina.

Alisema tayari Ofisi ya Msajili wa Hazina imeshafanya uamuzi wa kuyaunganisha mashirika 19 na kutengeneza saba. Rais Samia alitoa mfano wa Shirika la Maendeleo ya Taifa (NDC) ambalo alisema tangu anaanza kazi mwaka 1977 amekuwa akilisikia.

“Wakati huo lilikuwa likizalisha betri za redio zilizokuwa zikijulikana ‘National’ baadaye lilizalisha mipira ya magari inaitwa gereral tires lakini tangu hapo halikuwahi kusikika tena.
Kuanzia hapo, general tire ikafa kabisa, bwana ametoa bwana ametwaa na NDC haijulikani kama ipo au imekufa kwani kila mradi wake ni sifuri,” alisema. Rais Samia alisema, “Sijui ana mradi gani, hakuna.

Sijui ana chuma Liganga, Mchuchuma hakuna. Sasa unajiuliza huyu anafanya kazi gani, lakini lilipokuja pendekezo huyu sasa aondoshwe wizara imeandika mabarua kila sehemu NDC yetu, haiwezi kufutwa.”

Alisema inawezekana malengo yaliyokuwa yamewekwa juu ya NDC yalikuwa mazuri ila huenda yamepitwa na wakati, hivyo yanahitaji yarekebishwe au haina kazi. Amesema kwa sasa upo ushirikiano wa Taasisi za Umma na Binafsi (PPP) ambao huenda umechukua kazi za NDC lakini kufutwa kwake kunajenga hofu ambayo wakati mwingine isiyokuwa na ulazima.

Alitoa mfano wa mashirika yaliyochanganywa na kutengeneza kitu kimoja ni Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA) ambayo iliundwa kutokana na kuunganishwa taasisi ya utafiti ya viuatilifu vya kitropiki na kitengo cha huduma za afya za mimea ambazo zilikuwa zikifanya kazi zinazokaribiana na hayakuwa yanaleta faida.

“Kuchanganywa kwake sasa lile shirika lililoundwa (TPHPA) limeiwezesha Tanzania kupata vyeti vya ubora wa kimataifa kwa sababu malengo yote yamekusanywa na kufanya kazi moja na kukaa katika mlengo ambao ulitakiwa kufanyiwa kazi, sasa Tanzania ina viwango vya ubora wa kimataifa,” alisema.

Alisema kupatikana kwa vyeti hivyo vya ubora kumefanya kazi za Tanzania kutambuliwa kimataifa, masoko hayatakimbia bidhaa za Tanzania na wameweza kukusanya fedha na kutoa gawio serikalini. Amesema jambo hilo linathibitisha kuwapo faida ya kuchanganya mashirika ambayo hayafanyi vizuri huenda malengo yao yanafanana au yamepitwa na wakati.

“Kufuta pia si vibaya, kama uliundwa huko nyuma, haiui mtu jamani ambaye anazaliwa, anakua, anatumika, anatumika Mpaka anakua basi Mungu anasema basi anamchukua. Sasa itakuwa shirika tuliloliunda wenyewe kama halifanyi vizuri basi liondoke tu, hatuwezi kwenda kulinda nafasi za watu na mashirika hayazalishi, hayana tija haiwezekani,” alisema.

Alisema , akitoa mfano wa yale yanayotoka nje ya nchi namna ambavyo yamekuwa yakichukua zabuni ikiwemo za kujenga, biashara na kukusanya fedha kwenda nchini kwao.

“Sisi mashirika yetu yako hapahapa ndani, tunawapa nafasi nafasi wale, wabebe fedha zetu wapeleke kwao sisi tunaangalia tu, kwa hiyo nadhani wakati umefika wa kubadilika na kubadilika kweli kweli,” alisema.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Uwekezaji Mitaji ya Umma, Augustino Vuma, alitoa rai kwa taasisi ambazo hazifanyi vizuri kujitafakari na kuona ambavyo zinaweza kubadilika na kufanya vizuri zaidi ili tija ya uwekezaji wa mitaji ya umma iweze kuonekana.

Alisema kwa uzoefu waliona kama Kamati zipo sababu kama nne kubwa ambazo zinafanya taasisi zisifanye vizuri, moja ni ukosefu wa mitaji, ambapo kuna taasisi ambazo hazina mitaji ya kutosha na wakati mwingine zinakosa mitaji kutokana na madeni makubwa ambayo Serikali inakuwa nayo.

“Yaani Serikali inakwenda kukopa huduma kwenye taasisi hizo, lakini hailipi kwa wakati mfano mzuri ni taasisi ya Bohari ya Dawa ( MSD), Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) wa na TIB,” alisema Vuma.

Alisema kwa mtazamo wao taasisi hizo zikiwezeshwa vizuri hasa kwa Serikali kulipa madeni yake ambayo inadaiwa na taasisi hizi zinaweza kufanya vizuri na zikaleta maendeleo makubwa kwenye maendeleo ya nchi yetu.

Aidha, Vua alisema tatizo lingine ni uwezo mdogo wa viongozi , kwani kuna viongozi wengine wanakwenda kwenye kamati tunavyokwenda nao kwenye majadiliano unaona kabisa uwezo wao ni wa kawaida sana na pengine inatokana na upatikanaji wao sio wa kiushundani.

Alitaja sababu ya tatu kuwa ni ukosefu nidhamu, mtu anafanya kosa hawajibishwe kwa namna yoyote na mwisho ni minyororo ya kiutendaji hasa upande wa ajira na upande wa manunuzi .

“Unaweza kupata ntendaji mzuri sana wa taasisi, lakini wale kule anaowakuta hata akitaka kuwabadilisha kwa sababu uwezo wao ni mdogo mchakato wake unakuwa ni mgumu sana.

“Lakini kwa upande wa manunuzi akitaka kufanya manunuzi anakuta mchakato mrefu tofauti na sekta binafsi ambao ni mfupi,” alisema na kuongeza mwarobaini wa hayo ni sheria mpya ya uwekezaji ambapo kutakuwa na mfuko wa uwekezaji ambao utakuwa unatoa mitaji.