June 17, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Samia: TRA kusanyeni kodi kwa njia rafiki

Na Mwandishi Wetu,Timesmajiraonline, Simiyu

RAIS Samia Suluhu Hassan,ameitaka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kuendelea kukusanya kodi kwa njia rafiki kwa wananchi na kuwapatia elimu ya kodi,wale ambao hawana elimu ya kutosha juu ya ulipaji kodi kwa kile alichoeleza kujitegemea kiuchumi kunaletwa na Wananchi kupitia Kodi wanazolipa.

Rais Dk Samia alitoa kauli hiyo jana akiwa katika mkoa wa Simiyu,baada ya kuzindua jengo jipya la Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Aliwataka Watanzania kujenga utamaduni wa kulipa kodi kwa hiari,ili kuiwezesha nchi kujitegemea kiuchumi.

“Kutegemea msaada ni utumwa, hivyo TRA kupitia kodi zinazokusanywa zimekuwa zikitekeleza miradi ya kijamii kama vile kupeleka Maji, Umeme na huduma za Afya nchi nzima na katika miradi mikubwa ndiyo nchi imekuwa ikikopa au kupata msaada wa kutekeleza,”alisema Rais Samia

Alitumia uzinduzi huo wa jengo kuitaka TRA iendelee kukusanya kodi zaidi na kuahidi kuwaongezea nguvukazi pamoja na uwezo wa kujenga majengo ya kisasa zaidi.

Kwa upande wake Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Mwenda,alisema jengo hilo limegharimu kiasi cha sh. Bilioni 9.83 na ni miongoni mwa majengo mengine yanayojengwa nchi nzima kwa gharama ya sh. Bilioni 116.

“Mheshimiwa Rais tunashukuru kwa kutupatia fedha za ujenzi wa majengo yote yaliyokamilika na yanayoendelea kujengwa hii itasaidia tuendelee kukusanya Kodi na kuvuka malengo kama ilivyokuwa kwa miezi 11 mfululizo tangu kuanza mwaka wa fedha 2024/2025 pia tunashukuru umetuongezea nguvu Kazi ya Watumishi wapya 1896” alisema Mwenda.

“Tunataka TRA ikusanye zaidi ndiyo maana tumewaongezea nguvu Kazi na majengo ya kisasa, nendeni mkakusanye kodi kwa njia rafiki, lakini kwa wale masugu na viburi lazima nao wafanywe walipe Kodi kama ilivyo kwa wengine” alisema Rais Samia.

Aidha Rais Samia ameagiza kuongezwa kwa kasi ya ujenzi wa majengo ya TRA ambayo bado hayajakamilika ili yaanze kutoa huduma katika mazingira rafiki.

Kwa upande wake Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Juma Mwenda amesema jengo hilo na mengine yanayoendelea kujengwa nchini yataongeza utoaji huduma bora kwa Mlipakodi, yataongeza hamasa kwa Watumishi pia yataongeza makusanyo ya Kodi kwa ujumla.

“Rais tunashukuru kwa kutupatia fedha za ujenzi wa majengo yote yaliyokamilika na yanayoendelea kujengwa hii itasaidia tuendelee kukusanya kodi na kuvuka malengo kama ilivyokuwa kwa miezi 11 mfululizo tangu kuanza mwaka wa fedha 2024/2025 pia tunashukuru umetuongezea nguvu Kazi ya Watumishi wapya 1896” Kamishna Mkuu Mwenda alisema.

Wakati huo huo, Rais Samia alizindua viwanda viwili cha Pamba na Mabomba mkoani Simiyu huku akisisitiza kuwa, Serikali imedhamiria kufanya uwekezaji katika zao hilo na mabadiliko yake yataonekana taratibu kwa kukuza uchumi wa nchi, mkoa na watu.

Rais Dkt. Samia alisema hayo katika ziara yake Mkoani Simiyu wakati akizindua viwanda hivyo viwili ambavyo ni kiwanda cha kuchakata mabomba pamoja na kiwanda cha kuchakata pamba, wilayani Bariadi.

Dkt. Samia amezindua viwanda hivyo katika eneo la Salunda ambapo, amekiri kuridhishwa na uchakataji wa zao la pamba katika kiwanda hicho.

Pia alisema, ameridhika na maelezo mazuri aliyoyatoa Waziri wa Kilimo Hussein Bashe, mara baada ya kuwasili mkoani humo hivyo anatoa wito kwa wananchi kuwa tayari na mabadiliko yanayoendelea sekta ya Kilimo.

Rais Dkt. Samia alisema, mabadiliko hayaji mara moja ni hatua na yana maumivu lakini watakaoumia si wakulima bali wale waliozoea kuwalalia wakulima kwa kununua pamba kwa bei ya chini.

“Nawashukuru wananchi kwa mapokezi. Nimefungua kiwanda hiki cha mabomba na kuchakata pamba, nimeona kazi inayofanywa na
ubora wake nimejiridhisha, hatua hii itapunguza matumizi ya fedha za kigeni katika zao la pamba,”alisema.

Alisisitiza kuwa, kama ambavyo nchi imefanya vizuri katika zao la korosho, kahawa, tumbaku, mbaazi ndivyo ambavyo kwa sasa serikali inaenda kuweka nguvu katika kulipandisha zao la pamba.

“Uzalishaji wa mabomba utatusaidia sana, tunayo miradi mingi sana ya usambazaji maji sasa mabomba haya yanayozalishwa yatatusaidia huko.

“Tukiwa na wazee jana jioni Waziri wa Kilimo alitueleza mengi mipango ya Serikali katika kuliwezesha zao hili la pamba, tumepandisha zao moja moja sasa tumegeukia pamba hatua tunazochukua ni kwa faida yetu, mabadiliko yanakuwa na maumivu kidogo watakaoumia ni wale ambao hawalimi wanaonunua mazao kwa kuwalalia wakulima na hao ndio wanakuwa na kelele,”alisema.

Aliongeza kuwa “Hatua tunazochukua ni kwa faida ya nchi na wakulima tumefanikiwa katika korosho, tumbaku, kahawa, mbaazi huko wamefaidika sasa huku kwenye pamba tukae mguu sawa, Simiyu zao kubwa ni pamba na lengo la serikali ni kuwafikia wakulima wote,”alisema.

Alisema, mwekezaji wa kiwanda hicho amewaza vyema na ataungana na Serikali kuhakikisha nchi inasitisha upelekaji malighafi za pamba na kuitengeneza hapa hapa nchini ili watu wapate ajira.

“Hicho ndicho tunachotaka, Watanzania wenye uwezo wawekeze hapa na kukuza uchumi wetu sisi wenyewe niwaombe wafanyabiashara wengine wafanye jitihada za uwekezaji.
Serikali imefanya kazi nzuri za maendeleo na zinaonekana wekezeni nyumbani,”alisema.

Viwanda hivyo vyenye thamani ya Sh. bilioni 8, vinamilikiwa na Kampuni ya Moli Oil mills company LTD, ambao pia ni wamiliki wa kampuni za Nsagali.

Aidha viwanda hivyo vimezalisha takribani ajira 850 za moja kwa moja, pamoja na ajira nyingine 400, huku vikitoa fursa kwa wajasiriamali wadogo wadogo kunufaika kwa kufanya biashara za mama lishe.

Rais Dkt. Samia yuko katika ziara ya kikazi mkoani Simiyu, hadi Juni 19, mwaka huu.