*Ni wale waliopewa visiwa 15 kwa ajili ya uwekezaji, wasema baada hapo watanyang’nywa, wapongeza mwekezaji Hoteli Bawe Island he Cocoon Collection
Na Mwandishi Wetu, Timesmajiraonline,Zanzibar
RAIS Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, wametoa miezi mitatu kwa waliopewa visiwa vidogo vidogo visiwani Zanzibar kwa ajili ya uwekezaji kufanya hivyo ndani ya kipindi hicho, vingine watanyang’anywa.
Viongozi hao walitoa kauli hiyo jana kwa nyakati tofauti visiwani Zanzibar wakati wa uzinduzi wa Mradi wa Hoteli ya Kitalii iliyojengwa kwenye Kisiwa cha Bawe, inayoitwa Bawe Island Hoteli.
Mradi huo wa hoteli umejengwa kwenye moja visiwa vidogo vidogo kati ya 15 vilivyokodishwa kwa wawekezaji.
Uzinduzi wa hoteli hiyo ni mwendelezo wa Maadhimisho ya Miaka 61 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.
Awali wakati akimkaribisha Rais Samia ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye uzinduzi huo, Rais Mwinyi alisema wale wote waliopewa visiwa hivyo wanapewa miezi mitatu ya kufanya uwekezaji, vinginevyo watanyang’anywa.
Rais Samia kupitia hotuba yake naye alisema; “Nami naungana na Rais Dkt. Hussein Mwinyi, kuwataka wale wote waliopewa visiwa kwa ajili ya uwekezaji baada ya miezi mitatu bila kufanya hivyo wanyang’anywa.”
“Wawekezaji wapo wengi sasa, baada ya miezi mitatu kama hawajawekeza maana yake wapo wananadi visiwa vyetu, sasa kabla hawajatunadi ngoja tutafute wawekezaji wa kweli,” alisema Rais Mwinyi.
Rais Samia, alitumia fursa hiyo kuwashukuru wamiliki wa mradi kwa kutimiza ahadi zao kwa mujibu wa makubaliano yao na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Alisema mwaka jana wakati wa maadhimisho ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ndipo liliwekwa jiwe la msingi la mradi huo.
“Binafsi nimefarijika sana kuona uwekezaji kama huo umetekelezwa ndani ya muda na pili kwa kuzingatia miongozo na masharti yanayohitajika ya uwekezaji wa visiwa vidogo vidogo,” alisema Rais Samia.
Aidha, Rais Samia alisema mradi huo ni mradi wa tatu kuwekezwa na mwekezaji huo, ambapo anamiliki hoteli tatu visiwani Zanzibar.
“Wamewekeza kwenye mradi mitatu na hiyo ni ishara kwamba wawekezaji wetu wanaridhika na mazingira yaliyopo ya kufanya uwekezaji, lakini pia mazingira ya utawala, urasmu umepungua kwa kiasi kikubwa, sheria zimerekebishwa vizuri, hivyo wawekezaji wanavutiwa kuwekeza Zanzibar,” alisema.
Pia alisema mwekezaji huo amefanya uwekezaji wa dola za kimarekani milioni 42.
” Huo sio uwekezaji mdogo ndugu zangu, nimezunguka nimeona. Kuna uwekezaji wa kutengeneza umeme wa jua, lakini wana mradi wa kuchukua maji ya chumvi, kuyatoa chumvi yote na kufanya maji kwa ajili ya matumizi ya hoteli ndiyo maana gharama imekuwa kubwa mno,” alisema.
Alisema anaamini uamuzi wa wawekezaji hao kufanya uwekezaji huo wa tatu visiwani humo umetokana na uzuri wa visiwa vya Zanzibar pamoja na imani kubwa waliyonayo kwa Serikali na sera zetu nzuri.
Aidha, Rais Samia alisema uongozi ni kuona mbali, hivyo, Rais Mwinyi aliona mbali na kuja na wazo la kukodisha visiwa vidogo vidogo ili viwanufaishe.
“Tulikuwa na visiwa ambavyo vingeweza kujenga uchumi wa Zanzibar , lakini uchumi tuliukalia, kisiwa hiki kilikuwa kikitumiwa na wavuvi tu.
Walipomaliza kuvua tulichokuwa tunapata kufuata samaki kwenye soko la Malindi, ndiyo faida kuliyokuwa tukipata na kwa vijana kwenda kustarehe.
“Lakini leo hii mradi huu unaleta ajira 400 za watoto wa Kitanzania, umeleta ajira wakati wa ujenzi, umeleta ajira wakati wa uendeshaji, lakini utalipa kodi ndani ya Serikali, utatufanya tukuze mapato, lakini pia utakuza jina la Zanzibar,” alisema na kuongeza;
“Sio muda mrefu Bawe Island itakuwa ikitamba kwenye mitandao na wakieda nje wataimba Bawe Island.”
Alisema ilipotangazwa visiwa hivyo kukodishwa kwa wawekezaji walikuwa wakali kidogo. “Kila kitu kinaonekana hakiwezekani mpaka kifanyike, leo niambieni nani anajuta kuwa na mradi kama huu”?Alihoji na kuongeza;
“Mradi kama huu utaleta ajira, utaleta mapato na utainua jina la nchi yetu Zanzibar,” alisema.
Kuhusu Maadhimisho ya Miaka 61 ya Mapinduzi Zanzibar, Rais Samia alisema yanawakubusha lengo na dhamira ya Mapinduzi hayo.
Alisema Mpinduzi hayo yalilenga kuondoa ubaguzi na kuwaletea wananchi maendeleo na kustawishi hali zao. “Tupo hapa tumenawili, tunaimba, tumefurahi, tunapendeza, jamani mimi huwa naagalia harusi za Zanzibar.
Jamani ukiangalia harusi za Zanzibar hausemi hiki kisiwa kina maskini. Hakuna na yote ni kazi ya Mapinduzi Matukifu ya Zanzibar. Kwa wale vijana wa zamani ebu chukueni picha za mavazi ya mababu zetu muone leo mambo yalivyo,” alisema Rais Samia kuongeza;
“Ukiangalia harusi ya Zanzibar, hausemi Zanzibar kuna maskini. Yaani ukiangalia watu walivyovaa, zawadi wanazotoka nazo unasema ehee, hii Zanzibar au Ulaya? Mapinduzi yametuletea neema ndugu zangu.”
More Stories
Tanzania,Uturuki kushirikiana kuinua sekta ya utalii nchini
Wanaoficha watoto wenye ulemavu kusakwa
Mawakili Tabora walaani kuziwa kutekeleza majukumu