January 4, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Samia: Mwaka 2024 ulikuwa wa mafanikio

*Aanika mambo makubwa yaliyotekelezwa na Serikali, asisitiza ulikuwa wa kihistoria, sasa yajayo yanapendeza, asema 2025 ni muhimu kwa maendeleo ya demokrasia

Na Mwandishi Wetu,Timesmajiraonline,Dar

RAIS Samia Suluhu Hassan, amesema Mwaka 2024 ulikuwa mwaka wa kihistoria, wenye mafanikio na unaotupa matumaini zaidi tunapoitazama kesho ya Taifa letu.

Rais Samia alitoa kauli hiyo jana kupitia hotuba yake ya mwaka mpya kwa Watanzania. Alisema katika jitihada za kutekeleza majukumu yake alipata fursa ya kufanya ziara katika baadhi ya Mikoa, na kote alikopita alijionea ari na hamasa kubwa ya wananchi kujiletea maendeleo.

“Kuanzia Morogoro hadi Rukwa, Mwanza hadi Ruvuma na Zanzibar, kote niliona kazi inaendelea. Serikali inatekeleza majukumu yake, wananchi wanajituma na mabadiliko yanaonekana,” alisema Rais Samia.

***Masuala makubwa yaliyojiri

Rais Samiakupitia hotuba yake hiyo alianika masuala makubwa yaliyojiri, ambapo kwa mwaka 2024 tuliadhimisha miaka 60 ya kuasisiwa kwa Muungano wetu.

“Kama alivyowahi kusema Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere “Tanzania ni nchi ya kuundwa na sisi wenyewe, kwa hiari yetu wenyewe, baada ya kukomboa sehemu zake kutoka katika Ukoloni.”

Hivyo basi, tuendelee kujivunia na kuudumisha Utaifa wetu, uliojengwa katika misingi imara ya Muungano wa Jamii mbili zenye udugu wa asili,” alisema Rais Samia
.
Alisema pamoja na kuadhimisha miaka 60 ya Muungano, tuliadhimisha pia miaka 60 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar, miaka 60 ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania, miaka 60 ya Jeshi la Polisi, na miaka 60 ya Mbio za Mwenge wa Uhuru, ni fahari kwamba tulifanya maadhimisho hayo yote huku nchi yetu ikiwa salama yenye Amani na Utulivu.

“Kwa hakika, ninavipongeza vyombo vya ulinzi na usalama kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kulinda nchi yetu. Nawashukuru pia wananchi kwa kuendelea kudumisha amani na umoja wa kitaifa; umoja ambao unaifanya Tanzania kuwa na sifa ya kipekee,” alisema Rais Samia.

***Uchaguzi wa Serikali za mitaa

Alisema mwaka jana kulikuwa na Uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika kwa amani na utulivu.

“Katika uchaguzi ule, kwa mara ya kwanza, wagombea ambao hawakuwa na washindani ilibidi wapate ridhaa ya wananchi, kwa kupigiwa kura ya ndiyo au hapana.

Hii imeondosha rasmi utaratibu wa kupita bila kupingwa, ambayo ni hatua kubwa katika ujenzi wa demokrasia nchini,” alisema Rais Samia.

***Mwaka 2024, ulikuwa mwaka wa mafanikio

Aliongeza kwamba Mwaka 2024 ulikuwa wenye neema na mafanikio. “Hatuna budi kumshukuru Mungu kwa yote.

***Kuimarika kwa uchumi

Alisema Uchumi wa nchi yetu uliendelea kuimarika na kuwanufaisha wananchi.

Alifafanua kwamba kati ya Januari hadi Juni 2024 uchumi ulikua kwa asilimia 5.4 ikilinganishwa na asilimia 4.8 katika kipindi kama hicho mwaka 2023.

***Deni la Taifa

Kuhusu deni la Taifa nalo, Rais Samia alisema liliendelea kuwa himilivu. Mfumuko wa bei umebaki ndani ya lengo la asilimia 3, hali iliyochangiwa na sera madhubuti za kifedha.

***Kuongezeka kwa uwekezaji

“Mwaka 2024 tulishuhudia ongezeko la uwekezaji kutoka ndani na nje ya Nchi. Kupitia Kituo cha Uwekezaji Tanzania kati ya Januari hadi Novemba 2024, tumesajili miradi ya uwekezaji 865 yenye thamani ya Dola za kimarekani bilioni 7.7 inayotarajia kuzalisha ajira 205,000.

Mamlaka ya Maeneo Maalum ya Uzalishaji kwa Mauzo ya Nje (EPZA), imetoa vibali vya kuwekezwa nchini viwanda vipya vikubwa 15 vyenye thamani ya Dola za Marekani milioni 235, vinavyotarajia kuzalisha ajira karibu 6,000 na kuuza nje bidhaa zenye thamani ya Dola za kimarekani milioni 94 kwa mwaka,” alisema Rais Samia.

***Ukusanyaji mapato

Kwa upande wa mapato, Rais Samia alisema Mamlaka ya ukusanyaji Mapato Tanzania (TRA) imefanikiwa kukusanya sh. trilioni 21.276 kati ya mwezi Januari na Oktoba, 2024 sawa na asilimia 99.3 ya lengo.

“Hili ni ongezeko la asilimia 17.5 ikilinganishwa na makusanyo katika kipindi kama hicho mwaka 2023. ” alisema.

***Ujenzi uchumi wa kidijitali

Rais Samia alisema mwaka jana wameendelea na jitihada za kujenga uchumi wa kidijitali kupitia matumizi ya TEHAMA. Katika kufanikisha hilo.

“Tumeunda Wizara mahsusi ya TEHAMA na tayari tumezindua Mkakati wa Uchumi wa Kidijitali. Miongoni mwa mipango yetu ya baadaye katika kutekeleza mkakati huo ni kuhakikisha kuwa kila Mtanzania anatambulika kwa kutumia Jamii Namba, itakayotolewa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA).

***Diplomasia

Kwa upande wa Diplomasia, Rais Samia alisema mwaka huu nchi yetu ilizidi kuimarika na kutuletea manufaa makubwa katika nyanja za kimataifa.

“Tumepata heshima ya kushiriki Mkutano wa G20, ambao pamoja na maamuzi mengine yaliyofanyika, mkutano huo pia uliazimia kuunga mkono jitihada za upatikanaji wa nishati safi, na vile vile, uliazimia kuimarisha uwekezaji kwenye kilimo ili kuondosha njaa na umaskini duniani; jitihada zinazoendana na malengo yetu Tanzania,” alisema.

***Kung’ara kwa Tanzania

Rais Samia alisema kwa mara nyingine tena, Tanzania iling’ara kwenye medani za kimataifa baada ya mgombea wetu, Daktari Faustine Ndugulile kuwania na kushinda nafasi ya kuwa Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani, Kanda ya Afrika.

“Hata hivyo, kwa mapenzi ya Mwenyezi Mungu, Dkt. Ndugulile alituacha kabla hata ya kuingia ofisini. Tunazidi kumuombea pumziko la Amani,” alisema.

***Ziara katika nchi 16

Alisema katika ziara walizozifanya katika nchi 16 duniani, zilituwezesha kujenga mahusiano ya kidiplomasia, na kiuchumi. ziara yangu nchini Jamhuri ya Korea, ilifanikisha kupatikana fedha zenye masharti nafuu kiasi cha Dola za kimarekani bilioni 2.5 kwa ajili ya kutekeleza miradi katika sekta za maendeleo.

“Kupitia fedha hizo, pamoja na mambo mengine, tutajenga kituo cha kisasa cha mafunzo ya reli, chuo cha mafunzo ya anga na urubani, ujenzi wa kituo cha kusambaza umeme Nyakanazi, na kituo cha uchenjuaji wa madini na maabara za kisasa za vito.

Miradi mingine itakayoangaliwa ni mradi wa Uendelezaji wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Ujenzi wa Kongani ya Viwanda Bagamoyo, na Ununuzi wa Mabehewa ya Abiria na Mizigo kwa ajili ya Kipande cha Reli kutoka Mwanza hadi Isaka, Ujenzi wa Bandari ya Wete na Ujenzi wa Bandari ya Uvuvi Bagamoyo. Fedha hizo pia zitatumika kwenye Ujenzi wa Barabara Zanzibar, ujenzi wa Ukumbi wa Mikutano Zanzibar, na Ujenzi wa Studio ya Filamu ya Kisasa na Kituo cha burudani mbalimbali kwa ajili ya ajira za vijana,” alisema.

Ziara hiyo pia ilifanikisha kusainiwa kwa Mkataba wa masharti nafuu wenye kiasi cha Dola za Marekani milioni 163.6 kwa ajili ya kugharamia mradi wa Ujenzi wa Hospitali ya Binguni na Kituo cha Mafunzo ya Afya huko Zanzibar.

***Ziara nchini Chini

Kuhusu ziara nchini China, alisema pamoja na kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia, ilifungua milango ya soko la bidhaa mbalimbali ikiwemo mihogo mikavu, soya, mabondo ya samaki, mazao ya baharini, asali, mashudu ya alizeti na pilipili.

Ni matarajio yangu kuwa wakulima na sekta binafsi watachangamkia fursa hizi ili tuweze kunufaika na soko hilo. Wakati wa ziara hiyo, Tanzania, China na Zambia zilikubaliana kuifufua reli ya TAZARA ili kuboresha usafiri wa abiria na usafirishaji wa mizigo.

Kwa upande wa ukanda wa SADC, Rais Samia alisema walipata heshima ya kupokea Uenyekiti wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika, yenye jukumu la kusimamia masuala ya Ulinzi na Usalama katika Kanda hiyo, ambapo mbali na masuala mengine tumeweza kusimamia uangalizi wa chaguzi kwenye Nchi za Botswana, Mauritius, Msumbiji na Namibia.

***Matokeo ya kumarika kwa uchumi

Rais Samia alisema kuimarika kwa uchumi kumetuwezesha kuendelea kufanya mabadiliko chanya katika mifumo yetu wa Elimu Msingi na Sekondari hadi vyuo vya ufundi.

Tumeendelea kusogeza huduma bora za afya karibu zaidi na wananchi, kutandaza zaidi miundombinu ya umeme, na kusambaza umeme vijijini.

Aidha, tumetekeleza dhamira ya kumtua mama ndoo kichwani, kwa kusimamia utekelezaji wa miradi 1,300 ya maji nchi nzima. Kukamilika kwa miradi hio kutatufikisha kutimiza lengo la asilimia 95 mijini na asilimia 85 vijijini.

***Miradi ya kimkakati

Kuhusu Tukiangazia miradi ya kimkakati, Rais Samia alisema baadhi yake tayari imefikia hatua ya kuanza kutoa huduma.

Alisema Bwawa la Mwalimu Nyerere limeanza kuzalisha umeme, na kufanya hali ya huduma za umeme nchini kuimarika.

Aliongeza kuwa uzalishaji kwa sasa umefikia jumla ya Megawatt 3,169 ikilinganishwa na mahitaji ya Megawatt 1,888.

Aidha, alisema Mradi wa Reli ya Kisasa – SGR, unatoa huduma kutoka Dar es Salaam kupitia Morogoro hadi Dodoma.

Alisema Shirika la Reli lilikuwa linasafirisha wastani wa abiria laki 3 hadi 4 kwa mwaka. “Inafurahisha kwamba ndani ya miezi mitano ya huduma za SGR, zaidi ya abiria 1,200,000 wameshasafiri na reli hiyo.

“Tumeendelea na maboresho kwenye sekta ya anga na uwekezaji kwenye shirika la ndege Tanzania. Mwaka huu, Shirika letu limefikisha ndege 16, na limeongeza safari za ndani ya nchi na kimataifa kufikia 25, ikiwemo kuanza tena safari za abiria kwenda Afrika Kusini na kukamilisha taratibu za kuanza safari za mizigo kwenda China.

Mwaka huu Shirika limefanikiwa kusafirisha abiria zaidi ya milioni 1 na laki 1 na zaidi ya tani 10,000 za mizigo.”

Aidha, alisema Serikali pia imeendelea kuwekeza kwenye miundombinu ya anga na kuboresha mifumo kwenye viwanja vya ndege. Mwaka huu tuliendelea na ujenzi wa viwanja vya ndege vya Arusha, Kahama, Mpanda, na Songwe. Mwakani tunatarajia kukamilisha viwanja vya ndege vya Iringa, Mtwara, Songea, Kigoma, Msalato, Musoma, Shinyanga na Sumbawanga.

“Hapa nataka nisisitize kuwa, miradi hii ni yetu sote, na imejengwa kwa kutumia rasilimali zetu. Hivyo, tunawajibika kuitunza ili itunufaishe sisi na vizazi vijavyo kesho. Vitendo vya kuhujumu miradi hii ni kulihujumu Taifa,” alisema Rais Samia.

***Kuendeleza mageuzi

Aidha, Rais Samia alisema katika hatua nyingine, waliendeleza mageuzi ndani ya Serikali ili kuimarisha utendaji na ufanisi.
“Tuliendelea na zoezi la kubaini taasisi na mashirika yanayopaswa kufutwa, kuunganishwa au kurekebishwa kwa lengo la kuongeza tija na ufanisi zaidi.

Mwaka huu pia tuliendelea kuchukua hatua za kuimarisha sekta ya ushirika ili kuchochea maendeleo vijijini. Dhamira ya Serikali ni kurejesha hadhi ya ushirika nchini.

Ili kupata maendeleo endelevu kwa ushirika na wana-ushirika, Serikali imechagiza mchakato wa kuanzisha Benki ya Ushirika, ambayo iko katika hatua za mwisho, ikiwemo kufikia lengo la ukwasi wa sh. bilioni 50,” alisema.

Ushirikishaji sekta binafsi

Rais Samia alisema mwaka jana waliendelea kushirikisha sekta binafsi na kuhamasisha uwekezaji kwa njia ya ubia baina ya Serikali na Sekta Binafsi (PPP) ili kuongeza ufanisi katika sekta za uzalishaji na huduma. Katika kufanikisha hilo mpaka sasa kuna jumla ya miradi 74 ya Ubia ambayo ipo katika hatua mbalimbali za maandalizi na utekelezaji.

Alisema hadi kufikia mwezi Desemba 2024, miradi 4 imefikia hatua ya utekelezaji, ambapo miradi miwili 2 ni ya uendeshaji wa bandari inayosimamiwa na TPA.

Miradi mingine ni Ujenzi wa Jengo la Biashara (Business Complex) kubwa kuliko zote Kariakoo na ule wa Ubungo – East African Logistic.

  Miradi mingine inayotazamiwa kuanza utekelezaji mwakani 2025 ni ujenzi wa barabara ya Haraka (Express way) kutoka Kibaha- Chalinze - km 78.9, mradi wa Ukaguzi wa lazima wa vyombo vya moto chini ya Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Polisi, mradi wa mabasi yaendayo kwa haraka (BRT) chini ya DART na mradi wa Ujenzi wa Jengo la Biashara na Hoteli ya Nyota Nne katika Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere chini ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA).

***Nishati safi ya kupikia

Katika kukabiliana na athari za mazingira kutokana na matumizi ya kuni, mwaka huu tulizindua Mkakati wa Kitaifa wa Nishati Safi ya Kupikia.

“Niwatake wahusika wasimamie ipasavyo utekelezaji wa Mkakati wa kuchochea matumizi ya nishati safi ili kufikia lengo la asilimia 80 ifikapo mwaka 2034. Aidha, nitoe rai kwa sekta binafsi kuchangamkia fursa zitokanazo na kukua kwa matumizi ya nishati

**Mwaka tuliouanza

Rais Samia alisema Serikali yetu itaendelea kuimarisha na kusambaza huduma za kijamii (Afya, Elimu, Maji na Umeme), tutachochea maendeleo kupitia ujenzi wa miundombinu, kuwaongezea fursa vijana na wanawake katika Biashara ndogo na za kati, na kuimarisha ustahimilivu wa Taifa.

“Tutaendelea kukamilisha miradi ya kimkakati, ikiwemo Bwawa la Kuzalisha Umeme la Mwalimu Nyerere, Daraja la Kigongo/Busisi ambalo limefikia asilimia 94, linalotazamiwa kulikamilisha mwezi Februari, 2025.

Tutatoa kipaumbele katika utekelezaji wa miradi ya kupunguza msongamano katika miji mikubwa kama vile Jiji la Dar es Salaam, Arusha, Mwanza, Mbeya na Dodoma na kurahisisha usafiri na usafirishaji katika miji inayokua kwa kasi,” alisema.

Alisema miongoni mwa miradi hiyo ni mradi wa Barabara za Mzunguko katika Jiji la Dodoma ambao umefikia asilimia 80, upanuzi wa Barabara ya Uyole-Ifisi-Songwe Airport jijini Mbeya ambao umefikia asilimia 20, na Awamu ya Tatu na Nne ya miundombinu ya barabara za mwendo kasi jijini Dar es Salaam, huku tukianza huduma kwenye Awamu ya Pili kwa njia ya Mbagala iliyokwishakamilika.

“Mapema mwakani, tunatazamia Reli ya SGR, ianze kusafirisha mizigo kwa vipande vya Dar es Salaam hadi Dodoma kiasi cha tani milioni 1 kwa mwaka, lengo ni kukuza ushoroba wa kibiashara na kimaendeleo unaochochea uzalishaji na ajira kwa wananchi kote inapopita.

Vile vile, tutakamilisha kipande cha Mwanza hadi Isaka na kukifanya kianze kutoa huduma. Ujenzi wa vipande vyengine hadi Kigoma vitaendelea kujengwa kama ilivyopangwa,” alisema

Aidha, Rais Samia alisema nchi yetu imeendelea kusimamia utekelezaji wa Falsafa ya R4, inayohimiza Maridhiano, Ustahamilivu, Mageuzi na Kujenga nchi yetu.

***Uhuru wa Habari

Rais Samia alisema vile vile, tunaendeleza uhuru wa habari unaoashiriwa na idadi kubwa ya vyombo vya habari, uhuru wa kujieleza, na uhuru kutoa maoni kupitia vyombo mbalimbali; na hata uhuru wa kukusanyika na kujumuika.

Mwaka huu Ripoti ya Maboresho ya kodi kupokelewa

*Katika hatua nyingine, alisema mwaka huu watapokea Ripoti ya Tume ya Rais ya Maboresho ya Kodi ambayo itatusaidia kuboresha wigo na mifumo ya kodi, pamoja na kustawisha mazingira ya kibiashara nchini.

Katika utekelezaji wa mapendezo ya Tume ya Haki Jinai, mwakani 2025 tutakamilisha Sera na kufanya marekebisho ya sheria mbalimbali zinazohusiana na masuala ya haki jinai. Tutaendelea pia kutoa msaada wa kisheria kwa wahitaji. Hadi sasa, jumla ya wananchi 495,552 wameshanufaika na Msaada wa Kisheria wa Kampeni ya Mama Samia Legal Aid chini ya Wizara ya Katiba na Sheria.

***Mwaka 2025 ni muhimu kwa maendeleo ya demokrasia

Rais Samia alisemaMwaka 2025 ni mwaka maalum kwa maendeleo ya kisiasa na kidemokrasia nchini.

“Tutafanya Uchaguzi Mkuu kuwachagua Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Wabunge na Madiwani, na kwa upande wa Zanzibar, tutachagua Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na Madiwani.
Miongoni mwa maandalizi ya awali ya uchaguzi huo, ilikuwa ni kufanya mashauriano na wadau wote wa kisiasa yaliyopelekea kurekebishwa kwa sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani, Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, na Sheria ya Vyama vya Siasa.

Ni imani yetu kwamba sheria hizo zitatuongoza vyema katika kusimamia kwa ufanisi chaguzi zijazo. Nitoe rai kwa wananchi na wadau wote wa uchaguzi kuhakikisha tunaidumisha sifa ya Nchi yetu ya kuwa na demokrasia iliyojengeka juu ya msingi wa uhuru na haki,” alisema Rais Samia.