Lengo ni kuwawezesha wakulima na kuinua uchumi wa jamii
Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuzindua rasmi Benki ya Ushirika (CoopBank Tanzania) ifikapo Aprili 28 mwaka huu, ikiwa ni sehemu ya jitihada za serikali kufufua benki za kijamii zilizowahi kufilisika nchini.

Akizungumza jana jijini Dodoma, Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, alisema uzinduzi huo ni utekelezaji wa maagizo mahsusi kutoka kwa Rais Dkt. Samia, aliyelitaka Wizara ya Kilimo kuhakikisha benki hizo muhimu kwa wakulima na wananchi wa kawaida zinafufuliwa na kuanza kutoa huduma.
Kwa mujibu wa Waziri Bashe, Benki ya Ushirika itaanza kutoa huduma kwa matawi manne ya awali ambayo yapo katika mikoa ya Dodoma, Mtwara, Kilimanjaro na Tabora.


“Hii ni hatua ya awali, lakini hatua inayofuata ni kufungua matawi mengine katika mikoa ya Kagera, Mwanza, Dar es Salaam, Mbeya na Katavi,” alisema Bashe.
Aidha, Waziri Bashe alibainisha kuwa mbali na matawi hayo, benki hiyo pia itakuwa na mawakala nchi nzima ili kuhakikisha huduma zinawafikia wananchi wa maeneo yote ya Tanzania kwa urahisi zaidi.
“Kwa sasa mafunzo kwa mawakala wa benki hiyo yanaendelea ili kuhakikisha huduma bora na weledi kwa wananchi. Kabla ya uzinduzi wa Aprili 28, kutatanguliwa na kongamano la wanaushirika litakalofanyika Aprili 27,” aliongeza Bashe.


Kwa upande mwingine, Waziri huyo alieleza kuwa dhamira ya Rais Dkt. Samia ni kuhakikisha wakulima na jamii kwa ujumla wanakuwa na benki mbadala ambazo zitawasaidia kwa urahisi tofauti na benki za kibiashara ambazo mara nyingi zimekuwa kikwazo kwa wakulima kupata mikopo au huduma rafiki.
“Hili ni jambo la msingi kwa sababu benki nyingi za ushirika zilifilisika, na sasa Rais ametuagiza tuzirejeshe kwa ajili ya kuinua uchumi wa wakulima na wananchi wa kawaida,” alisema Bashe.
Aidha, alibainisha kuwa Wizara ya Kilimo kwa sasa ipo katika mazungumzo na Wizara ya Fedha na Mipango ili kuhakikisha Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) inarejea katika majukumu yake ya msingi ya kuwahudumia wakulima na sio kufanya biashara kama benki za kawaida.
“TADB ni Benki ya Kilimo, sio ya biashara, hivyo hata mikopo inayotolewa inapaswa kuwa na masharti rafiki kwa wakulima wetu ambao hawawezi kuhimili masharti ya mikopo ya kibiashara,” alisisitiza Bashe.





More Stories
Mbunge ataka safari za ndege kuanzia Dodoma
Mbogo aomba Tume kuchunguza madai ya waliokuwa wafanyakazi wa EAC
TMA yapongezwa kwa uboreshwaji wa taarifa za hali ya hewa