Na Reuben Kagaruki, TimesMajira Online, Dodoma
NDANI ya kipindi kifupi, Rais Samia Suluhu Hassan, amefanya mageuzi makubwa ndani ya sekta ya afya. Mageuzi hayo yameenda sambamba na upatikanaji wa uhakika wa bidhaa za afya kila kona nchini.
Hili linadhihirishwa na huduma za kibingwa zinazotolewa na madaktari bingwa kupitia kampeni ya Madaktari Bingwa wa Dkt. Samia.
Kutokana na kuwepo bidhaa za afya za kutosha, madaktari bingwa hao wamekuwa wakitoa matibabu ya kibingwa hadi kwenye ngazi ya wilaya, nchini kote, jambo ambalo halikuwahi kutokea huko nyuma.
Wanafanya hivyo, kwa kutambua kuwa Serikali ya Rais Samia imewezesha upatikanaji wa bidhaa za afya hadi chini.
Mfano, wagonjwa waliokuwa wakitakiwa kutoka mikoani kwenda Muhimbili kufuata huduma za Kibingwa na Ubingwa Bobezi nchini kama mashine za kusafisha damu (Dialysis Machine), MRI, CT- Scan, Ultrasound, Digital X-Ray pamoja na vitendanishi vyake, huduma hizo sasa zinapatikana mikoani.
Uwepo wa vifaa hivi unawezesha utambuzi wa magonjwa kwa usahihi na kutolewa kwa tiba sahihi. Hatua hiyo inazidi kuimarisha afya za Watanzania, hivyo kuwa nyenzo muhimu katika uzalishaji mali.
Mafanikio ya MSD yanawekwa wazi na Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Mavere Tukai, akisema hadi kufikia Juni 2024, Bohari ya Dawa imepata mafanikio mbalimbali katika kutekeleza majukumu yake.
Anasema mafanikio hayo yamepatikana katika maeneo ya kuongezeka kwa utimizaji wa mahitaji ya vituo vya kutolea huduma za afya (Dawa, Vifaa, Vifaa Tiba na Vitendanishi).
Kwa mujibu wa Tukai, Bohari ya Dawa imeendelea kuhakikisha mahitaji ya vituo vya kutolea huduma za afya yanatimizwa kwa mujibu wa maombi yao.
“Kutokana na kuimarika kwa utendaji, utimizaji wa dawa, vifaa na vifaa tiba kwa vituo vya kutolea huduma za afya umeongezeka kutoka asilimia 71 mwaka 2022/23 hadi kufikia asilimia 84 mwaka 2023/24 na hivyo bidhaa nyingi kuweza kupatikana kupitia MSD,” anasema.
Sambamba na hilo, anasema MSD imeendelea kufanya ununuzi na usambazaji wa vifaa tiba vinavyohitajika katika vituo vya kutolea kama mashine za kusafisha damu (Dialysis Machine), MRI, CT- Scan, Ultrasound, Digital X-Ray pamoja na vitendanishi vyake.
Anafafanua kwamba uwepo wa vifaa hivi unawezesha utambuzi wa magonjwa kwa usahihi na kutolewa kwa tiba sahihi.
Eneo jingine anasema kuongeza mizunguko ya usambazaji wa bidhaa za afya ili kuhakikisha bidhaa za afya zinapatikana wakati wote kwenye vituo vya kutolea huduma za afya, Serikali kupitia Bohari ya Dawa imeendelea kufanikisha usambazaji wa bidhaa za afya nchi nzima kwa mizunguko sita (vituo kupelekewa bidhaa kila baada ya miezi miwili) kutoka mizunguko minne (vituo kupelekewa bidhaa kila baada ya miezi mitatu) na hivyo kupelekea vituo kuwa na dawa toshelevu muda mwingi.
***Kuongezeka kwa mtaji
Tukai anasema kwa mwaka wa fedha 2023/24, Serikali imetoa kiasi cha sh. bilioni 100 kama mtaji wa kuwezesha MSD kuimarisha upatikanaji wa bidhaa za afya na kukabiliana na changamoto za mnyororo wa ugavi.
“Fedha hizi zimesaidia MSD kuwa na uwezo wa kuhudumia mahitaji ya vituo kwa wakati na kuweza kutengeneza mikakati itakayofanya taasisi iweze kununua kwa tija na kuimarisha mahusiano na wazabuni mbalimbali,” anasema Tukai.
Anataja eneo jingine la mafanikio kuwa ni kuimarika kwa makusanyo ya fedha kutoka vituo vya kutolea huduma za afya.
Maboresho yanayoendelea yamewezesha vituo vya kutolea huduma za afya kuwa na imani na utendaji wa MSD, ambapo makusanyo ya fedha yatokayo kwenye vyanzo mbalimbali vya vituo vya kutolea huduma za afya na kuletwa MSD yameongezeka kutoka kiasi cha sh. bilioni 40.3 mwaka 2022/23 na kufikia kiasi cha sh. bilioni 118.9 kwa mwaka 2023/24.
***Kuongezeka kwa Mapato ya MSD
Tukai anasema kutokana na maboresho yanayoendelea kufanywa na Serikali, Mapato ya Bohari ya Dawa yameendelea kuongezeka kutoka kiasi cha sh. bilioni 359.6. kwa mwaka 2022/23, hadi kufikia zaidi ya kiasi cha sh. bilioni 510.07 kwa mwaka wa fedha 2023/24 ikiwa ni ongezeko la sh. bilioni 150.43 ambayo ni sawa na asilimia 42.
***Utekelezaji wa Sera ya Viwanda
Katika kutekeleza sera ya uanzishwaji wa viwanda, anasema Bohari ya Dawa imechukua hatua zifuatazo;
Moja, Tukai anasema ili kuongeza ufanisi wa usimamizi na uendeshaji wa shughuli za uzalishaji, MSD imeanzisha Kampuni Tanzu inayoitwa; “MSD Medipharm Manufacturing Company Limited”.
Pamoja na hivyo, anasema Juni 2024, Bohari ya Dawa imezindua Bodi ya Usimamizi wa Kampuni Tanzu hiyo ambayo itakuwa na jukumu la usimamizi wa shughuli za uzalishaji wa bidhaa za afya.
Hivyo, Kampuni hii itakuwa na uwezo wa kuingia ubia na wawekezaji wengine.
“Kwa sasa, kampuni hii itasimamia Kiwanda cha Mipira ya Mikono, Idofi kilichopo Njombe, Eneo la viwanda la Zegereni, mkoani Pwani, na Kiwanda cha Barakoa Dar es Salaam,” anasema Tukai.
Aneo lingine kuongeza ununuzi wa Bidhaa za Afya kutoka kwa wazalishaji wa ndani, ambapo Serikali kupitia Bohari ya Dawa imeendelea kuongeza ununuzi wa bidhaa za afya kutoka kwa wazalishaji wa ndani ambapo kwa mwaka wa fedha 2023/24, bidhaa za afya zenye thamani ya sh. bilioni 22.1 zilinunuliwa kutoka kiasi cha sh. bilioni 14.1 mwaka 2021/22 ikiwa ni ongezeko la asilimia 57.
“Dhamira hii itasaidia kuongeza uzalishaji na kuvutia wawekezaji ambapo matumizi ya fedha za kigeni yatapungua na ajira zitatengenezwa nchini,” anasema.
*** Ushirikishaji wa Sekta Binafsi
Katika kufanikisha adhma ya Serikali ya kushirikisha sekta binafsi,anasema Bohari ya Dawa imetambua maeneo yanayohitaji ushirikiano na sekta binafsi na inafanya uchambuzi ili wawekezaji wenye sifa waweze kushiriki kwenye uanzishaji wa viwanda vya kuzalisha bidhaa za afya.
Aidha, anasema Bohari ya Dawa imekuwa ikifanya mawasiliano na balozi zetu zikiwemo Balozi za China, Korea Kusini, Urusi, Algeria na maeneo mengine duniani ili kuweza kufanya utambuzi wa wazalishaji, wawekezaji na kuwezesha ununuzi wa bidhaa za afya kwa uhakika, ubora na gharama nafuu kwa wazalishaji wa ndani.
***Uanzishaji wa Viwanda vya Kuzalisha Bidhaa za Afya Nchini
Anasema Bohari ya Dawa ina viwanda viwili, ambavyo ni kiwanda cha barakoa kilichopo eneo la Keko, Dar es Salaam na kiwanda cha mipira ya mikono kilichopo Idofi, mkoa wa Njombe.
Anasema Kiwanda cha kutengeneza Barakoa kinazalisha barakoa za kawaida na barakoa maalum (N95).
“Barakoa hizi hutumika kwenye matumizi mbalimbali ya kawaida kwa lengo la kujikinga na maambukizi au vihatarishi vinginevyo na pia hutumiwa na watoa huduma katika vituo vya kutolea huduma nchini.
Kiwanda cha barakoa kimefanikiwa kuzalisha na kusambaza barakoa zenye thamani ya zaidi ya sh. bilioni 4 na kufanya nchi kujitosheleza kwa uzalishaji wa barakoa.
Anataja kiwanda cha kutengeneza mipira ya mikono (Gloves) kinapatikana eneo la Idofi- mkoa wa Njombe na kimeanza uzalishaji Februari 2024.
Hadi kufikia Juni 2024, Kiwanda kimeweza kuzalisha gloves zaidi ya milioni 4.
“Hadi sasa, kiwanda hiki kimetoa ajira zipatazo 136 kwa wakazi wa eneo la Makambako na kufanya ununuzi kwenye kampuni mbalimbali ziliozopo eneo la Makambako.
Kwa kutengeneza mipira ya mikono ya kiuchunguzi “examination gloves” pekee kiwanda kitaweza kuokoa zaidi ya sh. bilioni 11.
***jenzi wa Maghala ya Kuhifadhi Bidhaa za Afya
Anasema kutokana na uwekezaji mkubwa wa Serikali kwenye ujenzi wa vituo vya kutolea huduma za afya, ongezeko la fedha za ununuzi wa bidhaa za afya na uwekezaji kwenye vifaa tiba, mahitaji ya miundombinu ya kuhifadhia bidhaa za afya yameongezeka.
Anasema Kwa kutambua ongezeko hilo, Serikali kupitia Bohari ya Dawa imeanza ujenzi wa maghala ya kisasa katika Kanda ya Mtwara na Dodoma ili kukidhi upungufu uliojitokeza.
Anafafanua kwamba ujenzi huo ukikamilika utagharimu kiasi cha sh. bilioni 40. Kwa sasa, anasema mradi umefikia asilimia 55 kwa ghala la Mtwara na asilimia 58 kwa ghala la Dodoma.
Anasema kukamilika kwa ujenzi wa maghala kutasaidia kuimarisha uhifadhi wa bidhaa za afya kwenye viwango stahiki, kusogeza huduma karibu na vituo vya kutolea huduma za afya, kupunguza gharama za uhifadhi na kuimarisha utunzaji wa bidhaa za afya.
Anasema ujenzi huu wa maghala unatarajia kuongeza nafasi ya uhifadhi wa bidhaa za afya kwa mita za mraba 12,000 ambapo kwa ghala lililopo Dodoma mita za mraba 7,200 zitaongezeka na ghala la Mtwara kiasi cha mita za mraba 4,800 zitaongezeka hivyo kufanya ongezeko la uhifadhi kutoka mita za mraba 56,858.57 na kufikia mita za mraba 68,858.57.
***Kufanya Maboresho ya Utendaji MSD
Anasema Serikali imeweza kufanya maboresho ya kiutendaji kwa kuteua Bodi ya Wadhamini na kufanya mabadiliko ya Menejimenti.\
Aidha, maboresho haya yameimarisha usimamizi wa ununuzi wa bidhaa za afya kwa kuimarisha ufuatiliaji wa mikataba, kuhakikisha uwepo wa mikataba ya muda mrefu, kuimarisha mifumo ya TEHAMA na kuimarisha utendaji.
***Mikakati ya mwaka 2024/25
Anasema Bohari ya Dawa imejiwekea mikakati ifuatayo ili kuboresha upatikanaji wa bidhaa za afya na kuweza kujiendesha kibiashara:
Moja, kupitia mtaji unaotolewa na Serikali, Bohari ya Dawa itafanya ununuzi wenye tija kutoka kwa wazalishaji na hivyo kuongeza upatikanaji wa bidhaa za afya.
Kupitia Kampuni Tanzu, Bohari ya Dawa itaendelea na jitihada za kushirikiana na sekta binafsi ili kuongeza idadi ya viwanda vya bidhaa za afya nchini hivyo kupunguza matumizi ya fedha za kigeni.
Nyingine ni kuimarisha upatikanaji wa bidhaa za afya kwa kuzingatia mahitaji yaliyopo kwenye Bima ya Afya ya Taifa na kuweza kutambua wahitaji zaidi wa bidhaa hizo nje ya MSD.
Nyingine ni kutekeleza ujenzi wa maghala ya kuhifadhia bidhaa za afya katika mikoa ya Mwanza, Dar es Salaam, Ruvuma, Arusha na Geita.
Mikakati mingine luongeza ufanisi, kuongeza uwezo wa kuhifadhi kwa kujenga maghala na kuangalia maeneo ambayo yatapunguza gharama za usambazaji.
Mingine ni kuimarisha mifumo ya TEHAMA inayohusu usimamizi wa maghala na ushiriki kwenye kutengeneza mifumo ya NesTm kupitia mifumo inayohusu gharama za uendeshaji (logistiki) kwa kuongeza usimamizi kupitia Idara maalum ya uendeshaji.
Mingine ni kuimarisha mifumo ya Utawala, kufanya maboresho ya muundo ili kuendana na utendaji, kufanya tafiti na kushirikiana na taasisi mbalimbali kuboresha uendeshaji wa taasisi zikiwemo Taasisi za Elimu ya Juu.
Mikakati mingine ni kuimarisha kitengo cha ndani cha usimamizi wa utendaji.
*** Bohari ya Dawa
Bohari ya Dawa (MSD) ni Taasisi ya Serikali iliyo chini ya Wizara ya Afya iliyoanzishwa mwaka 1993 kwa mujibu wa Sheria ya Bohari ya Dawa Na.13 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2021 ikiwa na majukumu manne (4); Uzalishaji, Ununuzi, Utunzaji na Usambazaji wa bidhaa za afya kwa ajili ya vituo vya kutolea huduma za umma na binafsi zilizoidhinishwa na Wizara ya Afya.
Bohari ya Dawa inahudumia vituo vya kutolea huduma za afya 8,224 kutoka vituo 7,662 mwaka 2022/23 sawa na ongezeko la vituo 562 nchi nzima kupitia Kanda zake 10 zilizopo Dodoma, Dar es Salaam, Mtwara, Mwanza, Tabora, Kilimanjaro, Tanga, Kagera, Mbeya na Iringa.
More Stories
Gridi za Tanzania, Kenya kuimarisha upatikanaji wa umeme
Mama Zainab:Watoto yatima ni jukumu la jamii yote
DC Korogwe awataka viongozi wa vijiji kuwatumikia wananchi kwa uadilifu