January 11, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Samia kutekeleza kwa dhati Sera ya uongezaji thamani madini nchini

Na Mwandishi Wetu,TimesmajiraOnline, Kahama

SERIKALI ya Rais Samia Suluhu Hassan, imedhamiria kutekeleza kwa dhati Sera ya uongezaji thamani ya madini ndani ya nchi kwa kutengeneza bidhaa zitokanazo na madini ghafi.

Katika kutekeleza azima hiyo imetenga eneo maalumu la ukanda wa kiuchumi (Buzwagi Special Economic Zone) katika eneo la ekari 1, 333 kwa ajili ya ujenzi wa viwanda vya kuongeza thamani madini na uzalishaji wa bidhaa za migodini, ambapo awali palikuwa pakifanyika shughuli za uchimbaji madini kupitia Kampuni ya Madini ya Barrick.

Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, aliyasema hayo juzi mkoani Shinyanga, Wilaya ya Kahama wakati wa uzinduzi wa Kituo cha Mafunzo cha Barick – Buzwagi Academy ambacho kitakwenda kutoa mafunzo mbalimbali ya kuongeza uelewa na maarifa katika masuala muhimu ya kwenye Sekta ya Madini.

“Moja kati ya maelekezo ya Rais ni kuhakikisha madini yetu yanaongezewa thamani nchini na kuongeza fursa za ajira kwa Watanzania, kuongeza ujuzi kwa nguvu kazi na kuchochea upatikanaji wa mapato ya nchi na hapa Buzwagi, ndio panakwenda kuleta mabadiliko makubwa,” alisema Mavunde.

Mwitikio wa ujenzi wa viwanda katika eneo hili umekuwa mkubwa na husasan katika viwanda vya kuongeza thamani madini na uzalishaji wa bidhaa za migodini ambazo awali nyingi zilikuwa zinanunuliwa nje ya nchi na sasa kupitia viwanda hivi zitapatikana hapa nchini.

Viwanda vitakavyokuwepo kwa awamu ya kwanza ni kiwanda cha usafishaji na uongezaji madini thamani (Multi Metals Facility) ambacho kipo chini ya Kampuni ya Tembo Nickel, Steel Balls Manufacture – Oriental Grinding Media (China), Mine Conveyors Belts – East Africa Conveyers Services, Solar Farms – Voltalia Ltd and SSI Energy Underground Wiremesh – Wireforce South Africa na Portable Water Plant chini ya Kampuni ya City Engineering.

Awali, Mkuu wa Wilaya wa Kahama, Mboni Mhita, aliipongeza na kuishurkuru Kampuni ya Barick kwa uwekezaji wa kipekee katika eneo la Kahama pamoja na ushirikiano mzuri baina ya Serikali na Kampuni ya Barick na kusema kwamba hatua hizi za makusudi zitasaidia kuchochea uchumi wa wilaya ya Kahama ambao baada ya mgodi wa Buzwagi kufungwa ulidorora.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Barick Dkt, Mark Bristow, alieleza kuwa Kampuni yao inaunga mkono juhudi za Serikali za uongezaji thamani madini na ushiriki wa wazawa kwa kuwekeza kwenye elimu ya vijana kama vile kituo cha mafunzo kwa wadau wa madini cha ‘Barick Academy’ ambacho kinatarajiwa kutoa mafunzo kwa watu 1024 kwa mwaka 2024, akaongeza pia wapo mbioni kuwapa nafasi za juu za uendeshaji migodi hapa nchini hiyo kwa watanzania.

Naye, Mbunge wa Kahama Mjini, Jumanne Kishimba, aliiomba Kampuni ya Barrick kuandaa mafunzo mafupi kwa wachimbaji wadogo kuwafundisha usimamizi na uendeshaji wa biashara ya madini na hasa dhahabu kwa kuwa wananchi wengi ambao ni wachimbaji hawana uelewa mkubwa wa biashara ya madini.