Atoa bil. 1.6 kukarabati miundombinu, na kuanza kwa ujenzi wa Mradi wa Miji 28
Na Yusuph Mussa, TimesMajira Online, Korogwe
MJI wa Korogwe uliopo katika Halmashauri ya Mji Korogwe mkoani Tanga umekuwa kwenye changamoto ya uhaba wa maji safi kwa miaka mingi huku wananchi wakijiuliza, kulikoni kuna vyanzo vingi vya maji ikiwemo Mto Pangani ambao umepita katikati ya mji huo, lakini bado maji yanapatikana kwa shida.
Jitihada mbalimbali zimekuwa zikifanywa na Serikali ili kuona kero ama changamoto hizo za upatikanaji wa maji safi zinatatuliwa, lakini sasa kero hiyo inakwenda mwisho baada ya Rais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kuonesha nia ya dhati ya kumaliza hilo tatizo baada ya kutoa sh. bilioni 1.6. kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu ya maji, na kuanza kwa utekelezaji wa Mradi wa Miji 28, mradi ambao utatatua changamoto ya maji kwa asilimia 100.
Fedha hizo zitaweza kujenga chanzo cha maji cha uhakika kutoka Mto Mashindei, na kufanya ukarabati mkubwa wa mabomba kwenye Mji wa Korogwe ambapo miundombinu hiyo imechakaa kwa kukaa zaidi ya miaka 50 bila kufanyiwa ukarabati mkubwa.
Mwandishi wa makala haya amefuatilia miaka miwili ya uongozi wa Awamu ya Sita wa Rais Dkt. Samia kwenye Sekta ya Maji katika Mji wa Korogwe, ambapo ameweza kutoa fedha kwenye miradi mitatu, na kati ya hiyo, miradi miwili imekamilika, na mmoja unaendelea kutekelezwa.
Na ili kujua kaza zilizofanywa kwa kipindi cha miaka miwili ya Dkt. Samia, mwandishi wa makala haya ameweza kuzungumza na Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Korogwe (KUWASA) Sifael Masawa, ambapo kupitia Mamlaka hiyo, Serikali imetoa fedha hizo ili kutatua tatizo la maji kwenye Mji wa Korogwe.
Masawa anasema kabla ya kuanza Mradi wa Maji Mashindei kwa ajili ya kuongeza maji katika Mji wa Korogwe, tayari Serikali ya Awamu ya Sita kupitia Mfuko wa Maji wa Taifa (NWF) ilitoa sh. milioni 719 kwa ajili ya Mradi wa Maji Bagamoyo.
Anasema Mradi wa Maji Bagamoyo una tenki moja lenye ujazo wa lita 225,000, una vilula tisa, mtandao wa mabomba wa zaidi ya kilomita 20, na unahudumia kata za Bagamoyo na Kilole, na mradi utahudumia wakazi zaidi ya 10,000. Mradi huo umekamilika Julai, mwaka 2022, na umekamilika kwa asilimia 100, huku chanzo chake cha maji ikiwa ni Mto Pangani na kisima kirefu.
Masawa anasema KUWASA pia ilipatiwa sh. milioni 498 kupitia fedha za UVIKO 19 kwa ajili ya kufanya ukarabati wa Mradi wa Maji kutoka chanzo cha Mto Mbeza ili kupeleka maji hayo kwenye matenki ya Kwamkole.
Kazi zilizofanyika kwenye mradi huo ambao umejengwa kwa kutumia Mkandarasi, ni kuweka bomba za plastic (uPVC) zenye kipenyo cha inchi sita urefu wa kilomita 6.4, huku chanzo cha maji kikiwa cha mtiririko.
Pia fedha hizo zilitumika kufanyia ukarabati tenki lenye ujazo wa lita 90, na mradi huo utanufaisha wananchi 20,000 wa Kata ya Mtonga kwenye mitaa ya Kwamkole, Mtonga Juu, Mtonga Chini na Msambiazi. Mradi huo ulianza Novemba 28, 2021 na kukamilika Juni, 2022, na umekamilika kwa asilimia 100.
Mradi wa Maji Mashindei chanzo chake cha maji ni cha mtiririko, na moja ya kazi zitakazofanyika ni kujenga Intake (banio/dakio la maji), ulazaji wa bomba la inchi sita kwa mtandao wa mabomba wa kilomita tisa.
Pia, ukarabati mkubwa wa mabomba na miundombinu chakavu katikati ya Mji wa Korogwe katika Kata ya Manundu, Mtonga (Kwamkole), Old Korogwe na Majengo, ambapo kutawekwa mtandao wa mabomba wa kilomita 24.9.
Mradi huo ukikamilika, utatumia matenki ya Kwamkole, ambapo matenki hayo moja lina ujazo wa lita 90,000 na jingine lina ujazo wa lita 225,000, hivyo kuweza kusambaza maji kwenye Mji wa Korogwe na viunga vyake.
“Kilio cha wananchi wa Mji wa Korogwe, ni uhaba wa maji. Na Serikali imekuwa ikifanya jitihada za upatikanaji wa maji kwenye mji huu kwa njia mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutoa maji Mto Pangani kwa kutumia pampu, eneo la Mtonga na Old Korogwe.
“Lakini pamoja na jitihada hizo, bado maji hayo yameshindwa kukidhi mahitaji, na hiyo ni kutokana na uchakavu wa miundombinu ya maji hasa mabomba, ambapo kwa uchakavu huo, kipenyo cha kupitisha maji kwenye bomba kimepungua. Hivyo, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ametupatia sh. bilioni 1.6 ili kujenga chanzo na kufanya ukarabati mkubwa wa mabomba na miundombinu mingine katikati ya Mji wa Korogwe” alisema Mkurugenzi Masawa.
Masawa anasema Mradi wa Maji Mashindei unajengwa na mkandarasi Frangem International Ltd wa mkoani Dar es Salaam, na tayari ujenzi umeanza Februari, mwaka huu, na mkandarasi huyo ameanza ujenzi wa Intake (banio/dakio la maji), na ujenzi huo umefikia asilimia 30, na utekelezaji wake ni wa miezi sita.
“Mradi wa Maji Mashindei unajengwa na mkandarasi Frangem International Ltd wa Dar es Salaam, na tayari ameanza ujenzi wa Intake, na ujenzi huo umefikia asilimia 30. Na katika sh. bilioni 1.6 za ujenzi huo wa mradi, tayari tumepokea sh. milioni 481. Na kati ya fedha hizo sh. bilioni 1.6, zitatumika kufanya ukarabati wa uchakavu wa mabomba katikati ya Mji wa Korogwe, na ukarabati huo ni mtandao wa mabomba kwa kilomita 24.9” alisema Masawa.
Masawa anasema, pamoja na changamoto za maji kwenye Mji wa Korogwe, bado kuna jitihada zinafanyika kuona wananchi wanapata maji hata kwa mgao, ambapo Mradi wa Maji Mtonga unahudumia Kata ya Mtonga na baadhi ya maeneo ya Kata ya Majengo eneo la Memba nao wakipata maji.
Anasema maeneo yanayopata maji kupitia chanzo cha Mtonga ni Mitaa ya Mtonga Chini, Mtonga Kati, Mtonga Juu, Msambiazi, Kwamkole na Memba, huku akielezea wanalazimika kufanya mgao kutoka na ukame ulioikumba Wilaya ya Korogwe kwa miaka miwili.
“Mradi huu unasaidia sana nyakati za kiangazi kwa vile mradi wake unatumia pampu, na chanzo chake ni cha uhakika kutoka Mto Pangani. Mradi unazalisha maji wastani wa lita 60,000 kwa saa, lakini kutokana na changamoto za umeme kuwa mdogo, uzalishaji haufanyiki kwa masaa yote 24 kwa siku. Mradi unahudumia zaidi ya wakazi zaidi ya 15,000.
Pia kuna mradi wa Kwasemangube unaohudumia kata ya Magunga pamoja na sehemu ya eneo la Zung’nat, Miradi mingine ni mradi wa Maji Kwamndolwa unaohudumia vijiji vya Kwameta na Kwamndolwa, mradi wa Maji wa Kwakombo na Kwamsisi, na mradi wa Maji Mgombezi unaohudumia kata yote ya Mgombezi.
Kutokana na changamoto ya ukame wa muda mrefu uliojitokeza na kufanya chanzo cha maji ya mtiririko kukauka, Serikali imeleta Mtambo wa kuchimba visima saba kwa ajili ya kukabiliana na changamoto ya maji. Mtambo huo ni kati ya mitambo 25 iliyonunuliwa na Serikali ya Awamu ya Sita ya Dkt. Samia. Kuletwa kwa mtambo huo ni jitihada za Mbunge wa Jimbo la Korogwe Mjini Dkt. Alfred Kimea kwa ajili ya kukabiliana na tatizo la maji kipindi cha kiangazi. Kwa sasa vimeshachimbwa visima viwili katika maeneo ya Magunga na Majengo.
More Stories
Ubunifu wa Rais Samia kupitia Royal Tour unavyozindi kunufaisha Tanzania
Rais Samia anavyojenga taasisi imara za haki jinai kukabilina na rushwa nchini
Rais Dk. Samia alivyowezesha Tanzania kuwa kinara usambazaji umeme Afrika