December 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Samia kukuza uchumi kwa kasi, kipaumbele miradi ya kimkakati

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema, azma ya Serikali anayoiongoza ni kuhakikisha inakamilisha na kuiratibu vyema miradi yote ya kimkakati iliyoanzishwa na inayoendelea kutekelezwa sambamba na kuhakisha uchumi wa nchi unakuwa kwa kasi.

Mipango hiyo imewafanya Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa kuazimia na kutoa tamko la kumpongeza Rais Samia na Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Dkt. Husein Ali Mwinyi kwa kazi nzuri wanayoifanya katika kuiongoza nchi na kusimamia utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM 2020 – 2025.

Akizungumza Mkoani Dodoma baada ya kutoka katika kikao cha kawaida cha Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, chini ya Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi na Rais wa Samia Suluhu Hassan katika ukumbi wa White House Dodoma, Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa Itikadi na Uenezi,Shaka Hamdu Shaka amesema, wajumbe wa Halmashauri Kuu wamebainisha kuwa, toka nchi ilipopata msiba mkubwa wa kuondokewa na aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli, ndani ya siku 100 za uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan ambapo ametoa na kuonyesha dira ya serikali anayoiongoza.

Shaka amesema, wajumbe hao wanaona serikali ya awamu ya sita inazingatia uadilifu, Utawala wa Sheria, Haki, Usawa, kuimarisha misingi ya demokrasia, umoja na mshikamano zaidi kuendelea kutunza amani na usalama wa nchi.

“Miradi yote iliyopo kwenye maeneo yenu viongozi wa CCM mnao wajibu wa kuifatilia, kuikagua na kujua uendelevu wake bila uwoga kwani huo ni wajibu wenu wa msingi katika kutusimamia Serikali, hilo liende sambamba na kuhakikisha mnasaidia kuona mapato ya Serikali hayapotei katika vyanzo vyote vya ukusanyaji, ikumbukwe ninyi ndio kioo cha kutumurika, kwavile ilani inayotekelezwa ni ya Chama Cha Mapinduzi lazima ifanikiwe kwa kiwango kikubwa,” amesema Shaka kwa niaba ya Mwenyekiti wa Chama hicho, Samia Suluhu Hasasan.