February 6, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Samia: Dunia imetambua kazi kubwa tunayoifanya

Na Mwandishi Wetu,Timesmajiraonline, Dodoma

RAIS Dkt. Samia Suluhu Hassan amewasili na kupokelewa kwa kishindo viongozi mbalimbali pamoja na wananchi kwenye uwanja wa ndege wa Dodoma akiwa na Tuzo Maalum ya Kimataifa ya The Global Goalkeeper Award.

Tuzo hiyo hutolewa kwa viongozi waliowezesha nchi zao kuharakisha maendeleo kuelekea kufikia malengo ya maendeleo endelevu.

Rais Samia amepewa Tuzo hiyo katika kipengele cha mapambano dhidi ya vifo vya akina mama wajawazito na watoto wachanga chini ya umri wa miaka mitano.

Akizungumza mara baada ya kuwasili jijini Dodoma, Rais Samia alisema tuzo hiyo ina maana kubwa sana , Dunia imejua jitihada zetu katika kuleta huduma za afya.

“Sio tu huduma za afya kwa ujumla lakini pia kwa mama na mtoto, kama mnavyojua miaka minne iliyopita vifo vya akina mama wakati wa kujifungua vilikuwa vinafikia 556 kati ya 100,000 wanaojifungua.

Hiyo ni nusu kwa nusu, nusu wanakufa, nusu wanapona, lakini kwa kuwa tumefanya uwekezaji mkubwa kwenye afya, uwekezaji kwenye kujenga majengo, uwekezaji kwenye kununua vifaa vya tiba, uwekezaji katika kusomesha madaktari na wafanyakazi wengine, kuajiri wafanyakazi wa afya ya msingi tumeweza kupunguza vifo vya akina mama na watoto,” alisema Rais Samia na kuongeza;

“Kwa akina mama tumeweza kupungumza vifo 556 hadi 104 kwa vizazi 100,000 .

Lakini lengo tuliloelekezwa na malengo ya dunia inapofika 2030 tuwe na vifo 70 tu, sasa tuna 104 ikifika 2020 tutafikia lengo au tutapita kidogo kwa sababu jitihada zinaendelea.”

Alisema tuzo hiyo sio ya Rais, Rais ni mpokeaji, lakini ni ya wahudumu wa afya kuanzia madaktari , madaktari bingwa, wakunga na wote wanaotoa huduma hiyo ndiyo Tuzo yao.

Alisema tuzo hiyo ina umuhimu mkubwa sana kama Taifa tunashukuru, kwani Tanzania ndiyo taifa la mwanzo kupewa tuzo hiyo kwa kazi kubwa tuliyoiweka katika sekta ya afya.