May 30, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Samia aweka historia,azindua Ujenzi jengo Makao Makuu ya CCM

Samia aweka historia,azindua Ujenzi jengo Makao Makuu ya CCM

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online, Dodoma

KATIKA kilele cha maono ya muda mrefu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa CCM, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameweka jiwe la msingi kuashiria uzinduzi rasmi wa ujenzi wa jengo jipya la kisasa la Makao Makuu ya CCM. 

Ujenzi huo unafanyika katika Kata ya Tambukareli jijini Dodoma, kwa gharama ya shilingi bilioni 34.1.

Akihutubia katika hafla ya uzinduzi, Dkt. Samia ameeleza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa ndoto ya muda mrefu ya chama, ikiwa ni matokeo ya maamuzi ya Halmashauri Kuu ya CCM yaliyofanyika mwaka 2024.

“Ni heshima kubwa kuwa sehemu ya utekelezaji wa ndoto ya muda mrefu.., Leo tunakwenda kuonyesha utekelezaji wa maamuzi ya Halmashauri Kuu ya Chama,” amesema Dkt. Samia.

Akiweka bayana dhamira ya chama kusogeza huduma karibu na wananchi, Dkt. Samia amesisitiza kuwa jengo hilo halitakuwa tu nembo ya chama, bali litatumika pia kama jukwaa la kuwasikiliza wananchi na kufikisha kero zao serikalini.

“Tutumie ofisi za Chama kuwasikiliza wananchi kero zao kisha kuziwasilisha serikalini,” ameongeza.

Jengo hilo linatarajiwa kukamilika kabla ya mwaka 2027, wakati CCM itakapoadhimisha Jubilee ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwake.