Na Penina Malundo,Timesmajiraonline
RAIS Samia Suluhu Hassan amewataka waandishi wa habari na vyombo vya gabari kwa ujumla kuutumia uhuru wa vyombo vya habari kuhabarisha umma na kuweka uzalendo wakati wakifanya kazi zao.
Akizungumza jjana wakati wa hafla ya utoaji Tuzo za Samia Kalamu Awards, Rais Samia alisema,jambo ambalo ameahidi mara kwa mara kwa wanahabari ni kukuza uhuru wa vyombo vya habari nchini na jambo hilo linaonekana wazi.
Aliwapongeza waandishi wa habari nchini kwa hatua waliyofikia ambapo miaka ya nyuma waandishi hao wa habari walikuwa wakikwama na kwa sababu ya kukosa ujuzi na uzalendo.
”Huko nyuma aidha kwa kutokujua au kuona kama tunafanya ndivyo, tulikuwa tunaongoza katika kuandika makala zinazobomoa nchi yetu na kuisema nchi yetu, lakini sasa hivi ukisoma makala nyingi zinajenga nchi yetu,zinasifia nchi yetu zinaeleza ukweli yanayotokea nchini na hata pale mnapoeleza mabovu ni mabovu ambayo yanahitaji kuelezwa ili kila mtu aone na Serikali ione ichukue hatua, kwa hiyo nawapongeza,”alisema.
Alisisitiza neno uzalendo kwa kusema kuwa wenzetu kule nje zile habari ambazo wana uhakika zinaenda kubomoa taifa lao, huzioni katika yombo vyao vya habari na wala hazitoki,lakini wao hao huku kwetu wanataka kujua kila kitu kuhusu kwetu.
Rais Samia alisema na hao wanaotaka kujua kuhusu nchi yetu wanawatumia waandishi wa habari wa Tanzania ili kusema kuna vitu gani.
”Sijui unajisikiaje kuona nchi yako inasemwa na vyombo hivyo vikubwa ulimwengu mzima. Ila kwa sasa hatua tuliyofikia nawapongeza sana waandishi wa habari mmekuwa mkiandika vitu vizuri kuhusu nchi yenu,nawahakikishia Serikali kupitia wizara ya utamaduni,sanaa na michezo ipo pamoja nanyi na tupo tayari kushirikiana nanyi kujenga uwezo wenu,kuondoa changamoto zinazowakabili hatua kwa hatua ili sekta ya habari iendelee vizuri,”alisema.
Akizungumzia suala la kukuza uhuru wa vyombo vya habari,Rais Samia alisema ahadi aliyohaidi ni kukuza uhuru wa vyombo vya habari na sasa takwimu zinasema zenyewe kwamba Tanzania uhuru wa vyombo vya habari ni mkubwa na unakua siku hadi siku.
Alisema kukua kwa uhuru wa vyombo vya habari maana yake si kukosa uzalendo kwa nchi yako hapana ni kuhakikisha unaandika habari zenye uzalendo na kuleta tija.
Alisema pia waandishi wa habari wanapoandika habari zao wanapaswa kuzingatia takwimu pindi wanapotoa taarifa zao hususan ufanywaji wa uchambuzi.
”Kutumia Takwimu kutoa taarifa zao kwani uandishi wa kutumia takwimu una manufaa makubwa kwa jamii na unatoa nafasi kubwa kwa jamii kuona maendeleo yanayofanywa na Serikali,”alisema
Aidha Rais Samia akizungumzia kuhusu matumizi ya lugha sanifu ya Kiswahili, aliwataka waandishi wa habari kutumia lugha vizuri ili taarifa wanazozitoa zieleweke na pia kukuza lugha hiyo hapa nchini na ulimwenguni kwa ujumla.
Alisema ni vema kuwepo kwa kiswahili sanifu ambacho waandishi wa habari wanakitumia ipasavyo ili wananchi wakisikie na kukielewa vizuri.

Akizungumzia agenda ya nishati safi ya kupikia,Rais Samia aliwapongeza waandaaji wa tuzo hizo za Samia Kalamu Awards kutokana na tuzo hizo kuangazia eneo hilo la Nishati Safi ambalo ni ajenda ya Tanzania Kimataifa na kusema amefurahi kuona waandishi wa habari waandikia kuhusiana na sekta hiyo.
Alisema suala la nishati safi ni ajenda ya Tanzania na kilichofanyika kwa wanahabari katika kukuza ajenda hiyo ni jambo ambalo linaonesha uzalendo mkubwa.
”Agenda ya nishati safi itasaidia utunzaji wa mazingira kwani takwimu zinaonesha kuwa zaidi ya hekari laki 4 za misitu zinakatwa ili kupata nishati kwenye maeneo mbalimbali ya nchi,”alisema.
Awali Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Profesa Palamagamba Kabudi aliwaambia waandishi wa habari kuwa uhuru wa kuandika na kutangaza habari unapewa nguvu na Katiba ya 18 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lakini pia Ibara ya 30 katiba hiyo inaweka mipaka ya uhuru huo.
Alisema Ibara ya 30 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano Tanzania imeweka mipaka ya uhuru wa habari kwa kuzingatia Usalama wa Taifa na Maadili ya Tanzania.
Aliwataka waandishi wa habari kufanya kazi zao kwa uhuru, huku wakiongozwa na mipaka ya Uhuru huo ili kuendelea kulinda maadili, utamaduni na Usalama wa Taifa.
More Stories
UAE yamtunuku Rais Samia Medali ya juu kabisa
Rais Samia amteua Mkurugenzi Mtendaji TANESCO
RMO,DMO waagizwa kumsimamia Mkurugenzi ununuzi vifaa ,vifaa tiba