December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Samia aunguruma mkutano nishati safi ya kupikia, ataja vikwazo

Na Mwandishi Wetu, Timesmajiraonline,Paris

RAIS Samia Suluhu Hassan, amesema licha ya Afrika kuwa na idadi kubwa ya watu na raslimari zote muhimu, ni bara la chini kuwa na upatikanaji wa nishati safi ya kupikia.

“Zaidi ya Waafrika milioni 900 wanatumia nishati isiyo safi ya kupikia, jambo ambalo linachangia uharibifu wa mazingira, upotevu wa bioanuai na athari za kiafya,” alisema.

Rais Samia ameyasema hayo jana jijini Paris, nchini Ufaransa wakati akihutubia mkutano wa viongozi, wadau na washiriki wa mkutano wa kimataifa wa nishati safi, akiwa mwenyekiti mwenza wa mkutano huo na Rais kinara wa nishati ya safi ya kupikia.

Amesisitiza kwamba nishati safi ya kupikia ina maeneo matatu yanayokwamisha matumizi yake, kwanza ikiwa ni maeneo ya vijiji ambapo watu wa vijijini wana uwezo mdogo kutokana na gharama kubwa za nishati hiyo na uhaba wa upatikanaji wake.

Pili, amesema ni Ulimwengu kwa ujumla kutolipa kipaumbele suala la matumizi ya nishati safi ya kupikia, ufadhili mdogo, na watu kutojua fursa za kiuchumi zilizopo katika nishati ya kupikia , hivyo kurudisha nyuma harakati hizo.

Tatu, Rais Samia amesema ni kutokuwepo kwa ushirikiano wa kuhakikisha nishati safi ya kupikia inapatikana kwa wote, hivyo alisisitiza upatikanaji, uwepo kwa upatikanaji wa nishati safi ya pikia, gharama ndogo na suluhu zinazotekelezeka.

Aidha, Rais Samia amesema kuongezeka kwa upatikanaji wa nishati safi ya kupikia kutasaidia wanawake kupata fursa zaidi ya kushiriki katika shughuli za kiuchumi, kupunguza umaskini na kuleta usawa wa kijinsia.

Amesema licha ya changamoto hizo, Tanzania ina dhamira ya kutekeleza mkakati wa taifa wa nishati safi ya kupikia uliozinduliwa hivi karibuni uliokusudia kufikia asilimia 80 ya Watanzania wanaotumia nishati hiyo ifikapo mwaka 3034.

Mkutano huo umehudhuriwa na watu zaidi 1,000 wakiwemo marais, viongozi mbalimbali, asasi za kiraia, watu mashuhuri wenye ushawishi kwenye masuala ya nishati safi na wadau wengine.

Malengo ni kuhakikisha Afrika inaenda mbali kupata uelewa lakini pia kuhakikisha matumizi ya nishati safi ya kupikia yanaongezeka, kuandaa sera madhubuti inayotekelezeka kwa ajili ya nishati safi ya kupikia na kuharakisha ushirikiano wa wadau katika suala hilo.