December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Samia atua Kariakoo, ashuhudia yaliyojiri

Aridhishwa na kazi ya uokoaji ilivyofanyika, asisitiza ukaguzi wa maghorofa Kariakoo, asema Tume ikitushauri tubomea, hatutasita

Na Mwandishi Wetu,TimesmajiraOnline, Dar

RAIS Samia Suluhu Hassan, amerejea nchini akitokea Brazil alipokuwa kwa ajili ya kuhudhuria mkutano wa G20 na kwenda moja kwa moja kujionea hali ya ghorofa lililoporomoka na kusababisha vifo vya watu 20 hadi jana saa tatu, huku wengine zaidi ya 85 wakinusurika.

Aidha, Rais Samia alienda Hospitali kuwajulia hali majeruhi. Akizungumza na wananchi Rais Samia alipongeza juhudi zilizofanyika wakati wa uokoaji.

“Kazi iliyokuwa ikifanyika hapa lengo letu ilikuwa ni kuwanusuru wenzetu waliokuwa wamenasa.

Pamoja na jitihada zilizofanywa na Serikali kuna wenzetu 20 hadi saa tatu asubuhi leo (jana) wamepoteza maisha.

Kwa wale manusuru bado Mungu ana kazi nao wasisosonoke,” alisema Rais Samia.
Alisema tukio hilo lilitokea akiwa safarini kuelekea kwenye mkutano wa G20 na leo amefika kushuhudia mwenyewe.”

Alisema baada ya kuliona janga, nimeona lilikuwa kubwa na la kutisha. Rais Samia alisema ameona ari ya umoja wa Watanzania tunapopatwa na majanga kama ilivyokuwa kule Hanang .

“Kila janga linapotokea tumeona Watanzania wanavyojitoa kusaidia kazi iliyofanywa hapa ni kubwa na kwa ushirikiano na weledi mkubwa, ninawashukuru wote mlioshiriki katika zoezi hili,” alisema Rais Samia na kuongeza;

“Tukio hili limetupa ujumbe mkubwa wa kuangalia usalama wa majengo yetu ya Kariakoo, ukiangalia jengo lilivyojengwa na nondo zile, halikuwa jengo imara.”

Alizidi kusema kuwa; “Tuingie Kariakoo kuangalia majengo yetu, nilipokuwa nje niliagiza Waziri Mkuu aunde Tume, ameniambia tayari ameunda timu ya watu 20.

Alisema taarifa ya Tume hiyo itawekwa bayana kwa Watanzania. “Kama itatushauri tubomoe majengo yasiyotufaa, hatutasita kufanya hivyo,” alisema.

Alisema miaka ya nyume kulishafanyika ukaguzi wa maghorofa hayo na Tume zilifanya uchanguzi na ripoti hizo na zenyewe zitasaidia.

Alisema ukiangalia kwa macho unaona kuna upungufu wa kiutendaji, bila shaka jengo halikupata vibali, na jengo hilo halikutazamwa ubora wake wakati wa ujenzi.

“Wote kwa pamoja tusema matukio kama haya yasijirudie.”

Aidha Rais Samia ameruhusu kufunguliwa kwa shughuli za biashara kwa maeneo ambayo yapo mbali na jengo lililoporomoka.

” Kwa yale maeneo ambayo yako mbali wananchi waendelee kufanya shughuli zao, lakini kwa eneo hili naomba shughuli zifunguliwe watu wasiwe karibu,” alisema.

Aliwashukuru waziri mkuu, mkuu wa mkoa timu zote za Serikali, sekta binafsi kwani nayo imetoa mchango mkubwa sana.

Alishukuruku vyombo vya ulinzi na usalama na hospitali zote zilizotoa huduma bure, akisisitiza kwamba huo ndiyo Utanzania.

Aidha, Rais Samia aliagiza jengo hilo liendelee kufukuliwa ndani kuona kama kuna wanadamu wenzetu ili watolewe.

Aidha, alishukuru wananchi kwani hakuna aliyetaka kuchukua mali zilizokuwepo kwenye jengo hilo.

Aliagiza mali zihifadhiwa mahali na wenye mali wataitwa baadaye kwenda kutambua mali zao.