January 11, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Samia atoa maelekezo majeruhi ajali Arusha

Na Mwandishi Wetu,TimesmajiraOnline,Arusha

RAIS Samia Suluhu Hassan, ameagiza majeruhi 21 wa ajali iliyoua watu 25 juzi jijini Arusha wapatiwe matibabu bila kulipia gharama zozote.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel, alipotembelea na kuwajua hali majeruhi wa ajali hiyo waliolazwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mount Meru.

“Rais Samia Suluhu Hassan ametuelekeza majeruhi wote wa ajali hii kupatiwa matibabu bila kulipa gharama zozote,” amesema Dkt. Mollel.

Dkt. Mollel amesema majeruhi wote wanaendelea vizuri na mmoja ndiye amepewa Rufaa ya kwenda hospitali ya Rufaa ya Kanda KCMC Mkoani Moshi.

Katika hatua nyingine Rais Samia Suluhu Hassan ametuma salamu
za rambirambi kwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongella kufuatia vifo vya watu 25 na majeruhi 21 vilivyotokea katika ajali hiyo.

“Rais Samia anawapa pole majeruhi wa ajali hiyo pamoja na wafiwa wote na anaungana na familia hizo katika kipindi hiki kigumu cha majonzi. Mwenyezi Mungu azilaze roho za marehemu wote mahali pema Peponi,” imeeleza taarifa ya Ikulu.

Kwa upande wake mmoja wa majeruhi Raia wa Togo, Apelo Apeto (32) ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa ubora wa huduma waliompatia na anayoendelea kupatiwa hospitalini hapo.

“Kwa ajali hii ningekuwa nchini kwetu tayari ningekuwa nimepoteza maisha, kwani kule bila kilipia huduma za matibabu hupatiwi huduma, lakini kwa Tanzania walivyowakarimu na weledi wameweza kuokoa maisha yangu mpaka sasa naendelea vizuri na naweza kuongea,” amesema raia huyo wa Togo

Raia huyo amesema alikuja nchini kwa semina ya mafunzo ya uongozi iliyokuwa ikifanyika mkoani hapo na baadaye walienda kufanya utalii wa kuangalia kabila la wamasai wakati wanarudi ndipo wakapata ajali hiyo.

Wakati huo huo idadi ya waliokufa kwenye ajali hiyo imeongezeka na kufikia watu 25, huku 21 katika ajali iliyotokea maeneo ya Ngaramtoni Kibaoni by Pass ikihusisha Lori na magari mengine madogo matatu Wilaya ya Arumeru Mkoa wa Arusha.

Akitoa taarifa ya ajali hiyo Kamishna wa Polisi Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi, CP Awadhi Juma Haji alipofika katika hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Arusha Mount Meru amesema ajali hiyo ilitokea Februari 24,2024 muda wa saa 11:00 jioni katika Barabara ya Arusha Namanga ambapo ilihusisha lori lenye namba za usajili KAC 943 H aina ya Mack lenye tela namba za usajili ZF 6778 mali ya kampuni ya KAY Construction ya Nairobi Nchini Kenya.

CP Awadhi ametaja idadi ya waliofariki katika ajali hiyo kuwa ni wanaume ni 14 na wanawake 10 na mtoto mmoja wa kike ambao wanafanya jumla ya waliokufa kuwa ni 25.

Raia wa kigeni waliofariki wanatoka mataifa Kenya, Togo, Madagascar, Burkina Faso, Afrika ya Kusini, Nigeria na Marekani.
Kwa upande wa majeruhi raia wa kigeni wanatoka mataifa ya Idadi ya majeruhi ni 21 wakiwemo raia wa kigeni kutoka mataifa ya Nigeria, Ivory Coast, Uswizi, Cameroon, Uingereza, Mali na Hawaii.

Katika ajali hiyo pia CP Awadhi alitaja idadi ya majeruhi kuwa ni 21 kati yao wanaume ni 14 na wanawake ni saba.

Ametaja magari yaliyopata ajali katika tukio hilo kuwa ni T 623 CQF aina ya Nissan Caravan, T 879 DBY aina ya Mercedes Benz Saloon na gari namba T 673 DEW aina ya Toyota coaster mali ya shule ya (New Vision).

Pia kamishna huyo wa opereshini na mafunzo ya Jeshi la Polisi nchini amekitaja chanzo cha ajali hiyo kuwa ni kufeli breki ya lori kitendo kilichopelekea kuyagonga magari mengine yaliyokuwa mbele yake.

Amesema Jeshi hilo linaendelea kumtafuta dereva aliyesababisha ajali hiyo ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yake.

Sambamba na hilo ametoa Pole kwa wananchi wa Mkoa wa Arusha na watanzania kwa ujumla na raia wa kigeni waliopoteza ndugu zao katika ajalii hiyo.