September 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Samia atoa maelekezo kuhusu sekta ya afya

*Ataka kufahamu nguvu kazi iliyopota nje ya vituo vya tiba, ikiwemo kwenye soko la ajira, aagiza ukamilishaji utafiti wa wataalam wa afya, apongeza Benki ya NBC uendelezaji sekta hiyo

Na Mwandishi Wetu,Timesmajiraonline,Dar

RAIS Samia Suluhu Hassan, ametoa maelekezo kadhaa ikiwemo kuitaka Wizara ya Afya kukamilisha utafiti wa kitaifa kubainisha hali halisi ya wataalamu wa afya nchini waliopo kwenye sekta ya ajira.

Rais Samia alitoa agizo na maelekezo mengine wakati wa kilele cha Kumbukizi ya Tatu ya Urithi wa Benjamin Mkapa katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es Salaam jana, ambapo alikuwa mgeni rasmi.

“Tungependa kufahamu nguvu kazi ya afya iliyo nje ya vituo vya tiba ikiwemo kwenye soko la ajira,” alisema Rais Samia.

Aidha, Rais Samia aliitaka Ofisi ya Waziri Mkuu kuimarisha timu ya uratibu wa rasilimani ya sekta ya afya inayojumuisha Wizara ya Afya, TAMISEMI, Utumishi, Wizara ya Elimu , Wizara ya Fedha na wawakilishi wa sekta ya binafsi ili iweze kufanya kazi zake ipasavyo.

Pia, Rais Samia aliagiza kufanyike kwa vikao vya mabaraza kitaaluma ili wajue jinsi wakatavyoweza kumeza nguvu kazi iliyo nje na mahitaji halisi yaliyopo ndani ya nchi . Kuhusu maslahi ndani ya sekta ya afya, Rais Samia alisema wataendelea nalo polepole.

“Tutapunguza leo hiki, kesho hiki , sitaki kuahidi kwamba tutayaangalia yote kwa mwaka mmoja, lakini niseme tunathamini kazi yenu, tunajua ugumu wa kazi yenu na tutaangalia maslahi yenu,” alisisitiza Rais Samia.

Kwa upande wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Raisa Samia aliagiza washirikiane na Wizara ya Afya kutengeneza mkakati wa diplomasia ya afya na kusaidia upatikanaji wa nafasi za mafunzo ya utaalamu kwa watumishi wa sekta ya afya ikiwemo vyuo vikuu vya sayansi ya tiba ya afya vya nje.

Kadhalika Rais samia aliwataka wataalamu wa afya wa pande zote mbili za Muungano wawe wanakutana mara kwa mara kujadili mambo au changamoto za afya zilizopo na jinsi ya kwenda pamoja

Rais Samia aliitaka wizara ya afya kujifunza kwa wenzao Zanzibar namna ya ubia kati ya Serikali na sekta binafsi inavyoweza kuongeza ufanisi ndani ya sekta ya afya na mahospitalini. “Wenzetu wameanza twende tujifunze wameanza vipi, tuweke kwenye maizngira ya kwetu ili huduma ziende haraka na huduma bora kwa watanzania

Wakati huo huo, Rais Samia Suluhu Hassan, amepongeza jitihada za Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) kwa kuendeleza sekta ya afya hapa nchini kupitia huduma za kibenki pamoja program zake mbalimbali zinazolenga kuboresha sekta hiyo muhimu.

Zaidi Rais Samia ameiomba benki hiyo kuangalia namna itakavyoweza kusaidia ufadhili wa masomo ya wataalamu wa afya kwa Watoto wenye hali usonji nchini ili kukabiliana na uhaba wa wataalamu hao.

Rais Samia ametoa pongezi hizo jana jijini Dar es Salaam wakati akihitimisha Kongamano la Rasilimali Watu wa Sekta ya Afya lililoandaliwa na Taasisi ya Benjamin Mkapa (BMF) katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam na kuhudhuliwa na wadau mbalimbali wa sekta ya afya pamoja na viongozi waandamizi wa kitaifa akiwemo Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Dkt Hussein Ally Mwinyi, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu na viongozi wengine wa serikali wakiwemo wastaafu.

Akizungumza kwenye hafla hiyo, Rais Samia alionesha kuvutiwa na jitihada za benki ya NBC katika kuhudumia wadau mbalimbali wa sekta ya afya kupitia mikopo isiyo na riba sambamba na kufadhili programu mbalimbali kwenye sekta hiyo ikiwemo ile ya ufadhili wa masomo kwa wakunga 100 inayotekelezwa na benki hiyo kwa kushirikiana na Taasisi ya Benjamin Mkapa.

“Nimefurahishwa na jitihada za NBC ambao wametoa katika hisani yao kurudisha kwa wananchi na ndio waliosomesha wale wakunga 100 kwa kushirikiana na Taasisi ya Benjamin Mkapa…sasa niwaombe jitihada hizi ziendelee zisiwe za mwaka mmoja.

Niwaombe sasa muwekeze kwenye kusomesha wataalamu kwenye fani ambazo taasisi na Wizara wataona zinastahili zaidi. Tumeskia Waziri wa Afya amesema kuna uhaba wa wataalamu kwenye eneo la watoto wetu wenye hali ya usonji naomba sasa NBC mjielekeze kusomesha hao wawe wengi,’’ alisema Rais Samia.

Pongezi hizo za Rais Samia zimekuja siku moja tu baada ya pongezi kama hizo kutolewa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alipotembelea banda la Maonesho ya huduma za benki hiyo mahususi kwa wadau wa afya lililopo kwenye viunga vya mkutano huo.