January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Samia atangaza Tanzania kumuunga mkono Odinga

Ni katika kinyang’anyiro cha nafasi ya Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja
wa Afrika (AU), ahudhuria uzinduzi wa kampeni zake Ikulu, nchini Kenya

Na Mwandishi Wetu, Timesmajiraonline,Kenya

RAIS Samia Suluhu Hassan, amesema Tanzania inamuuunga mkono Waziri Mkuu Mstaafu wa Kenya Raila Odinga anayewania nafasi ya Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AU).
 
Rais Dkt. Samia amesema hayo jana wakati akishiriki uzinduzi wa kampeni ya
kumnadi Mgombea huyo kwenye hafla iliyofanyika Ikulu ya Nairobi.

Hafla hiyo imehudhuriwa pia na Rais wa Uganda, Yoweri Museveni,
Rais wa Sudan Kusini, Salva Kiir Mayardit, Waziri Mkuu wa Jamhuri
ya Burundi, Gervais Ndirakobuca na viongozi wengine.

Aidha, Rais Dkt. Samia ameeleza kuwa Watanzania wanamfahamu Odinga
kama mwanamajumui wa Afrika anayeamini katika mtangamano wa Afrika na
manufaa yake.

Kwa upande mwingine, Rais Dkt. Samia amempongeza Odinga kwa
kudumisha mahusiano mazuri na Viongozi wa Afrika na wabia wake.
 
Rais Dkt. Samia amemuelezea, Odinga kama kiongozi mwenye busara na mwenye uwezo wa kujenga Umoja wa Afrika thabiti, unayochochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii ya bara la Afrika na yenye uwezo wa kutetea maslahi ya Afrika
kimataifa.