September 28, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kamati ya kukwamua mchakato wa Katiba kuundwa

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Dar es Salaam

RAIS Samia Suluhu Hassan ametangaza kuunda Kamati ya Watanzania itakayoishauri Serikali namna ya kukwamua mchakato wa Katiba kwa kuelekeza namna ya kwenda na suala hilo.

Rais Samia alitoa kauli hiyo Ikulu, jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na viongozi wa vyama 19 vya siasa vyenye usajili wa kudumu.

“Kwenye suala la Katiba, Tunataka kuanza na Kamati itakayokuja kutushauri. Katiba hii ni ya Watanzania. Tunaunda Kamati ya Watanzania wote ya kutushauri ni namna gani twende . Kwenye Kamati hii kutakuwa na wawakilishi kutoka sehemu mbalimbali.

Watakuwepo wanasiasa, wawakilishi wa vyama vya kiraia, wawakilishi wa vyombo vya kiraia, wawakilishi wa jumuiya za kimataifa.

Tutakuwa na uwakilishi kutoka sehemu zote. Kwa hiyo madai ya Katiba ya muda mrefu sasa yanakwenda kukwamuka na kufanyiwa kazi. Tutakuwa na kamati itakayofanyakazi kwa kupewa hadidu za rejea.

Hatutakuwa na Kamati ya lile vuguvugu. Tunataka wakati vuguvugu hilo linaendelea nchi inaendelea na shughuli zake za maendeleo. Tusipojenga vituo vya afya, barabara mtakuja kunipiga kelele, watu hawawezi kula Katiba…lazima shughuli zingine ziendelee,” alisema Rais Samia.