November 18, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Samia aridhishwa juhudi  uokoaji Kariakoo, atoa maelekezo

*Asema  waliokolewa  ni 84  hadi jana, Serikali kugharamia matibabu yao,  waliofariki kustiriwa ipasavyo

Na Jackline Martin, Time

RAIS  Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema  hadi kufikia saa nne jana asubuhi 

watu 84 wameokolewa na kufikishwa hospitali kupatiwa matibabu katika tukio  la kuporomoka  kwa  ghorofa, Kariakoo, jijini Dar es Salaam.

Kati ya hao , amesema mejeruhi 26 bado wanaendelea na matibabu na 13   wamepoteza  maisha.

Rais Samia .alitoa takwimu hizo jana wakati akitoa salamu Jijini Rio de Janeiro nchini Brazil ambako yupo kwa ajili ya kushiriki Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa nchi Wanachama wa Kundi la G20 unaotarajiwa kuanza leo 

Rais Samia alisema Serikali itabeba gharama za matibabu kwa wote waliojeruhiwa na kuhakikisha waliofariki wanasitiriwa .

Alisema hadi sasa sababu za kitaalamu za jengo hilo kuporomoka bado hazijachunguzwa na kubainishwa ,kwani kipaumbele kwa sasa kilikuwa ni kuwaokoa wananchi waliokuwa ndani ya jengo hilo.

 Rais Samia amemtaka Waziri Mkuu aongoze timu ya wakaguzi  waendelee na zoezi la kukagua eneo lote la Kariakoo na kupata taarifa kamili ya hali ya majengo  ilivyo

Pia amelitaka Jeshi la Polisi kupata taarifa kamili kwa mmiliki wa jengo lililoporomoka jinsi  ujenzi ulivyokuwa ukifanyika.

Rais Samia ametoa pole kwa ndugu, jamaa na marafiki walioguswa na tukio hilo huku akiwaomba Watanzania wote kuwaweka kwenye maombi watu wote

Walioathirika na tukio hilo na kuwaombea pumziko la amani wote waliotangulia mbele za haki.

“Serikali itaendelea kutoa taarifa zaidi kuhusu zoezi la uokozi hadi hapo zoezi hili litakapokamilika,” alisema.

Rais Samia alipongeza na kuvishukuru vyombo vyote vya usalama ambavyo vinaendelea na zoezi hilo.

Pia aliyashukuru mashirika binafsi na wananchi wote waliojitolea na waliojitoa na waliotoa ushirikiano katika zoezi hilo

Kadhalika aliwashukuru madaktari wanaoendelea kuwahudumia majeruhi

Pia Rais Samia amempongeza Waziri Mkuu, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaa na timu zao kwa kusimamia kazi kubwa iliyofanyika ya uokozi.

Rais Samia amesema Serikali inahakikisha ushirikiano wake kuanzia mwanzo wa zoezi hilo hadi mwisho na kwamba taarifa za uchunguzi zitakaopatikana zitawekwa wazi kwa wananchi wote na hatua zitakazochukuliwa .