Na Mwandishi Wetu,TimesmajiraOnline,Dar
KITENDO cha Rais Samia Suluhu Hassan, kuongoza nchi vizuri kimeongeza hamasa kwa wanawake kujitikeza kwa wingi kuwania uongozi katika uchaguzi mdogo wa madiwani.
Hiyo imedhihirishwa na idadi wa wanawake wanaojitokeza kuwania udiwani kwenye uchaguzi huo ambao hadi jana wanawake tisa ni kati ya wagombea 13 walijitokeza kuchukua fomu za uteuzi katika Kata ya Kimbiji katika Halmashauri ya Wilaya ya Kigamboni Mkoani Dares Salaam.
Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi Kata ya Kimbiji, Ricky Pascal, alisema mwitikio huo wa wanawake katika masuala ya uchaguzi ni kutokana na hamasa waliyoipata kutoka kwa Rais Samia, ambaye anaiongoza nchi vizuri.
“Niwapongeze wagombea wote waliochukua fomu kuwania udiwani katika Kata ya Kimbiji, hasa wanawake walioamua kuwania nafasi kwa wingi kutokana na hamasa waliyoipata kutoka kwa kiongozi wan chi,”alisema Pascal.
Pascal alisema, zimesalia siku mbili kwa pazia la kuchukua fomu za uteuzi kufungwa katika uchaguzi mdogo wa udiweani Kata ya Kimbiji lakini mwitikio wa wanawake kushiriki katika uchaguzi huo ni ishara ya ukuaji wa demokrasia nchini.
Wagombea hao majina yao na vyama wanavyotoka katika mabano ni Bi. Shani Ally Kitumbua (AAFP), Michael Makire Mzalendo (UDP), Bw. Shabani Masiku Chumu (Demokrasia Makini), .Kondo Abdu Hatibu ‘Lukali’ (CUF), Halima Abdalla Mbago (NLD), Innocent Fratern Shirima (CCK) na Rachel Paul Mwikola (UPDP).
Wengine ni Maimuna Mwinyipingu Yusuf (CCM), Bi. Neema Kassim Yegeyege (UMD), Dianarose Joseph Mhoja (ADA-Tadea), Joyce Ephraim Mweigule (DP) na Janeth Pius Mhando (TLP).
Wagombea hao walikabidhiwa fomu zao za uteuzi na Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi Kata ya Kimbiji, Ricky Pascal na Bi. Twidike Ntwima.
Tume ilitangaza uchaguzi Mdogo katika Kata 23 za Tanzania bara kufanyika Machi 20,2024 na fomu za uteuzi zilianza kutolewa Februari 27 hadi Machi 4 mwaka huu.
Mbali na Kata Kimbiji (Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni), Kata zingine zinazofanya uchaguzi ni Kasingirima (Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma/Ujiji), Ndevelwa (Halmashauri ya Manispaa ya Tabora), Msangani (Halmashauri ya Mji Kibaha), Fukayosi (Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo), Mlanzi (Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti), Utiri (Halmashauri ya Mji Mbinga) na Mbingamhalule (Halmashauri ya Wilaya ya Songea).
Nyingine ni Isebya (Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe), Kibata (Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa), Mshikamano (Halmashauri ya Wilaya ya Musoma), Busegwe (Halmashauri ya Wilaya ya Butiama), Nkokwa (Halmashauri ya Wilaya ya Kyela), Kamwene (Halmashauri ya Wilaya ya Mlimba), Chipuputa (Halmashauri ya Wilaya ya Nanyumbu), Buzilasoga (Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema), Mhande (Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba), Kabwe (Halmashauri ya Nkasi), Bukundi (Halmashauri ya Wilaya ya Meatu) Mkuzi (Halmashauri ya Wilaya ya Muheza) na Boma, Mtimbwani na Mayomboni (Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga).
More Stories
Watakaokwamisha mapato Kaliua kukiona cha moto
Dkt.Gwajima aagiza kuundwa kamati za ulinzi wa watoto
Kilo 673.2,dawa za kulevya zakamatwa Bahari ya Hindi