February 25, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Samia ajitosa madai yawalimu wasio na ajira

  • Ni wale wanaodai usahili nafasi za ajira kada ya ualimu zina upendeleo, rushwa, 4R kuwakutanisha na Wizara tatu, Simbachawene afunguka

Na Mwandishi Wetu,Timesmajiraonline,Dar

WAZIRI Nchi, Ofisi ya Rais Utumishi, George Simbachawene, amewaagiza makatibu Mkuu wa TAMISEMI, Wizara ya Elimu na Utumishi kuwaita wanaojiita Umoja wa Walimu Wasio na Ajira Tanzania (NETO) ili kukaa nao meza moja, kuwasilikiza kuhusiana na madai kuwa kuna vitendo vya upendeleo na rushwa katika usaili wa nafasi za ajira za kada ya ualimu.

Kwa mujibu wa Waziri Simbachawene uamuzi huo ni maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan ambaye anasema lazima nchi ije na maridhiano na maelewano, kwani migogoro haisaidii.

Simbachawene amesema mawazo yao ni mazuri wayalete watayachakata na kuyafanyia kazi.

“Tutawashirikisha na kuwa sehemu ya utatuzi wa changamoto iliyopo.

Nchi yetu kila Mtanzania ana haki ya kutoa mawazo vijana hawa wametoa mawazo mazuri,”alisema.

Waziri Simbachawene alisema ameagiza waitwe ili wakae meza moja kwani falsafa ya Rais Samia Suluhu Hassan, nchi yetu inaongozwa kwa misingi ya 4R.

Alisema alipopata waraka wa chama kinachojiita Umoja wa Walimu Wasiokuwa na Ajira kilichomsumbua sio uhalali wa chama, kilichomsumbua ni maoni na mawazo yao yaliyomo kwenye waraka huo.

“Kwanza maoni yao wameyaandika vizuri sana kwenye ule waraka mimi nilisoma , nimeona waraka una maudhui yanaweza kuwa yanaleta hoja ya kufikiri zaidi , lakini kuna malalamiko ambayo inabidi tuyajibu, lakini mimi siwezi kuyajibu wakati mimi sifahamu,” alisema Simbachawene.

Alikaribisha vijana hao kwenye ofisi yake Wizara ya Utumishi, kwani yeye ndiye anayesimamia sera ya ajira na ajira nchini .

“Nimewasiliana na wenzangu Wizara ya Elimu, Waziri Mchengerwa (Waziri wa TAMISEMI) wao ndio waajiri, mimi kazi yangu ni kusimamia ajira za nchi hii, kwa hiyo tumekubaliana tuwaite tukae nao mezani tuzungumze.

Na sisi tunasema kwa niaba ya Serikali, kama watakuwa tayari popote pale kama ni Dodoma, au Dar es Salaam, lakini ni wazo zuri tukutane makao makuu ya nchi tupate nafasi nzuri ili waeleze wazi wazi, na kwenye yule waraka tujue nani ni nani .

Na wale waliotajwa kwenye ule waraka kwa upendo mkubwa nawamuita.

Alisema wao kama wateule wa Rais Samia vijana hao wasomi kabisa kama wana manung’uniko yao lazima tuyasikilize, kwa hiyo wasiogope, waje wasikilizane, waelewane, kwani pengine mawazo yao yakazaa ushauri mzuri ambao utazaa jambo zuri kwa wao, lakini kwa taifa.

“Wasikilize ushauri wao, maoni yao ili pale penye changamoto tuweze kuzitatua ili elimu yetu iweze kusonga mbele, kwani maoni yao na mawazo yao sio ya kupuuza,” alisema Simbachawene.

Umoja huo usio rasmi unadai ni wasomi wa kada hiyo waliokosa ajira tangu mwaka 2015 hadi 2023 ni kutokana na usaili unaoendelea wa nafasi 14,648 za walimu zilizotangazwa na Sekretarieti ya Ajira.

Akijibu tuhuma hizo Februari 19, 2025 kupitia taarifa kwa umma, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini wa Sekretarieti ya ajira, Lynn Chawala aliwakumbusha wale wote wanaotoa taarifa za kupotosha kuhusu mchakato wa ajira za walimu unaoendelea nchini kote kuacha upotoshaji huo.

“Ili kutekeleza dhana ya uwazi, usaili wa kada za ualimu unasimamiwa kwa ushirikiano wa viongozi kutoka Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma, Ofisi ya Rais (Utumishi), Ofisi ya Rais (Tamisemi), Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Tume ya Utumishi wa Walimu, Taasisi nyingine za Umma pamoja na Ofisi za Wakuu wa Mikoa kote nchini.”