January 21, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Samia aja na mkakati wa kukabiliana na ajali

Ni katika barabara ya Morogoro-Dodoma, aagiza kujengwa kwa maegesho ya malori, kufungwa taa kwenye miji ya Dakawa, Kibaigwa

Na Mwandishi Wetu,Timesmajiraonline

RAIS Samia Suluhu Hassan, ameagiza kujengwa kwa maegesho ya malori na taa za barabarani katika miji ya Dakawa na Kibaigwa katika barabara ya Morogoro – Dodoma ili kupunguza ajali na kukuza biashara katika miji hiyo.

Akikagua barabara hiyo, Waziri wa Ujenzi Abdallah Ulega, amewataka Mameneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS ) wa mkoa wa Morogoro na Dodoma kufanyia kazi agizo hilo mara moja.

“Rais amenielekeza tuhakikishe kwenye barabara kuu nchini kote tunafunga taa za barabarani zinazotumia umeme wa jua (solar) katika miji inayokuwa ili kuongeza usalama, kupunguza ajali na kuimarisha biashara za wananchi wa maeneo hayo,”, alisisitiza Waziri Ulega.

Waziri Ulega amesema Mameneja wote wahakikishe miji inang’aa kwa taa za ‘Solar’ ambazo ni gharama nafuu na kusisitiza kuwa Barabara nzuri ni fursa hivyo zikiboreshwa zitachochea maendeleo na kukuza biashara haraka.

“Katika kupunguza msongamano wa magari Morogoro mjini tutajenga barabara wezeshi kati ya Nane nane hadi Msamvu na Kihonda hadi Mkundi tunaomba wananchi mtupe ushirikiano ili eneo hilo liboreshwe,” alisisitiza Ulega.

Alisema barabara ya Stesheni hadi Kihonda inajengwa kwa njia nne ili kupunguza msongamano na kuvutia uwekezaji.

Alimtaka Meneja wa TANROADS Mkoa wa Morogoro, Alinanuswe Kyamba kujenga eneo la maegesho lenye urefu wa mita 200 na kufunga taa 50 za umeme wa jua eneo la Dakawa na Eng. Zuhura Aman wa mkoa wa Dodoma kufanya hivyo eneo la Kibaigwa ili kupendezesha miji hiyo na kuchochea biashara ili zifanyike usiku na mchana.

Aidha, Ulega alimtaka Meneja wa TANROADS Mkoa wa Dodoma kuhakikisha ujenzi wa miradi ya dharura unaambatana na uwekaji wa taa za barabarani ili kupendezesha jiji na kujenga barabara za mchepuko ili kuondoa msongamano wa magari katikati ya jiji la Dodoma.

Kuhusu ujenzi wa miradi ya dharura Waziri Ulega, alisema Serikali imetoa sh. bilioni 54 kwaajili ya kukarabati madaraja yalioathirika na mvua za el-nino mkoani Morogoro na zaidi ya bilioni 35 mkoani Dodoma hivyo kuwataka wakandarasi waliopewa miradi hiyo kuongeza kasi ya ujenzi na kufanya kazi usiku na mchana.