*Amtaka Prof. Janabi kujiandaa kugombea nafasi ya aliyekuwa Mkurugenzi wa WHO Kanda ya Afrika, Dk. Faustine Ndugulile
Na Jackline Mkota, Timesmajiraonline
RAIS Samia Suluhu Hassan amewataka Mawaziri kuwatumia ipasavyo Makatibu Wakuu na wataalamu wataowakuta katika Wizara
zao ili kuongeza ufanisi ndani ya Serikali katika kuwahudumia wananchi.
Rais Dkt. Samia aliyasema hayo jana Ikulu ndogo ya Tunguu wakati akiwaapisha viongozi mbalimbali wakiwemo Mawaziri, Naibu Mawaziri, Naibu Makatibu Wakuu na Mabalozi wateule.
Aidha, Rais Dkt. Samia alisema katika kutekeleza mkakati wa taifa wa uchumi wa kidigitali ambao unachochewa na kasi ya ukuaji wa sekta ya mawasiliano na teknolojia ndani ya nchi na dunia nzima, ni vyema sasa kutenganisha majukumu hayo na yale ya sekta ya habari ili msisitizo wa kimkakati utekelezwe kwa ufanisi zaidi.
Kwa upande mwingine, Rais Dkt. Samia amemuagiza Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Ashat Kijaji kuchoche ufanisi na uimarishaji wa uchumi wa buluu pamoja na kuambatana na wataalamu katika kuwasikiliza na kutatua kero za wakulima na wafugaji.
Rais Dkt. Samia pia amemtaka Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano wa Mazingira) Hamad Yussuf Masauni kushughulikia ipasavyo masuala ya Muungano na kumtaka kushiriki kikamilifu katika majukwaa mbalimbali ili kupaza sauti kimkakati kuhusu masuala ya mazingira.
Vile vile, Rais Dkt. Samia amewataka Mabalozi wapya kwenda kuiwakilisha vyema Tanzania hasa katika maeneo ambayo kama taifa wana maslahi nayo hasa zile nchi tulizoshirikiana nazo katika ukombozi wa Bara letu la Afrika.
Wakati huo huo, Rais Samia Suluhu Hassan, amemtaka Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Profesa Mohamed Janabi, kujiandaa kugombea nafasi ya aliyekuwa Mkurugenzi wa Shirika la Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika, Dk Faustine Ndugulile. Dk Ndugulile.
Ndugulile, alifariki dunia Novemba 27, 2024 ikiwa ni miezi kadhaa baada ya kushinda nafasi hiyo.
Akizungumza mara baada ya kuwaapisha viongozi mbalimbali Ikulu, Ikulu Ndogo ya Tunguu, Zanzibar, Rais Samia alisema wamepitia wasifu na kubaini kwamba, Profesa Janabi ana sifa ya kurithi mikoba hiyo
“Naomba nifichue siri hapa, tumepitia zaidi na tukaona Profesa Janabi anafaa kuchukua nafasi ya Dkt. Ndugulile.
Hivyo, tunakundaa kwenda kugombea nafasi hiyo muda utakapofikia. Ujiandae,” amlisema Rais Samia.
Dkt. Ndugulile alitarajiwa kuanza kazi rasmi WHO Machi 2025, baada ya kupewa miezi sita ya kujipanga. Dk Ndugulile alikuwa Mtanzania wa kwanza, pia wa kwanza kutoka Afrika Mashariki kushika nafasi hiyo.
More Stories
Wizara ya madini yakusanya bil.521 nusu ya kwanza mwaka wa fedha 2024/25
Meya awafunda wenyeviti Serikali za Mitaa
Mgeja aipongeza CCM kwa uteuzi Wagombea Urais