December 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Samia aapisha aliowateua, afichua siri ya mabadiliko

*Awataka waende wafuate viapo na kufuata maadili ya kikazi yanayotakiwa,
Profesa . Kabudi, Lukuvi nao rasmi tena ndani ya Baraza ya Mawaziri

Na Mwandishi Wetu,Timesmajiraonline,Dar

RAIS Samia Suluhu Hassan, amesema mabadiliko aliyoyafanya kwa viongozi aliowateua kushika nyadhifa mbalimbali ni ya kawaida kwa lengo la kuongeza ufanisi katika maeneo yao.

Rais Samia alitoa kauli hiyo Ikulu jijini Dar es Salaam jana wakati akizungumza mara baada ya kuwaapisha viongozi hao ambao walitangazwa juzi usiku. Alisema kwa leo (jana) hatakuwa na muda mwingine wa kuzungumza, kwa sababu ana safari, lakini atawaita kwa sekta zao siku moja moja waende wakazungumze.

Alisema viongozi hao wameapa viapa kwa dini zao, waende wafuate viapo na kufuata maadili ya kikazi yanayotakiwa. “Katika kufanyakazi zenu kuna utaalam wenu ambao mmesomea binafsi na kujiongeza kwa kutumia akili zenu.

Kwa hiyo mnapoona zinaweza kutumika vizuri, basi zitumieni mfanyekazi tuwatumikie wananchi,” alisisitiza Rais Samia.

Akizungumza wakati wa kumkaribisha Rais Samia, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango, Alisema viapo walivyokula ni vizito sana, akawasihi wakaviishi katika nafasi zao walizoteuliwa.

“Lakini matumaini ya Rais (Samia) aliyewapa dhamana hiyo ni kwamba Watanzania watapata huduma bora katika nafasi zenu mbalimbali, vinginevyo watabaini kuwa tunapwaya katika nafasi zetu.

Wafanyenikazi kwa bidii, mkashirikiane na viongozi wengine mtakaowakuta ili kama taifa tuweze kwenda haraka zaidi na Mwenye Mungu awatangulie kwenye nafasi zenu,” alisema Dkt. Mpango.

Kwa upande wake Jaji Mkuu Prof. Ibrahim Juma, alimshukuru Rais Samia kwa Mahakama kuongezewa nguvu Jaji wa Mahakama ya Rufaa na kwamba viongozi walioapishwa huduma zao zinagusa mahakama.

Aliwataka wakafanyie kazi imani kubwa ambayo Rais amewapa kwa ajili ya wananchi wa Watanzania.

Alisema imani hiyo ndiyo itawawezesha kutekeleza sheria na kanuni. Alisema changamoto kubwa katika nchi zinazoendelea sio mapungugfu ya sheria au bajeti, bali ni wao wanaolengwa na sheria ambao wanakuja na tamaduni binafsi.

Alisema watakapoenda katika sehemu zao za kazi pamoja na kuangalia sheria, ni lazima waangalie nafsi zao wenyewe. “Tuna tabia zile ambazo zinafanya sheria ziweze zisifanye kazi,”alisema Profesa Jumaa .

Jambo lingine alilohimiza ambalo alisema linaonekana katika nchi zetu zinazoendelea ni kusisitiza sana haki, lakini tunasahau wajibu. “Kuna watu wameishajitokeza kwamba tunatawaliwa sana na haki , lakini tunasahau kwamba demokrasia inajengwa zaidi na kuwajibika, mwananchi inayelengwa na sheria, vilele ana haki na wajibu kwa nchi yake, kwa taasisi yake, tunatimiza hilo sharti kwa namna gani?” Alihoji na kuongeza;

“Kwa hiyo ninaomba tutakapokwenda kule tuangalie haki, lakini vile vile tusisahau wajibu.”

Uteuzi

Juzi usiku taarifa iliyosainiwa na Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Sharifa Nyanga, aliambatana mkeka wa viongozi mbalimbali walioteuliwa na Rais Samia pamoja na kuhamishwa katika mfasi mbalimbali mbalimbali.

Miongoni mwa viongozi hao ambao pia waliapishwa jana William Lukuvi na Profesa Palamagamba Kabudi.

Viongozi hao wamrejeshwa kwenye Baraza la Mawaziri, ambapo Profesa Kabudi ameapishwa kuwa Waziri wa Katiba na Sheria, huku Lukuvi akiteuliwa kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu).

Jenista Mhagama ameapishwa kuwa Waziri wa Afya kuchukua nafasi ya Ummy Mwalimu. Mhagama kabla ya uteuzi huo wa juzi alikuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu).

Pia Rais Samia amemwapisha Balozi Pindi Chana kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, awali alikuwa Waziri wa Katiba na Sheria. Balozi Chana anachukua nafasi ya Angellah Kairuki, aliyeteuliwa kuwa Mshauri wa Rais.

Aidha, Rais Samia pia alimwapisha Hamza Johari kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuchukua nafasi ya Jaji Eliezer Feleshi, ambaye ameteuliwa na jana kuapishwa kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani.

Kabla ya uteuzi huo Johari alikuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA). Wengine walioteuliwa ni Samwel Maneno, ambaye aliteuliwa kuwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, awali alikuwa Msaidizi wa Rais, Sheria.

Anachukua nafasi ya Balozi Kennedy Gastorn ambaye ameteuliwa kuwa Mshauri wa Rais, Sheria na Mikataba. Mwingine ni Dkt. Ally Possi ambaye anakuwa Wakili Mkuu wa Serikali, kabla ya uteuzi alikuwa Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Uchukuzi.

Mbali ya hao, Rais Samia pia ameteua Salum Hamduni kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga, ambaye kabla ya uteuzi alikuwa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru). Hamduni anachukua nafasi ya Profesa Siza Tumbo ambaye amerejea Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA).

Rais pia amemteua Ismail Rumatila kuwa Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Afya, awali alikuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA). Mwingine aliyeteuliwa na Rais ni Atupele Mwambene anayekuwa Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa anayeshughulikia masuala ya elimu.

Kabla ya uteuzi alikuwa Mkurugenzi wa Sera na Mipango, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia. Rais Samia amemteua Abdul Mhinte kuwa Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia mifugo.

Kabla ya uteuzi alikuwa Ofisa Mwandamizi, Ofisi ya Rais – Ikulu. Pia Methusela Ntonda ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, kabla ya uteuzi huo alikuwa Ofisa Mwandamizi, Ofisi ya Rais – Ikulu. Viongozi hao waliapishwa jana.

***Uhamisho wa naibu makatibu wakuu

Dkt. Grace Magembe amehamishwa kutoka Wizara ya Afya kwenda kuwa Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa anayeshughulikia masuala ya afya. Dkt. Charles Msonde amehamishwa kutoka Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwenda kuwa Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Ujenzi, huku Dkt. Wilson Charles amehamishwa kutoka Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwenda kuwa Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, anayeshughulikia masuala ya elimu ya msingi na sekondari.

Profesa Daniel Mushi amehamishwa kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwenda kuwa Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia anayeshughulikia masuala ya sayansi na elimu ya juu.

Dkt. Franklin Rwezimula amehamishwa kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwenda kuwa Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Katiba na Sheria, huku Dkt. Khatibu Kazungu amehamishwa kutoka Wizara ya Katiba na Sheria kwenda kuwa Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati anayeshughulikia masuala ya umeme na nishati jadidifu.

Katika uteuzi huo, Dkt James Mataragio aliyewahi kuwa mkurugenzi kuu wa Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC), amekuwa Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati anayeshughulikia masuala ya petroli na gesi, huku Ludovick Nduhiye akihamishwa kutoka Wizara ya Ujenzi kwenda kuwa Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Uchukuzi. Dk Suleiman Serera amehamishwa kutoka Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kwenda kuwa Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Kilimo anayeshughulikia masuala ya ushirika na umwagiliaji.

Dkt. Hussein Mohamed Omar amekuwa Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Kilimo anayeshughulikia masuala ya maendeleo ya mazao na usalama wa chakula.

***Wakuu wa wilaya wahamishwa

Rais amemhamisha Kanali Maulid Surumbu kutoka Wilaya ya Tarime kwenda Mbarali, akichukua nafasi ya Brigedia Jenerali Denis Mwila ambaye amepangiwa majukumu mengine.

Meja Edward Gowele amehamishwa kutoka Rufiji kwenda Tarime, huku James Kaji akihamishwa kutoka Tanga kwenda kuwa Moshi.

Zephania Sumaye amehamishwa kutoka Wilaya ya Moshi kwenda Lushoto, huku Japhari Mghamba akihamishwa kutoka Wilaya ya Lushoto kwenda Wilaya ya Tanga. Rebecca Msemwa amehamishwa kutoka Wilaya ya Morogoro kwenda Bahi, huku Gift Msuya kutoka Bahi kwenda Pangani na Mussa Kilakala kutoka Wilaya Pangani kwenda Wilaya ya Morogoro.

Rais Samia pia amefanya uteuzi wa katibu tawala wa wilaya, ambao Proscovia Mwambi ameteuliwa kuwa Katibu Tawala wa Wilaya ya Bukoba.

***Uhamisho wa ma-DED

Rais amefanya uhamisho wa wakurugenzi watendaji wa halmashauri, ambapo John Kayombo amehamishwa kutoka Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwenda kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Jiji la Arusha.

Juma Seph amehamishwa kutoka Halmashauri ya Jiji la Arusha kwenda Jiji la Tanga, huku Fredrick Sagamiko akihamishwa kutoka Jiji la Tanga kwenda Dodoma.

Elihuruma Mabelya amehamishwa kutoka Halmashauri ya Manispaa ya Temeke kwenda kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Jomary Satura amehamishwa kutoka Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwenda Manispaa ya Temeke, huku Joanfaith Kataraia amehamishwa kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro kwenda Manispaa ya Singida.

Jeshi Lupembe amehamishwa kutoka Halmashauri ya Manispaa ya Singida kwenda Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro, huku Khamis Katimba akihamishwa kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Msalala Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi, Rose Manumba amehamishwa kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi kwenda Wilaya ya Msalala huku Stephen Katemba akihamishwa kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga kwenda Mbarali. Missana Kwangura amehamishwa kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali kwenda Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga; huku Happines Msanga akihamishwa kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba kwenda Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe; na Dk Amon Mkoga amehamishwa kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe kwenda kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba.

***Wakuu wa taasisi nao wamo

Rais Samia amepangua pia wakuu wa taasisi alimteua Crispin Chalamila kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).

Kabla ya uteuzi alikuwa Ofisa Mwandamizi, Ofisi ya Rais – Ikulu. Moremi Marwa ameteuliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), kabla ya uteuzi alikuwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa Shirika la Magereza (Shima) na Dkt Irene Isaka ameteuliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) akichukua nafasi ya Bernard Konga.