*Hadi Agosti, 2024, Tanzania ilivuja rekodi ya watalii wa kimataifa 2,026,378, mapato ya sekta hiyo nayo yapaa, nchi yatwaa tuzo za mbalimbali za kimataifa
Na Mwadishi Wetu,Timesmajiraonline
WAKATI Watanzania wanaelekea kuaga mwaka 2024 na kukaribisha mwaka mpya mpya 2025, wanamaliza mwaka huo kwa kujivunia mafanikio makubwa yaliyopatikana katika sekta ya utalii kutokana na juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan.
Kwa mujibu wa takwimu kutoka sekta ya utalii hadi kufikia Agosti, 2024, Tanzania imepokea watalii wa kimataifa 2,026,378 ikiwa ni kiwango cha juu kabisa kuwahi kufikiwa kwenye historia ya Tanzania.
Aidha, takwimu hizo zinaonesha kuwa mapato yatokanayo na sekta hiyo, nayo yalifikia dola za Marekani bilioni 3.5.
Mafanikio hayo katika sekta ya utalii yamepatikana katika kipindi kifupi cha Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Samia.
“Juhudi hizo za Dkt. Samia, zimefanya idadi ya watalii wa kimataifa wanaotembelea nchi yetu kukua kwa kasi sambamba na ongezeko la mapato yatokanayo na sekta ya utalii,” alinukuliwa akisema hivi karibu Rais wa Zanzibar Dkt. Hussein Ali Mwinyi na kuongeza;
“Juhudi hizo za Rais Samia zimefanya Sekta ya Utalii kuendelea kuwa nguzo muhimu katika kukuza uchumi wa Tanzania, huku ikichangia asilimia 17.2 ya Pato Ghafi la Taifa.
Asilimia 25 ya mauzo ya nje na kuzalisha ajira zaidi ya milioni 1.5 ikiwa ni ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja kupitia mnyororo wake wa thamani.”
Lakini pia, Watanzania wameshuhudia juhudi zinazofanywa na Serikali chini ya uongozi wa Dkt. Samia, kwa kuimarisha miundombinu ya utalii ikiwemo kuendelea kuliimarisha Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL).
Juhudi nyingine ni pamoja na kuhamasisha mashirika mengine ya ndege ya kimataifa kuanzisha safari za moja kwa moja kati ya Tanzania na nchi zenye masoko ya utalii, kujenga barabara na reli za kisasa zinazounganisha vivutio vya utalii, kujenga na kukarabati viwanja vya ndege, na kuimarisha huduma nyingine muhimu za utalii.
Serikali chini ya uongozi wa Rais Samia imekuwa ikifanya hivyo kwa kutambua kwamba utalii ni sekta yenye ushindani mkubwa hasa kwa sekta ya utangazaji.
Hiyo ni kwa sababu bila kutangazwa utalii kimataifa, Tanzania haiwezi kufikia malengo iliyojiwekea.
Mafanikio hayo yamewezesha Tanzania kutambuliwa kimataifa na kupata tuzo mbalimbali.
Mfano, taarifa iliyotolewa Septemba, 2024 na Shirika la Utalii Duniani (UN Tourism – World Tourism Barometer) inaonesha kuwa, Tanzania imeshika nafasi ya sita Duniani na ya kwanza Barani Afrika kwa kuwa na ongezeko kubwa la watalii.
Miongoni mwa tuzo hizo ni zile zilizotolewa mwaka 2023 na World Travel Awards (WTA) ambayo imeitambua Bodi ya Utalii Tanzania kama Africa’s Leading Tourist Board, Kisiwa cha Thanda Shunghumbili, Mafia kama World Leading Exclusive Private Island, Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro kama Africa’s Leading Tourist Attraction.
Kutokana na mafanikio hayo Waziri wa Maliasi na Utalii, Balozi Dkt. Pindi Chana, anaweka wazi kwamba sekta ya Utalii imekuwa na mchango mkubwa kwenye Pato la Taifa, ambapo inachangia asilimia 17.
Aidha, mafanikio makubwa yanayopatikana nchini kupitia sekta ya utalii yanaitangaza Tanzania kimataifa na kuitambulisha duniani kuwa nchi ya kwanza Afrika inayofanya vizuri kwa utalii na ya sita dunia.
MWISHO=============
More Stories
Wananchi wa Ikuvilo watakiwa kujitokeza kuhakiki taarifa zao
Watanzania wahimizwa kutenda mema
Nani kuwa mrithi wa Kinana CCM?