Na Mwandishi Wetu, Timesmajiraonline
RAIS Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameagiza huduma za dharura zipelekwe kwenye maeneo yaliyopata athari kutokana na kimbunga Hidaya.
Hayo yamesemwa jana na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kwenye kikao cha dharura cha Kamati ya Maafa Kitaifa alichokiitisha kupokea taarifa ya hatua zilizochukuliwa kwenye maeneo yaliyopata athari.
“Rais ameelekeza hatua za haraka zichukuliwe katika maeneo yote yaliyoathiriwa na mvua zilizotokana na athari za kimbunga Hidaya ikiwa ni pamoja na kupeleka misaada,” amesema. Maeneo yatakayopelekewa misaada hiyo ni Mafia mkoani Pwani, Kilwa (Lindi) na Ifakara (Morogoro).
Waziri Mkuu ameliagiza Jeshi la Zimamoto na Uokoaji lihakikishe linakamilisha zoezi la uokoaji katika maeneo ya Kilwa ambapo zaidi ya kaya 40 zimezingirwa na maji. “Jeshi la Zimamoto mmefanya kazi kubwa, hakikisheni maeneo yenye makazi yaliyozingirwa na maji, wakazi wake wanaondolewa na kupelekwa maeneo salama pamoja na kupewa huduma zote muhimu.”
Wakati huohuo, Waziri Mkuu ameziagiza Wizara za Ujenzi, Uchukuzi, Afya, Maji, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mambo ya Ndani ya Nchi, Ulinzi na Fedha zichukue hatua za dharura ili kuhakikisha hakuna madhara zaidi yanatokea katika maeneo yaliyopatwa na athari.
“Wizara ya Ujenzi endeleeni kuchukua hatua zote za dharura zinazohitajika kuhakikisha maeneo ya barabara yaliyokatika yanarekebishwa na huduma za usafiri zinarudi haraka.”
Waziri Mkuu amepongeza jitihada zinazofanywa na Idara ya Menejimenti ya Maafa kwa kuendelea kufanya uratibu katika maeneo yote yaliyoathirika na kuwataka waendelee na uratibu katika maeneo yaliyopata madhara kuanzia juzi.
“Ongezeni nguvu katika maeneo ya Ifakara, Kilwa na Mafia na kuhakikisha wananchi wote walioathiriwa wanakuwa katika maeneo salama na wanapata huduma zote za msingi za kijamii.”
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ameiagiza Kamati ya Maafa ya Kitaifa izisimamie Kamati za mikoa na Wilaya ili misaada inayotolewa kwa waathirika iwafikie walengwa. “Kamati ya Kitaifa izielekeze Kamati za Mikoa na Wilaya zisimamie misaada yote ya waathirika ili ifike kwa wahusika, baadaye hali ikisharejea, tutataka tupate taarifa ya kina na jinsi ilivyotumika,” amesisitiza.
More Stories
The Desk & Chair yashusha neema Gereza la Butimba
TVLA,yapongezwa kwa kuzalisha chanjo
TAKUKURU,yasaidia kurejesha hekali 8