March 29, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Samamba:Uongezaji thamani madini ni mkakati wa serikali kukuza mchango wa sekta

Na Mwandishi wetu, Timesmajira

Katibu Mkuu Wizara ya Madini Mhandisi Yahya Samamba amesema kuwa, Serikali kupitia Wizara ya Madini imedhamiria kukuza sekta ya madini kwa kuhakikisha madini yanachakatwa na kuongezwa thamani hapa nchini badala ya kusafirishwa yakiwa ghafi. Hatua hii inalenga kuongeza mchango wa sekta ya madini katika Pato la Taifa, kukuza uchumi wa nchi na kulinda ajira za Watanzania.

Amesema hayo leo Machi 25, 2025, jijini Dodoma wakati wa hafla ya kusaini Hati ya Makubaliano (Memorandum of Understanding – MoU) kati ya Wizara ya Madini kupitia Kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC) na Kampuni ya Sunset Gem kutoka Thailand.

Mhandisi Samamba amesema kuwa, makubaliano hayo ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuhakikisha Tanzania inakuwa na uwezo wa kuongeza thamani madini ya vito badala ya kuyauza yakiwa ghafi.

Aidha, amesisitizakuwa, kupitia makubaliano hayo, Tanzania itanufaika na uhaulishaji wa teknolojia mpya ya uongezaji thamani madini sambamba na kuboresha uwezo wa Kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC), ambacho ni taasisi muhimu katika sekta ya madini ya vito.

Aidha, ameongeza kuwa Serikali inajenga jengo la ghorofa nane jijini Arusha kwa ajili ya kuimarisha kituo hicho na kuonesha dhamira ya dhati ya kuboresha mazingira ya biashara ya madini ya vito nchini.

“Tunataka kuhakikisha kuwa madini yetu hayauzwi ghafi, bali yanaongezwa thamani hapa nchini ili kuyawezesha kuchangia kikamilifu katika uchumi wetu. Hatua hii pia inalenga kuhakikisha ajira za Watanzania zinabaki ndani ya nchi kwa kuongeza wataalamu wa ndani katika tasnia ya madini ya vito,” amesema Mhandisi Samamba.

Kwa upande wake, Mtendaji wa Kampuni ya Sunset Gem kutoka Thailand, Pukkapon Piantumdee, amesema kuwa kampuni yake imebobea katika ukataji, ung’arishaji na utambuzi wa vito, na wanatarajia kutumia fursa hiyo kushirikiana na Tanzania katika kubadilishana uzoefu na utaalamu.

Naye, Kaimu Mratibu wa Kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC), Mhandisi Ally Maganga, amesema kuwa hatua hiyo itawapa fursa vijana wa Kitanzania na wanafunzi wa kituo hicho kwenda kujifunza zaidi nchini Thailand, pamoja na kupata ujuzi wa kisasa katika teknolojia ya uongezaji thamani madini.

Hatua hiyo inadhihirisha azma ya Serikali kuhakikisha kuwa Sekta ya Madini inafikia lengo la kuchangia asilimia 10 ya Pato la Taifa, hivyo ushirikiano na mataifa yaliyoendelea katika sekta hii, kama Thailand, ni hatua muhimu katika kufanikisha azma hiyo.