March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Sakaya :Wananchi chagueni viongozi makini

*Asisitiza wamchague kwa ajili ya hatma ya maendeleo ya Kaliua

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online-Tabora

WAKAZI wa Jimbo la Kaliua mkoani Tabora na majimbo mengine nchini wametakiwa kuchagua wabunge na madiwani wachapa kazi ambao watawasemea na kusimamia haki zao ipasavyo.

Hayo yamebainishwa na mgombea Ubunge Jimbo la Kaliua,Magdalena Sakaya kupitia Chama cha Wananchi CUF,wakati wa mkutano wake wa kampeni uliofanyika vijiji vya Igagala Namba 7 na Namba 5.

Sakaya amesema kuwa uchaguzi mkuu ni fursa muhimu kwa wananchi kupata viongozi wao kuanzia Rais, wabunge na madiwani, hivyo amewahimiza kuchagua kiongozi mwenye maono, uwezo na mchapa kazi, vinginevyo watajuta.

Kiongozi makini ni yule anayetanguliza mbele maslahi ya wananchi wake, siyo maslahi binafsi, hivyo akawataka kutofanya makosa Oktoba 29,2025 bali wamchague kuwa Mbunge wao ili akatetee maslahi yao bungeni.

Sakaya amesisitiza kuwa kama watampa ridhaa ya kuwa Mbunge atahakikisha huduma za afya zinapatikana katika maeneo yote na kwa upande wa vijiji ambavyo havina zahanati atasimamia ili zijengwe.

“Hatma ya maendeleo ya wakazi wa Jimbo hili ipo mikononi mwa kiongozi atakayechaguliwa, msifanye makosa bali chagueni mtu makini atakayetetea haki zenu na maendeleo yenu ambaye ni mimi,”amesema Sakaya.

Sanjari na hayo ameahidi kuwa atahakikisha kata zote ambazo hazina vituo vya afya vinajengwa ili kuwaondolea kero akinamama wajawazito, watoto na wazee ya kutembelea umbali mrefu kufuata huduma hizo katika kata nyingine.

Pia ameahidi kusimamia na kuhakikisha huduma ya nishati ya umeme inawafikia wananchi katika vijiji vyote vya Jimbo hilo, na nguzo za umeme zitafikishwa katika maeneo yote.

Hata hivyo amesema,ata hakikisha mikopo ya asilimia 10,inanufaisha makundi yote na wale wanaostahili kuingizwa katika Mfuko wa Kunusuru Kaya Maskini (TASAF) wanaingizwa bila upendeleo.