January 23, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Safari za Rais Samia nje na umuhimu wake kwa Taifa

Na Mwnadishi Wetu, Timesmajira Online, Dar

WAKATI wa Kampeni za uchaguzi mkuu mwaka 2005 sera ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ikiungwa mkono na Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) ilikuwa ni kupunguza safari za rais nje ya nchi, pindi chama hicho kingeshika dola.

Hoja hiyo ya CHADEMA ilitokana na kile kilichoelezwa kwamba Rais wa Serikali ya Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete, alikuwa akifanya ziara nyingi nje ya nchi.

Msingi wa hoja ya viongozi hao wa CHADEMA ilikuwa ni kuitaka Serikali yake ipunguze safari hizo ili kubana matumizi.

Baada ya Kikwete kumaliza ngwe yake, aliingia Rais wa Serikali ya Awamu Tano, Hayati John Magufuli, ambaye msimamo wake ulikuwa ni kutosafiri nje ya nchi akisema kwamba atafanya hivyo baada ya kumaliza muda wake wa kutumikia wadhifa huo.

Katika kipindi chake cha uongozi, hayati Magufuli hakusafiri nje ya Bara la Afrika na badala yake alikuwa akiwakilishwa katika mikutano mbalimbali na Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan (Sasa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania) na Waziri Mkuu Majaliwa Kassim.

Magufuli alieleza kwamba msimamo huo umelenga kupunguza matumizi makubwa ya Serikali yanayotumika kugharamia safari hizo. Ilifikia hatua hata Watanzania wengi wakaamini hivyo,kwamba Rais asiposafiri nje ya nchini anakuwa anabana matumizi.

Miongoni mwa waliokuwa wa kwanza kupiga uamuzi huo wa Hayati Rais Magufuli, walikuwa ni CHADEMA wakisema haiwezekani kiongozi wa nchi kutosafiri nje ya nchi na kushiriki mikutano ya kimataifa.

Pia Watanzania wengine hawakukubaliana na msimamo wa Hayati Magufuli, walikosoa hadharani msimamo huo, kwa sababu walikuwa wakijua faida nyingi zinazotokana na safari za Rais nje ya nchi ikilinganishwa na kile kidogo unachookoa kwa kutosafiri nje ambacho ni sawa na tone la maji kwenye bahari.

Mfano tangu Rais Samia aingie madarakani mwaka 2021 na kuanza kusafiri nje ya nchi ameweza kufungua nchini na wawekezaji wengi kuzidi kumimikika nchini na kielelezo cha hilo ni takwimu za Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) ambazo zinaonesha wawekezaji wengi wanazidi kufurika nchini.

Lakini mahusiano ya Tanzania na nchi nyingine yamezidi kuimarika na Serikali kuaminika kwa wawekezaji jambo ambalo linastahili kuungwa mkono na Watanzania wote.

Pamoja na kuwepo watu wasiounga mkono safari za nje za Rais, wao wanasahau usemi wa kwenye biashara usemao; ‘Mtendaji mkuu wa kampuni ndiye meneja masoko namba moja wa kampuni yake.”

Hili tunalitazama katika biashara, lakini tunaweza pia kulitazama kisiasa na hasa katika uongozi wa juu wa nchi.

Kubana matumizi ni jambo njema na kupunguza safari za nje zisizo za lazima ni jambo jema pia.

Lakini bado umuhimu wa Rais kama mkuu wa nchi ambaye mfano wake ni kama ule wa mtendaji mkuu (CEO) wa kampuni ana umuhimu mkubwa kutoka na kunadi kampuni yake ili kuongeza biashara.

Yapo mazingira ya kutuma wawakilishi lakini yapo mengine muhimu zaidi ambapo nafasi ya Rais inabaki pale bila kuhitaji kuwakilishwa.

Ni kutokana na umuhimu huu ndio maana Serikali kwa kutambua hilo, ilitumia mabilioni ya fedha kununua ndege maalumu ya masafa marefu ili kumwezesha Rais kusafiri kuwakilisha nchi na kuitangaza kimataifa.

Rais ndiye meneja masoko namba moja wa bidhaa zote na sifa zote za nchi yetu mbele ya mataifa mengine. Rais ni moja ya nembo za Taifa letu na kuficha uso wake kimataifa kunapoteza mwanga na nuru ya nchi yetu.

Rais ana baraza kubwa la mwaziri na watendaji chungu zima aliowachagua kumsaidia katika masuala mbalimbali ya kuendesha nchi, hivyo hatakiwi kuwa wasiwasi kuwaacha watu aliowachagua kuendesha nchi na yeye akatekeleze majukumu yake ya kimataifa.

Ni kweli kabisa kuna safari nyingine za nje hazina tija kwa nchi, lakini ukweli unabaki palepale kwamba Rais kama CEO namba moja wa Taifa, nafasi yake kusafiri kuwakilisha nchi yake ni muhimu na kuna mtu anayeweza kulalamika kuhusu hili kwani majukumu ya Rais ni ndani na nje ya nchi.

Tuchukue mfano mdogo wa CEO wa kampuni ya Barrick Gold Mine aliyewahi kusafiri kwa ndege ya kukodi kutoka Canada kuja nchini kuzungumzia sintofahamu iliyojitokeza kwenye suala la makinikia ya mchanga wa madini.

Si kana kwamba hana wasaidizi la hasha, bali alifanya hivyo kutokana na uzito wa suala lenyewe na kwamba yeye ndiye nembo kuu ya kampuni hiyo, hivyo kwa suala hilo, ‘hatumwi mtoto’.

Rais kama mkuu wa nchi anapaswa kuwakilisha nchi bila kujali ni gharama kiasi gani zitatumika.

Mfano, wakati wa Serikali ya Awamu ya Tano, Rais Magufuli hakuhudhuria Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ambao ni fursa adhimu ya wakuu wa mataifa duniani kukutana na kujadili masuala mbalimbali.

Ukiacha hilo hakuweza kuhudhuria mfululizo mara mbili Kongamano la kila mwaka la Uchumi Duniani huko Davos Uswiss ( World Economic Forum) ambalo ni fursa adhimu la wakuu wa nchi duniani, wanasiasa , wafanyabiashara wakubwa na makampuni makubwa duniani wanakutana kujadili na kuweka mikakati ya kukuza uchumi kwa mataifa yao na dunia kwa ujumla.

Kwa kweli sisi kama chombo cha habari tunampongeza Rais Samia ambaye amekuwa akihudhuria mkutano huo.

Ndiyo maana nasema Rais kutosafiri nje ni kukwepa jukumu lake lingine muhimu la kuwakilisha nchi kama CEO namba moja. Tunakumbuka Mwalimu Nyerere aliwahi kutamka kwamba; “ Tunahitaji kupata Rais ambaye hatutakuwa na shaka naye katika masuala mbalimbali ya kitaifa na kimataifa”.

Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, akiwa na Rais wa Marekani Joe Biden, Ikulu ya Marekani.

Ikimbukwe kwamba nchi hainyooshwi kwa kutosafiri, bali inaweza pia kunyooshwa vizuri zaidi kutokea nje ya nchi. Nje ya nchi kuna fursa nyingi zenye faida kubwa kwa maendeleo ya taifa letu, kwani Rais wa nchi kwa nafasi yake ndiye mwenye uwezo wa kuaminika.

Inawezekana suala la safari za nje kwa viongozi na watendaji limekuwa likitafsiriwa tofauti ndio maana leo inaonekana kwamba kukaa ndani ya nchi bila kusafiri ni kubana matumizi.

Tunashindwa kujiuliza kwamba je wanaosafiri wanatumia kiasi gani na kuingiza kiasi gani? Ni wazi kwamba kuna faida kubwa inayopatikana kwa wakuu wa nchi kusafiri.

Kuna mikataba mingi wanaingia kwa manufaa ya nchi na hili tumelishuhudia kwa Rais Samia. Tangu aingia madarakani amesaini mikataba mingi ya kimataifa ambayo ina manufaa kwa nchi huku idadi ya wawekezaji ikizidi kumiminika.

Lakini pia Rais Samia kupitia ziara za nje kimataifa anazidi kupata uzoefu wa masuala mbalimbali kwa faida ya taifa, mbali ya kutangaza nchi na kupanua wigo wa uhusiano.

Tumeshuhudia ziara za viongozi wa mataifa makubwa duniani ikiwemo makamu wa Rais wa Marekani. Haya yote ni mafunda ya Rais Samia kukuza ushirikiano. Tumeshuhudia mikutano mikubwa ya kimataifa ikifanyika hapa nchini, achilia mbali wakuu wa nchi mbalimbali ambao wamekuwa wakifanya ziara wakiambatana na ujumbe mkubwa.

Hii imekuwa fursa kubwa kwa uchumi wetu na haya ndiyo matokeo ya kuwa na kiongozi asiyejifungia ndani.

Inawezekana waasisi wa sera hii ya kupunguza safari za viongozi na watendaji nje ya nchi ambao ni CHADEMA na uliokuwa Muungano wa Ukawa kwenye uchaguzi wa mwaka 2015 hawakueleweka walikuwa wanalenga nini?

Tunapokuwa na Rais asiyesafiri tunafifisha taswira ya Taifa letu kwa mataifa mengine. Tunaweza kuona kuwa agenda ya kubana matumizi ni namba moja, lakini kumbe tunapoteza kikubwa na mengi zaidi ya hilo.

Tukumbuke kwamba kizuri ni lazima kigharamiwe, ndio maana tulinunua ndege ya Rais kwa ajili ya kuwezesha kushiriki kirahisi masuala mbalimbali yanayomuhusu faida kwa taifa.

Akitokea kwamba hatoki kutokana na kusimamia masuala ya hapa ndani ni kama kwamba haridhiki na utendaji wa mamia ya watu aliowateua baada ya kufanyiwa uhakiki wa kina na kuoneakana kwamba wana sifa za kumsaidia katika maeneo mbalimbali.

Uwezo wa wasaidizi wake ambao walionesha wakati wa maafa ya maporomoko ya tope, mawe na miti wilayani Hanang, mkoani Manyara ambayo yalitokea wakati Rais Samia akiwa nje ya nchi kikazi, ni kielelezo kwamba kiongozi huo ana wasaidizi imara na hakufanya kosa kuwateua kumsaidi.

Kwa jinsi wasaidizi wake walivyotekeleza maelekezo ya Rais akiwa nje ya nchi na jinsi wao walivyomudu majukumu yao ni kielelezo kwamba nchi inakuwa kwenye mikono salama, hata pale Rais anapokuwa kwenye majukumu ya kimataifa.

Katika mila za kiafrika baba hatakiwi kukaa nyumbani siku zote, ni lazima atoke kwenye mabaraza ya wenzake hata kama hapati chochote atajifunza mtazamo mpya juu ya masuala mbalimbali.

Waafrika wanaamini kwamba baba akibaki nyumbani kutwa matokeo yake ni kushinda na kugombana na watoto, jambo ambalo linaondoka furaha na amani ya familia.

Rais akisafiri nje kuna fursa nyingi na faida nyingi kwa maendelea ya nchi.

Kama nilivyosema awali, Rais wa nchi yoyote ni CEO namba moja wa kutangaza na kung’arisha taifa lake nje ya mipaka yake . Huyu ndiye mtu namba moja katika ‘kunadi na kulitafutia masoko taifa lake.’

Kuna kampuni kubwa za kigeni ambazo kila siku zinatafuta ukweli kujua undani wa mambo fulani kabla ya kufikia maamuzi yake kuwekeza au kuendesha shughuli zao katika nchi fulani.

Pamoja na kwamba baadhi ya nchi duniani zina vyombo mbalimbali vya kutangaza na kuvutia uwekezaji mitaji, ukweli unabaki pale pale kwamba meneja masoko namba moja ni rais au kiongozi wa nchi husika.

Mkuu wa nchi anapokaa na kuzungumza na wewekezaji vitega uchumi kwa lengo la kuwashawishi au kuwapa picha halisi ya ukweli wa mambo wanayohitaji katika nchi yake, anawajengea imani zaidi ya chombo chochote kile hata kama nchi itakuwa na tume au kamati maalumu kwa ajili ya kushughulikia hilo .

Ukweli unaoaminika zaidi kwa mwekezaji upo kwenye kinywa cha mkuu wa nchi husika ambaye akisimama na kuisemea nchi yake, hofu ya wawekezaji hao hutoweka haraka sana na mioyo yao kufunguka na kufikia uamuzi haraka.