Katikati ya Jiji la Mwanza, wilayani Nyamagana mtaa wa Hesawa ndipo yalipo makao makuu ya shirika la kutetea wafanyakazi wa nyumbani, linalojulikana kama WoteSawa. Mahali hapa pia ni makao ya muda ya watoto wa kike (mabinti), wanaookolewa kutoka utumikishwaji wa kazi za ndani na wale waliopitia ukatili kutoka kwa waajiri wao.
Miongoni mwa watoto wanaoishi hapa, ni binti mwenye umri wa miaka 13. Huyu alisafiri zaidi ya kilometa 700 kutoka mkoani Dodoma, akiwa ameahidiwa kusomeshwa akifika Mwanza. Hata hivyo baada ya kufika jijini Mwanza, alijikuta katika mazingira ya hatari zaidi, kuliko aliyoyaacha nyumbani kwao Dodoma. Ilivyo bahati kwake , alikutana na wasamaria wema na kumwezesha kubadili mtazamo wa safari ya maisha yake.
Hivi sasa binti huyu, Ushindi Matumaini (siyo jina lake halisi) anasoma darasa la tano katika shule ya msingi Nyamagana ‘B’ alikopelekwa na Shirika la WoteSawa. Safari ya binti huyu ilikuwaje? Fuatana na Mwandishi Wetu JUDITH FERDINAND katika makala haya.
Ushindi aliokolewa na Shirika la WoteSawa ambalo lilifanikiwa kumrejesha shule kuendelea na masomo baada ya kutoroka kwa ‘mwajiri’ wake jijini Mwanza, alikofikia akitokea kwao Dodoma.
Akiwa Dodoma, Ushindi alikuwa akisoma darasa la tatu. Siku moja, mama yake alimchukua kwenda naye Dodoma mjini kwa mwanamake ambaye alikuwa na malengo ya kumpeleka jijini Mwanza kwa ajili ya kufanya kazi za ndani na kusoma.
Ushindi anaeleza kuwa, baada ya kufika kwa huyo mama alimweleza mama yake kwamba kuna mtu anahitaji mfanyakazi wa ndani kwa makubaliano ya kumsomesha.
“Baada ya kusikia kuwa nitakuja Mwanza kuendelea na masomo nilikubali. Nikajiandaa na huyo mama alikuja kunichukua na kunileta hapa Mwanza.”
Hata hivyo anaeleza kuwa baada ya kufika Mwanza alifanyishwa kazi za ndani. Anasema shule zilipofunguliwa alikumbusha kuhusu ahadi ya kumsomesha, lakini ‘mwajiri’ wake alimuahidi kwamba angefanya hivyo, baada ya mume wake kurejea.
Ushindi anaeleza kuwa wakati akisubiri kutekelezwa kwa ahadi ya kupelekwa shule, aliendelea kufanya kazi ambazo ziliambatana na mateso, karaha na wakati mwingine alikuwa akinyimwa chakula.
“Mume wake aliporejea, niliwakumbusha tena kuhusu ahadi yao ya kunipeleka shule, lakini walikataa, huku wakiendelea kunitumikisha. Kuna siku mama alipika chakula akanituma dukani, akala chakula chote akamaliza kisha akanipa uji ambao haukuwa na sukari. Baada hapo aliniambia niendelee kufanya usafi,” anaeleza Ushindi.
Anataja changamoto nyingine alizopitia kuwa ni pamoja na kunyanyaswa na mwajiri hasa pale mtoto mdogo wa mwajiri huyo alipokuwa akilia, yeye alipigwa huku akigombezwa na kuulizwa kwanini amempiga mtoto huyo? kitu ambacho hakikuwa kweli.
Anasimulia kuwa siku moja asubuhi alitumwa kwa dada wa mwajiri wake akachukue fedha shilingi 13,500 ambazo bosi wake huyo alikuwa ametumiwa na mume wake, ambaye hakuwa akiishi hapo nyumbani.
“Baada ya kupatiwa fedha hizo, sikurudi tena nyumbani, nilitoroka. Nilitembea umbali mrefu, jua lilipokaribia kuzama nikafika mjini. Nilikuwa natembea nikifuata watu wanakoelekea, hadi nikafika eneo la Kirumba,” anaeleza Ushindi na kuongeza:
“Usiku nikaenda kwa mama lishe nikanunua chakula nikala na baada ya hapo nikatoka nje na kuingia mtaani kutafuta msaada wa mahali pa kulala. Kwa bahati mama mmoja alipita akaniuliza wewe mtoto unatokea wapi usiku huu?, nikamjibu kuwa sijui ninakotokea maana sikutaka anirudishe kwa mwajiri wangu. Aliniuliza,kwenu wapi? Nami nilimjibu kuwa kwetu ni Dodoma. Usiku huo yule mama alinipeleka nyumbani kwake,” anasema Ushindi.
Polisi, WoteSawa kisha shuleni
Ushindi anasema alilala kwa huyo mama na kulipopambazuka msamaria huyo alimpeleka kituo cha Polisi Kirumba na kupokewa na Askari Polisi ambao walimuhoji, kisha wakawapigia simu shirika la WoteSawa.
“Dada Renalda kutoka WoteSawa alinifuata kituoni hapo kesho yake akanichukua akanileta hapa kwenye shirika. Nilipofika hapa walinihoji nikawaambia nataka kusoma na wakanipeleka shule ya msingi Nyamagana nikaanza darasa la tatu kwa sababu wakati naacha shule kule Dodoma nilikuwa darasa la tatu mwaka 2021.
Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi Nyamagana’B’, Theresia Silias, anakiri kuwapo kwa mtoto Ushindi shuleni hapo ambaye alimpokea sambaba na mwingine kutoka Shirika la WoteSawa na kwamba wanaendelea vizuri kimasomo.
“Hawana utoro wa aina yoyote na kitabia wapo vizuri, hii inadhihirisha kwamba WoteSawa wanawalea vizuri. Wito wangu kwa wazazi wasikwepe jukumu la malezi tangu mtoto anapozaliwa na katika makuzi yake,” anasema Mwalimu Theresia na kuongeza:
“Mzazi anapomuachisha mtoto shule na kwenda kufanya kazi za ndani anakuwa amemkatisha ndoto zake, kwani huwezi jua mtoto huyo baadaye angekuwa nani,”.
Mmoja wa wananchi mkoani Mwanza Baltazary Mashaka, anaeleza kuwa mzazi mwenye uelewa hawezi kumkatisha mwanaye masomo ili akafanye kazi za ndani ambazo ni za muda tu.
“Mtoto akipata elimu na akasoma vizuri baadaye anaweza kuja kuwa msaada, kwahiyo unapomkatisha masomo ili akafanye kazi za ndani, unakuwa unamtendea ukatili na kufifisha ndoto zake za baadaye,” anasema Mashaka.
Kwa mujibu wa shirika la WoteSawa, kumekuwa na wimbi la watoto wenye umri chini ya miaka 14 kukatishwa masomo na kuajiriwa.
Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini ya mwaka 2004, mtoto chini ya miaka 14 anayeendelea na masomo haruhusiwi kufanya kazi wakati wa saa za shule na zaidi ya hapo haruhusiwi/hapaswi kufanya kazi kwa zaidi ya saa tatu kwa siku.
Kwa mujibu wa Shirika la Kazi Duniani (ILO) ajira kwa mtoto, ni kitendo cha mtoto husika kufanya kazi au shughuli ambazo ni hatari kwake au zinazoweza kuhatarisha ukuaji wake wa kimwili, kiakili, kijamii au kielimu.
Alikotokea Ushindi
Katika simulizi yake, Ushindi anaeleza kuwa alikuwa anaishi na shangazi yake katika kijiji cha Rufati kilichopo mkoani Dodoma ambako aliandikishwa darasa la kwanza baada ya kutimiza umri wa kuanza shule.
Binti huyo anasema wakati akiishi kwa shangazi yake huyo, alikuwa akiteswa kwa kupigwa na wakati mwingine kunyimwa mahitaji muhimu ya shule.
Anasema pamoja na manyanyaso hayo, alitakiwa kufanya kazi za nyumbani kabla ya kwenda shule na baada ya kurejea kutoka shuleni.
“Nilikuwa naamka asubuhi, nafanya kazi, lakini mtoto wake (wa shangazi yake) wa kiume na watoto wengine tuliokuwa tukiishi nao, wao walikuwa wakiamka tu, wanaenda shule,”anasema Ushindi na kuongeza:
“Nilikuwa naosha vyombo na kufagia uwanja, ndipo nijiandae kwenda shuleni. Kwa bahati wakati nasoma darasa la kwanza mwanzoni nilipewa mtihani nikafanya vizuri, wakanivusha darasa na kuingia la pili”.
Anaongeza kuwa alipoingia darasa la tatu, alimuomba shangazi yake amnunulie madaftari sita yaliokuwa yanahitajika lakini alimnunulia daftari moja tu.
“Kuna mwanafunzi alienda kwao na kuacha madaftari darasani, hivyo niliyachukua nikaanza kuyatumia, kwani alikua ameyaandikia kidogo. Baadhi ya wanafunzi wenzangu walikwenda kunishitaki kwa shangazi yangu”.
“Usiku alikata fimbo kubwa akaihifadhi, huku akinelekeza nifanye usafi. Nilivyomaliza tu, nikaenda kumwaga uchafu kisha nikatoroka moja kwa moja,” anaeleza Ushindi na kuongeza:
“Nilikimbia katikati ya mashamba ya alizeti mpaka nikafika karibu na nyumbani kwetu, lakini nikaogopa kwenda nyumbani kwa sababu mama yangu angenipiga na kunirudisha tena kwa shangazi. Niliakaa hapo na kujificha kwani kulikuwa na miti mirefu pia eneo hilo lilikuwa limepandwa mahindi”.
Ushindi anasema, alikaa katikati ya mahindi na alipochoka alipitiwa na usingizi, na alishtuka kutoka usingizini kukiwa tayari kumepambazuka. Anasema akiwa bado katikati ya mahindi, alimuona baba yake mdogo akipita kwa kutumia njia inayopita kwenye shamba hilo.
“Nilimwona baba mdogo, nilinyanyuka na kujisogeza ndani zaidi ili asinione,” anasimulia Ushindi na kuongeza kuwa akiwa katika harakati hizo, macho yake yaligongana na macho ya mama yake ambaye alikuwa upande tofauti na alikopita baba yake mdogo.
Anasema, mama yake alimchukua na kumpelekea nyumbani ambako alipewa chakula, baada ya kumweleza kwamba alikuwa akihisi a njaa na hapo alimweleza mzazi wake huyo yote yaliyomsibu. “Baada ya kumuhadithia mama alinielewa,” anasema Ushindi na kuongeza:
“Lakini baba mdogo aliporejea nyumbani na kunikuta, akataka wanirudishe kwa shangazi, lakini nikawaambia mimi sitaki kwenda tena kwa shangazi. Baadaye niliambiwa kwamba tutakwenda Dodoma mjini mimi na mama.” Kwa mujibu wa maelezo yake, huko alikopelekwa ni kwa mwanamke ambaye alimuunganisha na mtu mwingine ambaye baadaye alimsafirisha kwenda naye Mwanza.
Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009 inataja haki za msingi za mtoto na kuweka bayana kuwa uamuzi wowote kuhusu mtoto lazima uzingatie maslahi yake kama yanavyotajwa kwenye sheria na kanuni zake.
Kadhalika kanuni za utekelezaji wa sheria hiyo zinaweka bayana kwamba ni kosa kwa mzazi atakayeacha kumpeleka shule mtoto ambaye amefikisha umri wa miaka saba,na kwamba ni kosa kwa mzazi anayeshindwa kumsimamia mtoto wake mpaka atakapohitimu darasa la saba.
Kwa mujibu wa sheria hiyo na kanuni zake, utoro ni kosa la jinai na hivyo mtoto mtoro au mzazi ambaye anasababisha mtoto wake awe mtoro, wote wanaweza kushitakiwa kwa kosa la jinai.
Kauli ya Mama mzazi
Jitihada za Times Majira kumtafuta mama mzazi wa Ushindi kwa simu kwa zaidi ya siku saba kwa msaada wa shirika la WoteSawa hazikufanikiwa. Hata hivyo kwa mujibu wa shirika la WoteSawa mama huyo wa Ushindi alihojiwa kabla ya shirika kuanza kumuhudumia binti yake kwa kumpeleka shule.
Taarifa kutoka ndani ya Shirika hilo, zinasema kuwa alipohojiwa sababu za kumruhusu mtoto wake kwenda kufanya kazi za ndani badala ya kuendelea na shule, mama huyo alisema hali hiyo inatokana na ugumu wa maisha, hasa baada ya kutengana na baba wa mtoto huyo.
Ofisa Ustawi wa Jamii wa shirika la WoteSawa, Renalda Mambo anasema mama huyo alishindwa kumlea binti yake Ushindi kutokana na yeye kuishi maisha ya kuhamahama kwa ajili ya kufanya vibarua ili kujipatia kipato.
“Kwa maelezo yake kutokana nahali hiyo mama yake Ushindi aliona siyo vyema binti yake,akaishi maisha ya kutangatanga mara leo hapa kesho kule, hivyo alilazimika kumpeleka kwa bibi yake ambako pia ndiko alikokuwa anaishi na shangazi yake,” anasema Renalda.
Anasema kutokana na changamoto alizokuwa anapitia binti huyo kwa shangazi yake, siku moja alikuja mke wa mtoto wa mdogo wake na mama Ushindi (ambaye Ushindi anamuita wifi), amkuchukua binti huyo kwa makubaliano kuwa atamsaidia kumsomesha atakapomfikisha Mwanza.
Renalda anasema walipozungumza kwa simu na mama yake Ushindi, walibaini kwamba tayari mama huyo alikuwa na taarifa kuhusu mateso aliyokuwa akiyapata binti yake jijini Mwanza ambayo ni pamoja na kunyimwa chakula na jinsi ambavyo ahadi ya kusomeshwa kwake haikutekelezwa.
Kwa maelezo ya Renalda, mama yake Ushindi pia alionekana mwenye ufahamu wa jinsi binti yake alivyotoroka kutoka nyumbani kwa mtu alikokuwa akiishi na alifanya hivyo siku alipotumwa kwenda kuchukua fedha kwa wakala wa huduma za kifedha.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Foundation Karibu Tanzania (FKT), Asunta Ngatunga kati ya mwaka 2007 hadi 2024, wamehudumia watoto 900 na kati yao zaidi ya 700 sawa na asilimia 80 wakidaiwa kufanyiwa vitendo vya ukatili na ndugu zao wa karibu.
Ngatunga alikuwa akizungumza wakati Mtandao wa Polisi Wanawake Tanzania (TPF-Net) Mkoa wa Mwanza walipotembelea shirika la FKT na kutoa misaada kwa watoto waathirika wa vitendo vya ukatili.
Ripoti ya Haki za Binadamu iliyotolewa na Kituo ha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) ya 2021 inabainisha kuwa ukatili wa kimwili na kisaikolojia dhidi ya watoto ni miongoni mwa matukio yaliyobainika watoto kufanyiwa, yakishika nafasi ya pili nyuma ya ukatili wa kingono.
“Kupitia utafiti wa matukio yanayoripotiwa na vyombo vya habari na programu ya ufuatiliaji wa haki za binadamu, LHRC ilikusanya takribani matukio 57 ya ukatili wa kimwili na kisaikolojia dhidi ya watoto ,” inasomeka sehemu ya ripoti hiyo.
Kadhalika Ripoti ya Utafiti wa Utumikishwaji wa Watoto Tanzania ya mwaka 2014 iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), inabainisha kuwa asilimia 84.2 ya wafanyakazi wa ndani ni watoto wa kike huku asilimia 15.8 wakiwa ni watoto wa kiume.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo kati ya watoto milioni 15 wenye umri kati ya miaka 5 hadi 17, watoto milioni 4.2 sawa na asilimia 28.8 wanatumikishwa katika kazi mbalimbali za kiuchumi.
Wakati wa uzinduzi wa ripoti hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa NBS, Dkt. Albina Chuwa alisema utafiti huo unabainisha kuwa watoto wanafanya kazi zaidi katika sekta za kilimo, misitu na uvuvi ambazo zinaajiri asilimia 92.1 ya watoto wote wanaojishughulisha na shughuli za kiuchumi.
Ndoto na matamanio ya Ushindi
Ushindi anaeleza kuwa akimaliza masomo anatamani awe Rais kama alivyokuwa Hayati Dkt.John Magufuli na sasa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ili aweze kusaidia watoto wanaoonewa.
“Nilikuwa nampenda Magufuli kwasababu alikuwa akitatua matatizo ya watu. Pia alikuwa anatupenda hata sisi akisema shule zote wanafunzi wasome bure. Hivyo na mimi nikiwa Rais nitawatatulia wananchi matatizo yao au nikiwa mwanajeshi nitalinda taifa na watoto wasionewe,”anasema Ushindi na kuongeza:
“Nikikutana na Rais Samia nitamuomba atusaidie kuzuia njia zote mbaya ambazo wazazi wanatumia kupeleka watoto mjini kufanya kazi za ndani, pia shule zote nchini ziwe na chakula ambacho kinawatosha wanafunzi wote ili tufanye vizuri kwenye masomo.”
Ushindi anamuomba Rais Samia awezeshe shule zote za msingi ili ziwe bora kwa kujenga madarasa mengi mazuri yenye madawati ya kutosha ili wanafunzi wasibanane madarasani.
Oktoba 15,2023 Rais Samia alizindua shule za msingi zilizojengwa na Mradi wa kuimarisha Shule za Awali na Msingi (BOOST) katika shule ya msingi Imbele katika Manispaa ya Singida.
Uzinduzi huo ulifanywa kama alama ya kuzinduliwa kwa shule zote nchini zilizojengwa kupitia mradi huo ambao unasaidia watoto kupata elimu bora.
BOOST ni mradi unaotekelezwa kwa miaka mitano kuanzia mwaka 2021 kupitia Wizara za Elimu, Sayansi na Teknolojia na Ofisi ya Rais-Tamisemi chini ya ufadhili wa Benki ya Dunia. unataraji kugharimu shilingi tirioni 1.5.
Taarifa za serikali zinaonesha kuwa hadi Septemba 2023 Sh. Bilioni 230 zilikuwa zimeishatolewa huku ujenzi wa shule za msingi 194, madarasa ya awali 364 na , madarasa ya shule za msingi 2,303 ukiwa umekamilika.
Kudhibiti utumikishaji watoto.
Pia Ushindi anaiomba Serikali iwadhibiti wazazi na ambao wanataka watoto wao kufanya kazi katika umri mdogo pamoja na wale wanaowatorosha wanafunzi kwa ajili ya kuwatumikisha kazi mbalimbali, ili kukomesha tabia hizo.
“Wasiwapeleke mjini kufanya kazi kwa sababu kuna mambo mengi, kwani watoto wao wanaweza kuteswa na wengine kugeuka kuwa watoto wa mitaani.
“Mama yangu aliambiwa nakuja Mwanza kusoma, lakini niliishia kufanyishwa kazi za ndani nikiwa na miaka 10 na isingekuwa bahati ya kukutana na yule mama msamaria aliyenpeleka polisi na baadaye kuletwa hapa WoteSawa, sijui ningekuwa wapi,” anasema Ushindi.
Kadhalika analiomba shirika la WoteSawa, liendelee kuwasaidia wasichana ambao wanateseka na wanaokatishwa masomo kutokana na sababu mbalimbali na kujikuta wanafanya kazi za ndani ili nao waweze kutimiza ndoto zao.
Ofisa Ustawi wa Jamii wa Shirika la WoteSawa Renalda Mambo, anaeleza kuwa mwaka 2023 walipokea kesi 19 za watoto wenye umri chini ya miaka 14 waliokuwa wameajiriwa katika kazi za nyumbani, huku kukiwa kesi 67 za wafanyakazi wa nyumbani waliokuwa wamedhulumiwa mishahara yao, vipigo na kubakwa.
Renalda anasema shirika hilo limeweka kituo katika Wilaya ya Ngara mkoani Kagera kwa ajili ya kuzuia watoto wanaotoka wilayani humo kwenda Mwanza kwa ajili ya kutumikishwa kwenye kazi za nyumbani.
“Januari hadi Novemba 2023, tulifanikiwa kuokoa watoto 53. Tunafanya kazi hii kwa kushirikiana na viongozi wa serikali za mitaa, Ofisa Ustawi, Polisi, Dawati la Jinsia na Watoto, Mahakama na wasamaria wema ili kuhakikisha tunapata taarifa mbalimbali zinazohusu ukatili dhidi ya wafanyakazi wa nyumbani,” anasema Renalda.
Anasema uzoefu unaonesha kuwa wakati watoto wanatumikishwa kwa kazi za nyumbani, baadhi ya wazazi hupokea mshahara wa mtoto.
“Umaskini ni kikwazo kwa watoto hawa hasa wenye umri mdogo, kwani kwa mujibu wa sheria mtoto mwenye umri chini ya miaka 14 haruhusiwi kufanya kazi za ndani lakini ukiangalia shirika letu tumekuwa tukiwaokoa wenye miaka 9, 12 na 13,” anasema Renalda.
Takwimu zilizotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbroad Mutafungwa zinaeleza kuwa mwaka 2022 yaliripotiwa matukio ya kutoroshwa wanafunzi 31 na kwamba mwaka 2023 yaliripotiwa matukio 30 na kati ya Januari na Aprili,2024 yalikuwa yameripotiwa matukio 8..
Kwa upande wa ukatili kwa watoto mwaka 2022 kulikuwa na matukio 72, mwaka 2023 matukio 63 na kati ya Januari na Aprili 2024 yalikuwa yameripotiwa matukio 25.
More Stories
Miaka 63 ya Uhuru na rekodi treni ya SGR
Alama saba muhimu za Rais Samia kwenye mkutano G20
Mageuzi yanayofanywa na Rais Samia kwa mashirika ya umma kuongeza tija