Na Allan Kitwe, Timesmajira ,Arusha
VYAMA vya Ushirika wa Akiba na Mikopo nchini (SACCOS) vimetakiwa kufanya kazi kwa weledi na uadilifu mkubwa ili mali na fedha za wanachama wao zitumike kuboresha maisha yao.
Rai hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Rasilimali Watu wa Wizara ya Fedha, Lusius Mwenda alipokuwa akifungua Mkutano Mkuu wa 12 wa mwaka wa Hazina SACCOS uliofanyika katika ukumbi wa AICC Jijini Arusha.
Amesema kuwa baadhi ya SACCOS zimekuwa hazisimamii ipasavyo mali na fedha za michango ya wanachama wao hali inayopelekea vyama hivyo kutoaminika ikiwemo kusababisha upotevu wa mali za wanachama.
Mwenda amesisitiza kuwa serikali inafuatilia kwa karibu zaidi utendaji wa SACCOS zote na kuonya kuwa chama chochote kitakachobainika kutumia vibaya mali na fedha za wanachama wake kitachukuliwa hatua kali za kisheria.

‘Viongozi mliopewa dhamana ya kusimamia SACCOS fanyeni kazi kwa uadilifu mkubwa, hatutaki kusikia vitendo vya ubadhirifu wala matumizi mabaya ya rasilimali zao, kinyume na hapo tutachukua hatua kali kwa waliohusika’, ameeleza.
Mwenda amepongeza Uongozi wa Hazina SACCOS kwa kusimamia vizuri rasilimali za wanachama wao na kumwezesha mtu mmoja mmoja kuinuka kiuchumi kupitia huduma za mikopo zinazotolewa.
Amefafanua kuwa Viongozi wa SACCOS wanapaswa kuwa waaminifu na kuonesha weledi katika kusimamia mabilioni ya fedha za michango ya wanachama wao, yeyote atakayebainika kutumia nafasi yake kujinufaisha atawajibika.
Malengo ya Vyama vya Akiba na Mikopo ni kuboresha maisha ya wanachama wao kupitia huduma za kifedha, siyo kuwa chanzo cha migogoro na hasara, hivyo akaonya kuwa Wizara haitasita kuchukua hatua kwa chama chochote.
Mtendaji Mkuu wa Hazina SACCOS, Dkt. Festo Mwaipaja, ameeleza kuwa chama hicho ni mkombozi kwa waajiriwa wote wa serikali na hata waajiriwa wapya wanapata mkopo ili kuwaepusha na changamoto za ugumu wa maisha.
Amebainisha kuwa mikopo hiyo yenye riba nafuu hutolewa ndani ya masaa 24 ili kuwaondolea changamoto za ugumu wa maisha hasa wanapoanza ajira katika utumishi wa umma.
Ameeleza mafanikio makubwa yaliyopatikana kuwa ni kuongezeka wanachama kutoka 8,889 hadi 9,806, thamani ya mali kupanda kutoka sh bilioni 36.3 hadi bilioni 45.3, akiba na amana za wanachama kufikia sh bilioni 38.6, na hisa kupanda hadi sh bilioni 4.56.

More Stories
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako
TTCL yaadhimisha siku ya Wanawake kwa kutoa msaada JKCI
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi