Na Ashura Jumapili ,TimesMajira online,Karagwe
Watu saba wamepoteza maisha huku wengine tisa wakijeruhiwa katika ajali iliyohusisha magari matatu katika kizuizi cha barabarani kilichopo kijiji cha Kihanga Kata ya Kihanga Wilaya ya Karagwe mkoani Kagera,huku chanzo cha ajali hiyo ikidaiwa ni uzembe wa dereva wa lori aina ya scania yenye namba T621 AJQ na Trela namba T472 EAQ.
Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Kagera Blasius Chatanda,amehibitisha kutokea kwa ajali hiyo Desemba 03,2014 saa 5:00 asubuhi,ikihusisha lori aina ya scania yenye namba T621 AJQ na Trela namba T472 EAQ likiwa linatokea Kayanga Wilaya ya Karagwe kwenda Kyaka lilipofika Kihanga katika kizuizi cha barabarani yalikuwepo magari mawili.
Moja lilikuwa costa namba T367 ECP pamoja na toyota haice yenye namba za usajili T973 DGD,yakiwa yamesimama yanaendelea kukaguliwa na Maofisa Uhamiaji mita takribani kumi kutoka kwenye kizuizi ndipo Scania iliyagonga kutokea nyuma na kusababisha ajali hiyo.
Amesema uzembe wa dereva umesababisha ajali hiyo,inaonekana alikuja katika mwendo mkali na haikusababishwa na kufeli breki,kwani huko nyuma alikotoka alipita katika mlima wa Kishoju na kwenye kona hivyo ingekuwa breki ule mteremko asingeumaliza.
“Gari hilo limetokea Mbeya likiwa limebeba mchele kuupeleka Mtukula na baada ya kushusha mchele lilipata mzigo mwingine Karagwe wa kurudi nao Mbeya ambayo ni parachichi.Huyu dereva ni mgeni katika eneo hilo, kutokana na uzembe na kutokuchukua tahadhari,alikuja katika mwendo ambao ni mkali akaigonga toyota haice pamoja na costa,” amesema Chatanda
Amesema watu saba wamefariki katika ajali hiyo kati yao wanawake wanne, mwanaume mmoja na watoto wawili huku majeruhi wakiwa tisa wanaume wanne na wanawake watano.
“Ni wazi kwamba tahadhari za alama barabarani hakuzichukua kwani barabara hiyo inazo alama za barabara na hata kabla ya kizuizi kuna alama pia” amesema Chatanda
Mmoja wa mashuhuda wa ajali hiyo,Adamu Alon mtengeneza majokofu kutoka Kayanga amesema kuwa, ameitwa na mteja Kyaka wilaya ya Misenyi na kupanda Kosta ambayo imehusika kwenye ajali walivyofika Mgakorongo walikuta hilo lori likiwa limesimama dereva anaongea na askari wa usalama barabarani wakapita.
Amesema, wakati gari hilo limefika Kihanga katika kizuizi cha barabarani ndipo Scania hiyo ikagonga gari lao likiwa linakaguliwa na Maofisa Uhamiaji.
“Nilikuwa nimekaa kiti cha mbele na dereva wakati tunatakiwa kuonesha kitambulisho na Ofisa Uhamiaji ndipo nikasikia kishindo na gari ambalo nilikuwemo likahama na kwenda mbele.Mimi na Ofisa Uhamiaji,tulidondoka chini baadaye nilipopata fahamu niliona scania tulioipita Mgakorongo ndiyo imetugonga,”.
Majeruhi wamelazwa katika hospitali ya Wilaya ya Karagwe iliyopo Nyakanongo pamoja na miili ya marehemu imehifadhiwa katika hospitali hiyo.
More Stories
Kamati ya Mfuko wa Jimbo Musoma Vijijini yagawa vifaa vya ujenzi
Hatma mrithi wa Kinana kupatikana
Mrithi wa Kinana CCM kujulikana katika Mkutano Mkuu wa Jan 18/19