December 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Saba mbaroni kwa tuhuma za udanganyifu mtihani wa darasa la 7

Judith Ferdinand, Timesmajira Online, Mwanza

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza limewahoji watu saba kwa tuhuma za kosa la udanganyifu wa mtihani ya darasa la saba kwa kuwachukua wanafunzi wa sekondari na kuwafanyisha mtihani huo kwa niaba ya wanafunzi wa darasa la saba.

Akizungumza jijini hapa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza SACP.Wilbord Mutafungwa, ameeleza kuwa tukio hilo lilitokea Septemba 13,2023 majira ya saa nane mchana shule ya msingi Igulumuki,Kata ya Igulumuki Tarafa ya Sengerema wakati kamati ya mitihani ya wilaya ya Sengerema ilipotembelea shule hiyo kwa ajili ukaguzi na kubaini kufanyika kwa udanganyifu huo.

Ambapo mkondo namba mbili na namba tatu kulikuwa kumeingizwa wanafunzi wa sekondari watatu na kufanya mitihani ya darasa la saba.

Mutafungwa amewataja watuhumiwa waliokamatwa na wanaendelea kuhojiwa ni Maiko Sheusi,(35) Mwalimu wa shule ya sekondari Sima ambaye ni msimamizi Mkuu iwa mtihani shule ya msingi Igulumuki,Musa Mwashihava (38),Mwalimu wa shule ya sekondari Kilabela ambaye ni Msimamizi wa mtihani mkondo namba 2.

Huku wengine ni Bonasi Balozi(33),Mwalimu wa shule ya sekondari Buzilasoga ambaye alikuwa msimamizi wa mtihani mkondo namba 3, Azizi Mohamed(36) ,Mwalimu wa Taaluma shule ya msingi Igulumuki ,Shadrack Bwana (14) mwanafunzi wa shule ya sekondari Sima, Revocatus Paulo(14) mwanafunzi wa shule ya sekondari Sima pamoja na Pendo Bukoma(14) mwanafunzi wa shule ya sekondari Sima mkazi wa Igulumuki.

“Kufuatia tukio hilo Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi Igulumuki aitwaye Amlesian Mahingu Mfungo aliweza kukimbia mpaka tunaendelea na jitihada za kumsaka ili aweze kukamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria,watuhumiwa wote wamehojiwa kwa kina na watafikishwa mahakamani haraka iwezekanavyo baada ya upelelezi kukamilika,”ameeleza Mutafungwa.

Pia ameeleza kuwa jeshi hilo Mkoa wa Mwanza pamoja na kutoa elimu limeendelea kuimarisha ulinzi maeneo yote na halitasita kuchukua hatua kali za kisheria kwa wahalifu.