December 22, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Getrude Rwakatare 1950-2020

Na Mwandishi Wetu

KIFO cha ghafla Mchungaji wa Kanisa la Mlima wa Moto (Mikocheni B Assemblies of God ) Mchungaji Getrude Rwakatare (70) kimepokelewa kwa mshtuko na simanzi kubwa na Watanzania wakiongozwa na Rais John Magufuli.

Kifo cha Mchungaji Rwakatare kilichotokea jana alfajiri na taarifa za awali za kifo chake kuthibitishwa na mtoto wake, Muta Rwakatare, kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii akisema alikuwa akisumbuliwa na shinikizo la damu.

“Ni bahati mbaya imetokea asubuhi ya leo (jana) saa 11 kasoro, alikuwa na matatizo ya moyo, jana tulimkimbiza hospitali lakini bahati mbaya imetokea, tupo katika hatua ya kuangalia namna gani tutafanya ili tuweze kumpumzisha mama yetu,” alisema Muta.

Kufuatia kifo hicho, Rais John Magufuli na Spika wa Bunge, Job Ndugai, walituma salama za rambirambi kwa familia ya Mchungaji Rwakatare, ambaye alikuwa Mbunge wa viti maalum kwa tiketi ya CCM.

Rais Magufuli alituma salamu za rambirambi kwa familia, wabunge na waumini wa Kanisa la Mlima wa Moto kufuatia kifo hicho kilichotokea jijini Dar es Salaam.

Katika salamu hizo, Rais Magufuli alielezea kusikitishwa na kifo cha Mchungaji Rwakatare akisema alikuwa mcha Mungu, mwenye upendo, asiye na majivuno, aliyepigania umoja na amani na aliyeipenda nchi yake kwa dhati.

Pamoja na kutoa pole kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki, Rais Magufuli alimuomba Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai kufikisha salamu zake za pole kwa wabunge wote na pia amewapa pole waumini wa Kanisa la Mlima wa Moto ambalo alikuwa kiongozi wake.

“Katika kipindi hiki cha majonzi, tumuombee Mchungaji Rwakatare apumzike mahali pema peponi na nawasihi waumini wa Kanisa la Mlima wa Moto muendelee kuwa wamoja na muendeleze mazuri yote yaliyofanywa na Mchungaji Rwakatare wakati wa uhai wake” alisema Rais Magufuli.

Spika Ndugai

Kufuatia kifo hicho,  Spika Ndugai alitoa taarifa kwa vyombo vya habari akitangaza kifo ch Mchungaji Rwakatare kilichotokea  alfajiri ya jana.

“Nimepokea kwa mshtuko na masikitiko makubwa taarifa za kifo cha Mheshimiwa Rwakatare. Natoa pole kwa wafiwa wote wakiwemo familia ya marehemu na Mungu awape uvumilivu na subira katika kipindi hiki,” alisema Spika Ndugai.Mchungaji Rwakatare alizaliwa Desemba 31, 1950.

CCM

Wakati huo huo, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimesema kimepokea kwa mshtuko na huzuni kubwa taarifa za kifo cha Mchungaji Rwakatare, ambaye amekuwa Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Morogoro kwa tiketi CCM.

Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa Dar es Salaam jana na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole, ilieleza kuwa Mchungaji Rwakatare pamoja na majukumu ya kichama na kibunge amekuwa kiongozi wa kiroho.

“Amekuwa na mchango mkubwa katika kukuza na kuimarisha Maisha ya kiimani na kiroho ya waumini na Watanzania wengi.  Mama Rwakatare wakati wote wa uongozi wake alikuwa sehemu ya viongozi wa kisiasa na kiimani ambao waliamini katika uelewa wa pamoja wa matarajio ya kisiasa ya Watanzania, ujenzi wa siasa safi na za kimaendeleo, alihubiri na kusimamia haki, amekuwa kiongozi shupavu, Mama wa familia, Mama wa kiimani na kiroho kwa wengi,” alisema Pole pole kupitia taarifa hiyo kwa vyombo vya habari.

Alisema uongozi wa CCM chini ya Mwenyekiti wa CCM, Rais Magufuli na Katibu Mkuu wa CCM, Bashiru Ally unatoa salamu za pole kwa familia ya Marehemu, ndugu, jamaa, marafiki, waumini wa Kanisa la Mlima wa Moto, wanachama wa CCM wa Mkoa wa Morogoro na hasa Wilaya ya Kilombero na wote walioguswa na msiba huu.