Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online
Wakala wa Nishati Vijijini (REA), umesema utahakikisha unashirikiana na sekta binafsi katika kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora na nishati ya uhakika vijijini.
Mkurugenzi wa Teknolojia za Nishati Jadidifu na Nishati Mbadala wa REA, Mhandisi Advera Mwijage amesema hayo baada ya kukagua maendeleo ya mradi wa ujenzi wa umeme wa maji (kilovoti 2400) wa Idete wilayani Kilolo unaotekelezwa na Kampuni ya Lung’ali Natural Resources Co ltd.
Amesema, REA mpaka sasa imeishatoa ruzuku ya shilingi bilioni 4 kwa mradi huo ulio chini ya Kanisa Katoliki mkoani Iringa ambazo zimetumika kwa utafiti wa mazingira, ujenzi wa bomba la maji na jengo lenye mtambo wa kuzalishia umeme (Power House).
Pia, amesema, REA ina wajibu wa kuwaunganisha wazalishaji wadogo na taasisi zinazotoa mikopo kwa riba nafuu ambapo Benki ya TIB, imeikopesha kampuni hiyo ili ikamilishe mradi huo wa umeme kwa wakati na kuingiza kwenye gridi ya taifa.
“REA inafanya kazi na sekta binafsi katika kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora ya nishati vijijini na kuchangia katika
shughuli za uchumi zinazoongeza kipato kwa wananchi,” amesema Mhandisi Mwijage.
Ameongeza,m serikali peke yake haiwezi kufanya kila kitu hasa katika miradi ya maendeleo inayogusa wananchi na hivyo kutambua
umuhimu wa ushiriki wa sekta binafsi.
Serikali imekuwa ikiipatia REA fedha ili kuwawezesha kufadhili miradi ya wazalishaji wadogo binafsi wa umeme, ili miradi hiyo ichangie katika kiasi cha umeme
kinachozalishwa katika gridi ya taifa .
Mhandisi Mwijage ameweka wazi umuhimu wa wazalishaji wadogo wa umeme, katika
maendeleo ya wananchi, na kusema serikali itaendelea kushirikiana nao.
Akieleza zaidi, amesema miradi ya uzalishaji umeme wa maji inasaidia kupunguza uzalishaji wa hewa ya ukaa na inatunza mazingira hasa kwa kuwezesha kuachana na matumizi ya jenerata katika kuzalisha umeme.
“Miradi hii pia inaiongezea serikali kipato kwa kulipa kodi, kuzalisha ajira na kuwapa wananchi uhakika wa upatikanaji wa umeme na hivyo kushiriki kikamilifu katika shughuli za kujiongezea kipato,” amesema Mkurugenzi wa Nishati Mbadala na Teknolojia.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni inayozalisha umeme huo wa maji, Lung’ali Natural Resources, Padre Luciano Mpoma amesema
wanatarajia kuanza uzalishaji wa umeme Januari mwakani na kwamba ujenzi unaendelea vizuri.
Mradi huo utakapokamilika amesema, wananchi wa Idete na maeneo mengine watakuwa na umeme wa uhakika na hivyo kuweza kushiriki kikamilifu
katika shughuli za kiuchumi na huduma za kijamii.
Naye Mwenyekiti wa Kata ya Kidete, Henry Kikoti ameelezea shauku ya wananchi kutaka mradi huo ukamilike kwani utaenda kuwa suluhu kwa umeme wa uhakika kwani uliopo hautoshelezi mahitaji ya shughuli za kiuchumi hasa kutokana na maendeleo na uwekezaji wa wananchi katika
nyanja mbalimbali za kiuchumi.
More Stories
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa
NLD kipo tayari kwa uchaguzi wa Serikali za Mitaa