June 11, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

RUWASA yakamilisha ujenzi wa visima Korogwe

Na Yusuph Mussa,Timesmajiraonline,Korogwe

WAKALA wa Majisafi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Wilaya ya Korogwe kupitia program ya visima 900 nchini, imetekeleza ujenzi wa visima vinane, ambapo vitano vimejengwa Jimbo la Korogwe Vijijini na vitatu Jimbo la Korogwe Mjini na kukamilika kwa asilimia 100.

Hayo yamesemwa Juni 9, 2025 na Meneja wa RUWASA Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga Muharami Mohamed wakati anasoma taarifa mbele ya Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa Ismail Ali Ussi alipofika kuweka Jiwe la Ufunguzi Mradi wa Visima na Point Source katika vijiji vya Mgombezi, Mgambo na Kwamngumi (Kilole Mzee), uliofanyika Mtaa wa Mgombezi.

“Mradi huu umetekelezwa kwa muda wa miezi mitano kuanzia Disemba 16, 2024 hadi Mei 30, 2025 kupitia fedha za lipa kwa matokeo (PforR). Mradi huu wa visima vinane (8) umetekelezwa na wakandarasi wawili kwa jumla ya sh.
481,472,450, ambapo Hydro Experts and Civil Works Company Ltd amechimba visima vinane (8) kwa Mkataba Na. TR140/025/2024/2025/W/49 wenye thamani ya sh. 247,974,050.

“Na Frangem International Ltd amejenga
miundombinu ya maji (Water Point Source) katika visima vyote vinane (8) kwa Mkataba Na.TR140/025/2024/2025/W/50 wenye thamani ya sh. 233,498,400. Kwa eneo la Korogwe mjini ambalo tupo leo, kazi zilizopangwa na kutekelezwa ni
uchimbaji wa visima vitatu, ujenzi wa vibanda vyenye minara ya kuwekea matangi, kufunga matanki ya plastiki yenye ujazo wa lita 10,000 kila moja”amesema Mhandisi Mohamed.

Mhandisi Mohamed amesema kazi nyingine ni kufunga bomba (Plumbing work),kuunga umeme kwenye point source tatu na Kufunga pump tatu, kazi hizi zote zimekamilika mnamo Mei 30, 2025 kwa asilimia 100. Gharama ya uchimbaji na ujenzi wa visima hivyo vitatu ni sh. 180,552,168, ambapo hadi kukamilika kwake jumla ya sh. 136,344,802 zimelipwa kwa wakandarasi wote wawili.

“Maji yanayozalishwa katika visima hivi vitatu ni lita za ujazo 49,320 (Mgombezi 26,400, Kilole Mzee 19,200 na Mgambo 3,720) kwa saa. Kiasi hiki cha maji kimeongeza hali ya huduma (coverage) kutoka asilimia 82 hadi kufika asilimia 84.5 ya sasa. Ili mradi huu uwe endelevu utakabidhiwa kwa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira HTM kwa ajili ya uendeshaji na matengenezo.

“Kwa niaba ya wananchi, tunamshukuru Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuondoa kero ya maji kwa wananchi wapatao 7,232 wa vijiji vya Mgombezi, Kilole Mzee na Mgambo” amesema Mhandisi Mohamed.

Akizungumza na wananchi waliofika kwenye ufunguzi huo, Ussi aliwataka kulinda vyanzo vya maji na miundombinu ili miradi ya maji iwe endelevu, kwani walinzi wa kwanza wa miundombinu ya maji ni wananchi wenyewe ambao huduma hiyo imewalenga wao wenyewe moja kwa moja.