May 8, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

RUWASA yaagizwa kufanya utafiti kutoa maji Kinyamwenda kwenda Gairu

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma

NAIBU Waziri wa Maji Mhandisi Matthew Kundo amemuagiza Meneja wa Wakala wa Maji Mijini na Vijijini (RUWASA) Mkoa wa Singida afanye utafiti na kujiridhisha kama maji kutoka mradi wa Kinyamwenda yanaweza kufikishwa Kijiji Cha Gairu ili kutatua changamoto ya maji kwa wananchi wa Gairu.

Mhandisi Kundo ameyasema hayo Mei 7,2025 kufuatia swali la nyongeza la Mbunge wa Singida Kaskazini Abeid Ighondo ambaye alihoji Serikali kwa nini Serikali isichukue maji kwenye mradi wa Kinyamwenda Badala ya kuchukulia mradi wa Sagara ambao upo mbali na wananchi na hivyo hivyo kuendelea kusababisha adha ya maji.

“Badala ya kuchukua maji kwenye mradi wa Sagara kwa nini tusichukue kwenye mradi wa kinyamwenda ambao unatoa maji lita 20,000 kwa saa na unaweza kusambaza vijiji zaidi ya vitano na utawezesha  kupeleka maji na kitongoji cha Misuna ambacho kipo karibu na kitongoji Cha Gairu ambacho kinapata maji yasiyo salama kwa matumizi ya binadamu, lakini pia tungeweza kuchukua maji ya Sagara yakapelekwa kitongoji cha Mangida “amehoji Ighondo na kuongeza kuwa

“Kitongoji cha Muungano kilichopo Kijiji Cha Mpambaa hawana maji, lakini kitongoji hicho kina miradi ya migodi ya Madini ya dhahabu Serikali ina Mpango gani wa kuwapatia wananchi hawa kisima cha maji kinachoweza kuondoa changamoto hiyo lakini pia kingeweza kuondoa changamoto maeneo ya migodi?”

Akijibu maswali hayo Mhandisi Kundo amekiri kwamba ni kweli Gairu kwenda Sagara kuna umbali na kwamba lengo la Serikali ni kwamba mradi unapokamilika maji yapatikane kwa gharama nafuu .

Aidha amesema amepokea ushauri wa Mbunge huku akisema,kuna mradi wa milioni 950 maeneo ya Kinyamwenda na hivyo kutumia fursa hiyo kumwelekeza Meneja wa RUWASA Mkoa wa Singida kuona namna ya mradi wa Kinyamwenda unavyoweza kufukisha maji kitongoji cha Gairu pamoja na vijiji na vitongoji ambavyo vimezunguka mradi huo.

Pia Mhandisi Kundo amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha wananchi wake wanapata maji safi na salama na hivyo wataenda   kufanya utafiti pale ajiridhishe ukubwa wa tatizo Ili kuona kama kitachimbwa kisima kingine au  kama ni kupanua skimu nyingine ifikishe maji ,Serikali itafanya hivyo  hivyo.

Katika swali la msingi Ighondo alitaka kujua lini Serikali itasambaza maji salama katika Kitongoji cha Gairu Kijiji cha Sagara ambao wanatumia maji yenye chumvi. 

Akijibu swali hilo,Mhandisi Kundo amesema  lengo la Serikali ni kuhakikisha huduma ya majisafi na salama inapatikana kwa wananchi waishio vijijini ikiwemo Kitongoji cha Gairu ambacho kwa sasa kwa sehemu kinapata huduma kupitia Skimu ya Maji ya Sagara.

Hata hivyo Mbunge Ighondo akatoa taarifa kwamba wananchi wa Gairu hawapati maji katika mradi wa Sagara kwa sababu ya umbali uliopo huku akisema mradi wa Sagara upo mlimani hivyo wananchi wanashindwa kupanda mlima kufuata maji hayo