Na Moses Ng’wat,Timesmajiraonline,Ileje.
MKUU wa Mkoa wa Songwe, Dkt.Francis Michael, ameagiza Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (Ruwasa) mkoani Songwe, kuhakikisha kuwa shule ya wasichana ya Ileje (Ileje Girls) inapatiwa huduma ya maji ndani ya siku tatu, ikiwemo kupeleka mtambo wa kuchimba kisima ili kupata ufumbuzi wa kudumu wa tatizo la ukosefu maji kwa wanafunzi shuleni hapo.
Dkt. Michael ametoa agizo hilo, Novemba 3, 2033 mara baada ya kufanya ziara kwenye shule hiyo, kwa ajili ya kukagua Maendeleo ya Ujenzi wa majengo mawili ambayo ni nyumba moja ya Mwalimu itakayotumiwa na familia mbili, inayogharimu kiasi cha sh. Milioni 100 ambazo ni fedha kutoka serikali Kuu, pamoja na jengo la Maktaba.
Mkuu wa Mkoa amechukua hatua hiyo, baada ya Mkuu wa shule hiyo, Valeria Haule, kueleza changamoto ya ukosefu wa maji shuleni hapo, ambapo alisema inawalazimu kila siku kununua maji kutoka kwa wachuuzi.
Baada ya kupokea changamoto hiyo, Mkuu wa Mkoa alilazimika kumpigia simu Meneja wa Ruwasa Mkoa wa Songwe, Mhandisi Charles Pambe, na kumtaka kupeleka timu ya wataalam wa maji katika shule hiyo kwa ajili ya kupeleka mabomba yatakayotumika kutoa maji kwenye kisima kilichokuwa kikitumiwa na Mkandarasi wa Barabara Mpemba – Isongole hadi kuyafikisha shuleni hapo.
Mbali na kupeleka maji hayo ya kisima kwa dhararua, pia Mkuu wa Mkoa alimtaka Meneja huyo wa Ruwasa kupeleka mtambo shuleni hapo kwa ajili ya kuchimba kisima kitakachomaliza kabisa tatizo hilo la ukosefu wa maji.
“Meneja umeniambia una magari matatu ya kuchimba visima yapo Tunduma, sasa nataka hadi kufika jumapili (Novemba 5, 2023) uwe umeleta gari moja na kuanza kuchimba kisima hapa” alitoa maelekezo hayo kwa njia ya simu.
Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa Mkoa alimuagiza Wakala wa Barabara nchini (Tanroads) kuruhusu moja ya nyumba zilizokuwa zikitumiwa na Mkandarasi alijenga barabara ya Mpemba- Isongole itumike kwa ajili ya bweni kwa ajili ya wanafunzi hao wa kike, kwani tayari Tanroads ilishatoa nyumba nyingine mbili zinazotumika kama mabweni katika shule hiyo.
Awali katika taarifa yake, Mkuu wa shule hiyo, Haule alisema bweni moja lilikuwa likilaza wanafunzi 38, hivyo kupata nyumba moja kutasaidia kupunguza msongamano, wakati wanajipanga kujenga mabweni ya kudumu shuleni hapo.
More Stories
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa Â
Polisi Mbeya yawataka waandishi wa habari kutoa taarifa sahihi