December 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

RUWASA waja na Luku kukomesha tatizo la maji hewa

Na Yusuph Mussa, Timesmajira Online Mbeya

WAKALA wa Maji Safi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) wamekuja na mwarobaini wa kumaliza tatizo la wananchi kupata maji hewa kwa kuanzisha dira za maji za lipia maji kadri utumiavyo (Maji ya Luku) ambazo zitatumia kadi na sarafu ili kupata huduma ya maji nyumbani.

Ofisa Maendeleo ya Jamii RUWASA Makao Makuu, Mahadia Mkandason (wa tatu kushoto) akiwaonesha wananchi kadi itakayotumika kwenye Maji ya Luku (Mita), katika banda la RUWASA lililopo kwenye maonesho ya Kimataifa ya Nane Nane yanayofanyika kwenye Viwanja vya Mwakangale jijini Mbeya.

Pia dira hizo za maji za malipo kabla ya matumizi ambazo zitafungwa katika skimu za maji vijijini, malipo ya maji yataunganishwa na Mfumo wa Malipo ya Serikali (GePG) ili kuona fedha za Serikali hazipotei ama kuliwa zikiwa mbichi.

Hayo yamesemwa Agosti 3, 2023 na Ofisa Uhusiano wa RUWASA Makao Makuu Ramadhan Juma wakati anazungumza na mwandishi wa habari hizi kwenye banda la RUWASA lililopo katika maonesho ya Kimataifa ya Nane Nane yanayofanyika kwenye Viwanja vya Mwakangale jijini Mbeya.

Juma amesema, wapo kwenye majaribio ya kutumia dira (mita) hizo ambazo zinatengenezwa na vyuo viwili hapa nchini ambavyo ni Chuo Kikuu cha Sayansi Mbeya (MUST) na Chuo cha Sayansi cha Arusha, nia ikiwa kutaka kuboresha upatikanaji wa maji, lakini pia kuona wananchi wanalipia maji kwa kadri wanavyotumia.

“Katika kuboresha makusanyo ya fedha kwenye miradi ya maji vijijini, RUWASA imeingia makubaliano na Chuo cha Ufundi cha Arusha, Chuo Kikuu cha Sayansi Mbeya na Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) kupitia kampuni yake tanzu DTB ili kubuni dira za maji za malipo kabla ya matumizi (pre-paid water meters), ambazo zitafungwa katika skimu za maji vijijini,”.

Afisa Uhusiano wa RUWASA Makao Makuu Ramadhan Juma (kushoto), akitoa maelezo kwa mmoja wa wananchi waliotembelea banda la RUWASA kwenye maonesho ya Kimataifa ya Nane Nane yanayofanyika kwenye Viwanja vya Mwakangale jijini Mbeya.

Pia amesema RUWASA imefungua akaunti kila mkoa, ambazo zitapokea fedha za malipo ya mauzo ya maji ambazo zinazokusanywa zitakuwa zikitumwa kwenda kwa vyombo vya watoa huduma ngazi ya jamii (CBWSOs) husika kwa awamu kutegemeana na mpango wa matumizi ya fedha ulioidhinishwa.

Afisa Maendeleo ya Jamii RUWASA Makao Makuu, Mahadia Mkandason (kushoto) akitoa maelezo kwa wananchi waliotembelea banda la RUWASA lililopo kwenye Maonesho ya Kimataifa ya Nane Nane yanayofanyika kwenye Viwanja vya Mwakangale jijini Mbeya.

Juma amesema RUWASA imepata mafanikio makubwa tangu kuanzishwa kwake Juni, 2019, ambapo imeweza kuongeza upatikanaji wa maji vijijini kutoka asilimia 64.8 hadi kufikia asilimia 77 za sasa huku nia yao ni kufikia asilimia 85 ya utoaji wa maji vijijini ifikapo mwaka 2025.

“Adhima yao ya kutoa huduma ya maji kwa wananchi imeonekana kwenda vizuri, kwani upatikanaji maji kitaifa umefikia asilimia 77 za utoaji huduma ya maji vijijini, ukilinganisha na upatikanaji wa maji kitaifa wa asilimia 64.8 kabla ya kuanzishwa RUWASA Juni, 2019.

“Kwango hicho ni kikubwa kwa miaka takribani mitatu nia yetu ni kufikia asilimia 85 ya upatikanaji wa maji vijijini ifikapo mwaka 2025,hivyo tunawaahidi wananchi kuwa tutaendelea kuwatumikia na kuhakikisha maji yanawafikia hadi nyumbani kwao,”amesema Juma.