January 30, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

RUWASA Katavi yasaini mkataba ujenzi bwawa la Nsekwa

Na George Mwigulu,Timesmajiraonline,Katavi.

WAKALA wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Mkoa wa Katavi, inaendelea kuchukua hatua za makusudi kuimarisha huduma ya maji safi salama ili kuchochea jamii yenye afya njema na ustawi wa maendeleo kupitia maji safi ya kunywa.

Ili kufanikisha adhima hiyo,RUWASA Januari 27, 2025 imeingia makubaliano ya utiaji saini  wa mkataba na Mkadarasi kwa ajili  ya ujenzi wa bwawa la maji Nsenkwa na ujenzi wa miundombinu ya kuchuja na kutibu maji katika bwawa hilo wilayani Mlele.

Kaimu Meneja wa RUWASA,Mlele Mhandisi Charles Mengo akitia saini ya makubaliano ya mkataba mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mwanamvua Mrindoko na Kaimu Meneja wa RUWASA Katavi Christian Mpena, amesema mradi huo umelenga kuboresha upatikanaji wa maji safi na salama huku ukitarajia kuwahudumia ya watu 68,426 wilayani humo.

Ametaja vijiji vitakavyonufaika na mradi huo ni pamoja na kijiji cha Inyonga, Kalovya, Kamalampaka utende, Mgombe, Kanoge, Wachawaseme, Mtakuja, Nsenkwa, Kaulolo, Ipwaga, Mapili, Masigo, Kamsisi, Imalauduki na Songambele.

Mhandisi Mengo ameweka wazi katika vijiji hivyo, Ruwasa inatarajia kutoa huduma ya maji lita za ujazo zaidi ya milioni 499.508 kwa mwaka huku bwawa hilo likiwa na uwezo wa kuhifadhi lita bilioni 2.8

“Mradi huu ni muhimu kwani utaweza kuhudumia siyo wakazi wa maeneo haya pekee bali kwa wafugaji ni mwarobaini tosha wa kutokomeza uhaba wa maji kwa mifug.Hivyo mradi utawezesha wafugaji kupata maji ya mifugo kupitia mabirika mawili ya kunyweshea mifugo” Amesema.

Ujenzi wa mabirika ya kunyweshea mifungo unatajwa kuwa suluhu ya kupunguza au kumaliza tatizo kubwa la uharibifu wa vyazo vya maji.

Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mwanamvua Mrindoko, amewataka wananchi na watendaji wa serikali wilaya ya Mlele kushirikiana kwa hali na mali na mkandarasi kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati.

Mrindoko amemkubusha mkandarasi kutekeleza mradi huo kwa wakati huku akizingatia viwango vya juu ili kuendana na thamani halisi ya fedha kama ilivyoainishwa kwenye mkataba na hatua za kinidhamu na sheria zitachukuliwa kama kutakuwapo na uzembe au ubabaishaji wowote katika utekelezaji wa mradi.

Mariam Hussan, Mkazi wa kijiji cha Nsekwa ameipongeza serikali kwa kazi kubwa ya kuhakikisha huduma ya maji safi na salama inaendelea kuimarika huku akitoa ombi kwa wasimamizi wa ujenzi wa mradi huo kuwa na moyo wa kizalendo wa kujenga bila kufanya makosa ya ubadhirifu.

Amebainisha kuwa mradi huo utaleta suluhisho la kudumu kwa matatizo ya upatikanaji wa maji safi na salama na kuchochea maeneleo ya kiuchumi na kijamii katika maeneo yao.