December 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rushwa ya ngono vyuoni yazidi kuitesa TAKUKURU

Na Zuhura Zukheir, TimesMajira Online, Iringa

KUFUATIA kukithiri kwa taarifa za vitendo vya rushwa ya ngono vyuo, wanafunzi nchini wametakiwa kutowafumbia macho walimu na wahadhiri wanaojihusisha na vitendo hivyo kwani vinaharibu malengo ya wahusika kimasomo na maisha yao kwa ujumla.

Wito huo umetolewa na Kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU mkoa wa Iringa, Mweli Kilimali wakati akizungumza na klabu za wapinga rushwa za vyuo vikuu na vya kati katika mafunzo  ya siku moja  yaliyofanyika mjini Iringa

Mweli amesema wanafunzi wasipojitambua na kupinga rushwa ya ngono watajiweka katika mazingira magumu kimaisha na kuliletea taifa hasara kutokana na kuzalisha watumishi wabovu ambao wanapatikana kwa kupata alama za juu baada ya kutoa rushwa ya ngono.

Aliwataka wanafunzi kuacha tabia ya uvivu wa kujisomea ili waweze kufanya vizuri katika mitihani yao.

Amesema wakijisomea wataweza kufanya mitihani yao kwa kujiamini, hali itayowafanya kuepuka vishawishi kutoka kwa wahadhiri wanaoendekeza vitendo vya rushwa ya ngono.

Amesema ubaya wa rushwa umeanzia katika vitabu vya dini, ambapo Quran tukufu na Biblia takatifu zote zimekema vitendo hivyo vya rushwa vyenye maudhui ya kupora haki isiyo halali.

“Rushwa ndugu zangu ni adui, rusha ni mbaya, rushwa imekemewa katika vitabu vyetu vitukufu ndani ya Quran tukufu na katika Biblia takatifu na tena rushwa hii ya ngono inavunja utu na kumdhalilisha mtenda na mtendewa, hivyo kataeni rushwa,”amesema Mweli.

Naye Mkuu wa Kitivo cha Elimu katika Chuo Kikuu cha RUCU, Profesa Gaudence Mpangala, alikili kuwepo kwa vitendo hivyo vyuoni na kuwataka wanafunzi kuacha woga badala yake watoe taarifa kwa vyombo vinavyoshughulikia masuala ya ukatili wa kijinsia katika ngazi za chuo, Polisi au TAKUKURU.

Amesema chuo chake kikibaini na kupata ushahidi wa kutosha kuwa mhadhiri anajihusisha na masuala ya rushwa ya ngono huwa hakuna maelezo, bali hupoteza kazi yake mara moja.

Amesema uamuzi inakuwa ni fundidho kwa wahadhiri wengine kama wana vitendo hivyo kuacha mara moja.

Kwa upande wake, Mshauri wa Wanafunzi wa RUCU, Martha Magembe aliwataka wanafunzi hao kutokuwa chanzo cha rushwa ya ngono kwa kutoa ushawishi kwa wahadhiri wao badala yake wahakikishe wanakuwa na msaada wa kufuatilia masomo.

Amesema kuna baadhi ya wanafunzi wanafanyiwa vitendo vya kikatili, lakini wananyamaza kutokana na woga au kuhofia kupoteza kitu fulani kutokana na vitisho hivyo wanahitaji kusaidiwa.