November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rungwe yajivunia kupunguza vifo vya mama na mtoto

Na Esther Macha,TimesmajiraOnline,Mbeya

HALMASHAURI ya Wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya imesema kuwa katika kipindi cha miaka mitatu ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan wameweza kupunguza vifo vya wajawazito kutoka vifo 60 kwa watu 100,000 na kufikia vifo 36 kwa watu 100

Renatus Mchau ni Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Rungwe mkoani hapa amesema hayo wakati wa kutoa taarifa ya utekelezaji wa miradi na mafanikio ya miaka mitatu ya Rais Dkt.Samia kwa msemaji mkuu wa serikali katika ukumbi wa mikutano wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa mbeya.

Aidha Mchau amesema kuwa kwenye eneo la vifo vya watoto wachanga walikuwa na vifo 22 kwa 1000 na kuwa mpaka Sasa wamefikia vifo 13 kwa watoto 1000 kutokana na uboreshaji wa huduma za afya.

“Kwenye maeneo yaliyokuwa yakisumbua katika eneo la uboreshaji wa huduma za afya ni eneo la vifo vya wajawazito na watoto lakini hivi sasa tunajivunia kazi kubwa iliyofanywa na serikali chini ya Rais Samia”amesema Mkurugenzi huyo.

Akizungumzia kuhusu ujenzi wa hospitali ya Makandana Mchau amesema kuna ujenzi wa jengo kubwa la golofa moja unaendelea ambalo wanategemea kuwa na wifi za kisasa ,majengo ya utawala ambapo lengo ni kuboresha huduma za afya kwa wananchi.

“Tumeweza kupata fedha zaidi ya Bil.2 na mradi huu mpaka sasa yupo kwenye hatua za kuta, lakini bado tumepata fedha zaidi ya shilingi Bil.2 kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya afya ambapo fedha hiyo imetoka serikali kuu “amesema Mchau .

Akielezea zaidi katika taarifa yake Mkurugenzi Mchau amesema pia wameweza kujenga vituo vipya vya afya vinne na kufikia vituo tisa ,lakini pia kupitia mapato ya ndani kumejengwa kituo cha afya kimoja cha kata ya Kinyala ambacho kimegharimu mil.400.