
Na Israel Mwaisaka, Rukwa
Mkuu wa mkoa Rukwa Charles Makongoro Nyerere amesisitiza umuhimu wa uwazi na usimamizi madhubuti wa Fedha za miradi ya miundombinu
Ameyasema hayo Jana Marchi 2,2026 alipokuwa aliongoza kikao Cha 44 Cha Bodi ya Barabara
Amesema kuwa Serikali inaendelea kuwekeza kwa kiwango kikubwa katika sekta ya barabara ili kuchochea ukuaji wa uchumi, kurahisisha usafirishaji na kupanua fursa za biashara za kikanda.
Amesema kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026, Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) umeidhinishiwa Sh bilioni 15.2 kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa barabara za mkoa. Aidha, Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) imepangiwa Sh bilioni 11.2 kwa matengenezo ya barabara za mijini na vijijini.
Makongoro alidai kuwa fedha hizo zinapaswa kusimamiwa kwa umakini ili ziwe na tija kwa wananchi, hususan katika kurahisisha usafirishaji wa mazao ya kilimo na uvuvi, kupunguza gharama za usafiri na kuongeza ajira.
Aliongeza kuwa Mkoa umejipanga kuimarisha barabara zinazounganisha Rukwa na nchi jirani za Zambia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, pamoja na kuboresha bandari za Ziwa Tanganyika ikiwemo Kabwe na Kasanga, hatua itakayopanua wigo wa biashara na kupunguza msongamano katika mpaka wa Tunduma.
Hata hivyo, Mkuu wa Mkoa ametumia kikao hicho kuwataka wananchi kuacha kuvamia na kutumia hifadhi za barabara, kupitisha mifugo kiholela barabarani na kugeuza barabara kuwa maegesho, akisisitiza kuwa ulinzi wa miundombinu ni wajibu wa kila mwananchi.
Aidha, amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt,Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuimarisha miundombinu ya kimkakati, akieleza kuwa kiwanja cha ndege cha Sumbawanga kimefikia asilimia 96 ya ujenzi kikiwa kimegharimu shilingi bilioni 60.1, huku ndege zikitarajiwa kuanza kutoa huduma mwezi huu wa Machi 2026.
Kikao hicho kimeweka mkazo katika kuimarisha usimamizi, uwazi na ufanisi wa utekelezaji wa miradi ya barabara kwa maendeleo ya Mkoa wa Rukwa na Taifa kwa ujumla.

More Stories
Kihongosi amtaka mkandarasi kuwalipa vibarua stahiki zao
DC Mbozi afuturisha wananchi, asisitiza mshikamano na Umoja.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali: Nina imani mubna utendaji kazi wa ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria