Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Mhe. Joseph Mkirikiti amesema anaridhishwa na jitihada za makusudi zinazoendelea kuchukuliwa na Wizara ya Maji katika kuwafikishia huduma ya maji wananchi wake.
Mhe. Mkirikiti amesema hayo ofisini kwake hivi karibuni alipotembelewa na Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga wakati wa ziara yake ya kukagua utekelezaji wa miradi ya maji mkoani humo sambamba na kukagua uwezekano wa kujenga miradi mikubwa kwa kutumia chanzo cha maji cha Ziwa Tanganyika.
“Wizara ya Maji ni wizara ya kimapinduzi, nimetembelea miradi yenu mingi nimeshuhudia mapinduzi makubwa. Miradi inatekelezwa kwa kasi na ufanisi mkubwa, kwakweli ninawapongeza sana mnatekeleza Ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi kivitendo,” alisema Mhe. Mkirikiti.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga alisema Wizara imejipanga vyema kuhakikisha azma na dhamira ya Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kumtua mama ndoo kichwani inafikiwa kwa ukamilifu.
“Mhe. Rais Samia ametuelekeza kuwa hataki kusikia wala kuona ucheleweshwaji wa ukamilishwaji wa miradi ya maji na hataki kusikia wala kuona ubadhirifu kwenye miradi ya maji,” alisema Mhandisi Sanga.
Alisema Wizara inatekeleza kwa vitendo maelekezo ya Mhe. Rais Samia “Wizara ya Maji kwa sasa ni wizara ya ufumbuzi wa changamoto ya maji na sio wizara ya lawama na ukame,” alisema Mhandisi Sanga.
More Stories
Mhandisi Kundo agoma kuweka jiwe la msingi mradi wa maji
Tanzania Mwenyeji wa Mkutano wa nchi zinazozalisha kahawa Afrika
Watatu mbaroni kwa tuhuma za mauaji wakigombania shamba