
Na Mwandishi Wetu, TimesmajiraOnline, Mbarali
MKURUGENZI wa Bonde la Maji la Rufiji, Mhandisi David Munkyala, amesema kuwa matumizi ya michezo ni miongoni mwa njia zinazotumika kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa usimamizi na uhifadhi wa rasilimali za maji, kutokana na mwitikio mkubwa wa vijana katika shughuli za michezo.
Mhandisi Munkyala amesema hayo mwishoni mwa wiki wakati akifunga mashindano ya soka ya Rufiji Basin Cup yaliyofanyika katika Viwanja vya Polisi Chimala, Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya.
Amesema matumizi ya michezo yamelenga kufikisha ujumbe wa uhifadhi wa vyanzo vya maji kwa wananchi wengi zaidi, hususan vijana ambao ni kundi kubwa linalojihusisha na shughuli za michezo.
Ameeleza kuwa mashindano hayo ni sehemu ya utekelezaji wa Mradi wa Nature-Based Solutions (NBS) Usangu, unaofadhiliwa na Benki ya Dunia na Serikali ya Japan kupitia Benki ya Dunia, ambao unalenga kutumia suluhisho zinazotegemea mifumo ya asili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi katika eneo la Usangu.
“Ili kupeleka ujumbe huu kwa jamii, tulilazimika kutumia michezo kwa kuamini kuwa kundi kubwa la vijana limejikita katika michezo, hivyo ni rahisi ujumbe kuwafikia. Michezo pia ni ajira, vipaji na afya, ndiyo maana tukaamua kutumia fursa hiyo kufikisha elimu kwa kaulimbiu ya utunzaji wa vyanzo vya maji,” amesema Munkyala.
Aidha, Mhandisi Munkyala ameipongeza taasisi isiyo ya kiserikali ya SALIOTA Organization inayojihusisha na utunzaji wa mazingira na mapambano dhidi ya ukatili kwa kushiriki kuratibu mashindano hayo yaliyodumu kwa takribani mwezi mmoja.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa SALIOTA Organization, Elisha Mwanikawaga, amesema ligi hiyo ilianza Oktoba 6 mwaka huu na kushirikisha vijiji 48, huku jumla ya michezo 56 ikichezwa.
Amesema kupitia mashindano hayo wamefanikiwa kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu uhifadhi wa rasilimali za maji, mazingira, mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia pamoja na matumizi ya nishati safi.
“Ligi hii ya Rufiji Basin Cup imeleta hamasa kubwa kuhusu uhifadhi wa maji na mazingira. Hadi tunamaliza mashindano, tumeweza kuwafikia watu 58,000 kati ya 80,000 tuliokuwa tumelenga, sawa na asilimia 72.5,” amesema Mwanikawaga.
Ameongeza kuwa mashindano hayo yamechangia kuwahamasisha vijana kushiriki katika juhudi za kutunza vyanzo vya maji ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali.
Katika matokeo ya mashindano hayo, timu ya Isunula FC imeibuka mshindi wa kwanza na kujinyakulia kitita cha Sh milioni moja pamoja na kombe, huku Azimio Mswiswi FC ikiibuka mshindi wa pili.

More Stories
Makonda awataka wafanyabiashara kujiweka tayari kunufaika na AFCON 2027
Wadau wa maendeleo waunga mkono ajenda ya Sifuri tatu
120 wafanyiwa uchunguzi wa fistula Chunya