Na Penina Malundo,TimesMajira
WAFANYABIASHARA na watoa huduma nchini wametakiwa kuanza kujiandaa mapema kutumia fursa za kiuchumi zitakazotokana na mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027, ikiwemo kupanua biashara zao, kujitangaza na kuimarisha mifumo ya malipo ya kidijitali ili kunufaika na wageni watakaotembelea Tanzania.
Wito huo umetolewa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, aliyesema mashindano hayo yanayotarajiwa kufanyika kwa pamoja nchini Tanzania, Kenya na Uganda ni fursa kubwa kwa wananchi kuongeza kipato, kukuza biashara na kuinua uchumi.
Makonda amesema maandalizi ya AFCON hayapaswi kujikita katika ujenzi na uboreshaji wa viwanja pamoja na miundombinu ya michezo pekee, bali yanapaswa kuwashirikisha wananchi katika kujiandaa kunufaika na fursa zitakazojitokeza kabla, wakati na baada ya mashindano hayo.

Alisema wafanyabiashara wanapaswa kutumia muda uliopo kusajili biashara zao, kuzitambulisha kupitia mitandao ya kijamii na kuboresha huduma wanazotoa ili waweze kukidhi mahitaji ya wageni kutoka mataifa mbalimbali.
Ametaja sekta zinazotarajiwa kunufaika kuwa ni hoteli, usafiri, utalii, usafi, matangazo na biashara ndogo ndogo, kutokana na ongezeko la mahitaji ya huduma litakalosababishwa na ujio wa timu, viongozi, mashabiki na watalii.
Aidha, amesisitiza wananchi kujifunza lugha za kimataifa ikiwemo Kiingereza, Kifaransa na Kiarabu ili kurahisisha mawasiliano na wageni watakaofika nchini, akieleza kuwa maandalizi ya wananchi ni sehemu muhimu ya mafanikio ya mashindano hayo.
Makonda amesema AFCON 2027 itakayohusisha timu 24 na mechi 52 kwa muda wa siku 29, ni hatua ya kihistoria kwa Afrika Mashariki, huku Tanzania ikitarajiwa kuwa mwenyeji wa sehemu kubwa ya mechi hizo zitakazofanyika Dar es Salaam, Arusha na Zanzibar.
Amesema mashindano hayo yatakayofanyika katika nchi tatu za Afrika Mashariki pia yatatoa fursa ya kuitangaza Tanzania kimataifa, kuongeza idadi ya watalii na kuimarisha ushirikiano wa kikanda.
Ameongeza kuwa kwa mara ya kwanza Kiswahili kinatarajiwa kutumika kama lugha rasmi ya mashindano hayo, hatua itakayoongeza hadhi ya lugha hiyo na kuitangaza zaidi katika medani za kimataifa.
Pia amewapongeza Rais wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Uganda, Yoweri Museveni na Rais wa Kenya, William Ruto kwa kushirikiana katika kuhakikisha nchi hizo zinajiandaa kwa mafanikio ya mashindano hayo.
Amemshukuru Rais Samia kwa uwekezaji na msukumo alioutoa katika maandalizi ya AFCON 2027, akiwataka Watanzania kutumia fursa hiyo kujitangaza, kukuza biashara na kuboresha maisha yao.
Amesisitiza kuwa mafanikio ya mashindano hayo hayatapimwa kwa ubora wa viwanja, idadi ya mabao au shangwe za mashabiki pekee, bali pia kwa namna yatakavyosaidia kukuza biashara, kuongeza watalii na kuboresha maisha ya wananchi.

More Stories
Wadau wa maendeleo waunga mkono ajenda ya Sifuri tatu
120 wafanyiwa uchunguzi wa fistula Chunya
Vikundi 39 Mbeya Dc vyapatiwa Mil.941