November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe

Rufaa ya Mbowe, vigogo CHADEMA kusikilizwa Mei

Na Grace Gurisha

RUFAA iliyokatwa na Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe na wenzake saba katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kupinga hukumu iliyotolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, itaanza kusikilizwa Mei 13, mwaka huu.

Mbowe na washtakiwa wenzake saba walikata rufaa kupinga hukumu waliohukumiwa hivi karibuni na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, mjijini Dar es Salaam kwenye ya uchochezi iliyokuwa ikiwakabili, ambapo walitozwa faini ya mamilioni ya fedha.

Jana kesi hiyo iliitwa kwa ajili ya kutajwa mbele ya Jaji Mfawidhi wa Kanda hiyo, Lameck Mlacha ambaye pamoja na mambo mengine aliahirisha kesi hiyo hadi Aprili 28, mwaka huu. Hata hivyo, Jaji Mlacha alipanga kesi hiyo kuanza kusikilizwa mbele ya Jaji Elvin Mgeta Mei 13, mwaka huu.

Katika rufaa hiyo namba 76 ya mwaka 2020 wakata rufani ni Mbowe, wengine ni Katibu Mkuu wa chama hicho, John Mnyika, Naibu Katibu Mkuu-Zanzibar, Salum Mwalimu,  Mbunge wa Iringa Mjini,  Peter Msigwa, Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko, Halima Mdee (Kawe), John Heche (Tarime Vijijini) na Ester Bulaya (Bunda).

Machi 10, 2020 Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu iliwahukumu warufani hao pamoja na  Dkt. Vicent Mashinji aliyehamia CCM mwaka huu. Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba  aliwahukumu kulipa faini ya sh. milioni 350 au kifungo cha miezi mitano jela baada ya kuwatia hatiani kwa makosa 12 kati ya 13 yaliokuwa yakiwakabili.

Warufani hao kwa nyakati tofauti walilipa faini hiyo na kukwepa kifungo. Katika rufaa yao wanadai Mahakama ya Kisutu ilikosea kisheria kushindwa kufanya mchanganuo mzuri kwa kufuata ushahidi uliotolewa.

Pia wanadai mahakama imeshindwa kuainisha viini vya makosa dhidi ya mashtaka na kuwahukumu bila  kuzingatia utetezi wa washitakiwa. Wanadai mahakama imeshindwa kuzingatia ushahidi kwa kushindwa kuangalia uwepo au ushiriki wa baadhi ya washitakiwa kwenye mkutano na kuwahukumu kwenye mashtaka ya  2,3 na 4.

Warufani hao wanadai mahakama hiyo ilikosea kupokea vielelezo vya kielektroniki ambavyo ni video, imekosea kisheria kuzingatia mashtaka ya 11,12 na 13 yamewafanya washitakiwa washindwe kujitetea.

Pia wanadai kuwa Mahakama ilikosea kisheria kuangalia maneno yaliyotolewa katika mashtaka ya 5,6,7,8,9,10 kwamba hayawezi kuhesabika kuwa makosa ya jinai kwa mujibu wa maamuzi yaliyotolewa katika kesi ya Hussein Katanga dhidi ya Jamhuri (1974) ukurasa wa 97 wa hukumu hiyo.

Pia wanadai hakukuwa na maelekezo ya awali yaliyofanyika sambamba na kupuuzwa kwa haki ya uwakilishi.

Wanadai mahakama ilikosea katika kutoa adhabu dhidi ya warufani ya kulipa faini ambayo ilikuwa inajitegemea wakati adhabu ya kifungo ilikuwa inaenda kwa pamoja hali hiyo imesababisha kuleta mkanganyiko wa kisheria.

Hata hivyo, warufani hao wanaiomba mahakama iamuru hukumu na adhabu iliyotolewa dhidi ya warufani ifutwe.