December 29, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

RPC Ngonyani: Vyombo vya habari chachu ya kupunguza uhalifu

Na George Mwigulu, Timesmajira Online,Katavi

Ushirikiano uliopo baina ya Jeshi la Polisi na Waandishi wa Habari Mkoa wa Katavi kupitia mpango wa polisi jamii umekuwa chachu kubwa ya kutokomeza vitendo vya kihalifu mkoani humo.

Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Katavi, ACP Kaster Ngonyani amezungumza hayo kwenye mdahalo maalumu ulioandaliwa na Umoja Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC) na kufanyika katika ukumbi wa St.Mathias uliopo Manispaa ya Mpanda.

Picha ya pamoja ikijumuisha Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Katavi,ACP Kaster Ngonyani, Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa habari MKoa wa Katavi Walter Mguluchuma,Ofisa Mipango Msaidizi kutoka UTPC na baadhi ya maofisa wa Jeshi la Polisi na waandishi wa habari.

Lengo la mdahalo huo awamu ya pili ni kuelimishana kitaaluma,kujenga na kuimarisha uhusiano na ushirikiano wa kikazi baina ya Jeshi la Polisi na Waandishi wa Habari utakao saidia kuepuka migongano inayoweza kuhatarisha zaidi usalama wa waandishi wa habari.

ACP.Ngonyani amesema Jeshi la polisi katika kutoa elimu kwa wananchi wa Mkoa wa Katavi waandishi wa habari wamekuwa kiungo muhimu kupitia vyombo vyao vya habari kuweza kuufikia umma kwa haraka.

“Ushirikiano huu tuliokuwa nao mwaka 2023 naomba uendelee mwaka 2024 katika kutoa elimu wanahabari ni chachu yetu hadi sasa Mkoa wa Katavi upo salama uharifu umepungua hata ukiingia kwenye RB zetu kwenye vituo vya polisi makosa ni machache sana kwa kuwa waandishi wa habari na jeshi la polisi tumeshirikiana kupinga uhalifu,” amesema ACP.Ngonyani.

Ofisa Mipango Msaidizi wa UTPC akiwasilisha mada katika mdahalo uliojumuisha jeshi la polisi na waandishi wa habari Mkoa wa Katavi

Akiwasilisha mada ya kuendeleza uhusiano mzuri na jeshi hilo na vyombo vya habari,SSP.Juma Jumanne amesema kuwa wanatambua umuhimu wa vyombo vya habari kwani uelimisha jamii juu ya madhara ya uhalifu,umuhimu wa utoaji taarifa za uhalifu na wahalifu mambo ambayo ni kazi ya msingi ya jeshi hilo.

SSP.Jumanne amefafanua kuwa waandishi wa habari wanaingia kwenye migogoro na jeshi la polisi pale ambapo kila mmoja kutokutambua majukumu ya mwingine jambo ambalo linapaswa kuepukwa kwa kujengeana uwezo wa kitaaluma.

Amesema vyombo vya habari vinanafasi na jukumu la kuandika habari za kisayansi,kijamii,michezo,mahakama na uchunguzi kwa ufundi,utaalamu na uchambuzi wa kina na kupaswa kuepuka kuripoti zaidi kuliko kuelimisha jamii juu ya madhara ya uhalifu.

“ Nitoe nukuu hii mnielewe…mwanzilishi wa kampuni ya magazeti ya Scrips Mr Willing Scripts, aliwahi kusema jukumu la vyombo vya habari ni kuwastarehesha wale wanaotaabika na kuwataabisha wanaostarehe na msimamizi wa habari wa Ikulu ya Marekani Mccury alisema huwezi kuwastarehesha au kuwataabisha watu bila kuwapa habari bora,” Amesema SSP Jumanne wakati akisisitiza waandishi wa habari kuzingatia maadili ya kazi.

Edmund Kipungu,Ofisa ameeleza kuwa uhusiano ukiimarishwa kwa vitendo utajenga usalama kwa waandishi wa habari pamoja na kutokomeza zaidi uharifu.

Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Katavi, Walter Mguluchuma wakati akifunga mdahalo huo amesema kuelekea uchanguzi wa serikali za mitaa mwaka huu na uchanguzi mkuu wa mwaka 2025 waandishi wanapaswa kuepuka kujihusisha na masuala ya kisiasa kwani yatawapunguzia imani kwa wananchi na kuhatarisha usalama wao.

Mguluchuma amesema waandishi wa habari wanapaswa kufanya kazi kwa kuzingatia maadili na kuepuka kuvunja sheria za nchi kwa sababu wao ni waandishi kwani watashughurikiwa kama wahalifu wengine.

Walter Mguluchuma,Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Katavi akifunga mdahalo wa awamu ya pili uliondaliwa na UTPC