December 27, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

RPC.Mutafungwa atoa maagizo kwa wakaguzi kata

Judith Ferdinand, Timesmajira Online, Mwanza

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) Wilbrod Mutafungwa ametoa maagizo kwa Wakaguzi Kata wa Mkoa wa Mwanza kwenda kusimamia usalama kwenye Kata zao.

Maagizo hayo ameyatoa Mei 13, 2024 wilayani ya Nyamagana mkoani hapa alipokutana na watu wenye Ualbino, Wakaguzi Kata na Viongozi wa Ustawi wa Jamii mkoani hapa.

Akizungumza wakati wa mkutano huo, Kamanda Mutafungwa amewataka Wakaguzi Kata kwenda kuyatambua maeneo wanayoishi watu wenye Ualbino, kusimamia mashauri yao mahakamani na kuangalia matishio ya kiusalama kwao ikiwemo migogoro ya ardhi na familia.

Katika hatua nyingine, Kamanda Mutafungwa amewakumbusha watu wenye Ualbino kuyapa uzito mambo ambayo siyo ya kawaida yanayojitokeza kwao kwa kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa.

Aidha, ameonya kuchukua hatua kali za kisheria kwa waganga wa jadi ambao bado wanapiga ramli chonganishi kwani elimu ya kutosha imeshatolewa kwao juu ya madhara ya vitendo hivyo.

Kwa upande wake Ofisa Ustawi wa Wilaya ya Nyamagana na Mratibu wa shughuli za Wazee na Walemavu Edith Ngowi amewataka Wakaguzi Kata kwenda kushirikisha kamati za watu wenye ulemavu zilizopo katika maeneo hayo ili kutatua changamoto za makundi mbalimbali.

Kwa upande wao, watu wenye Ualbino wameiomba jamii isiwatenge bali ishirikiane nao katika mambo yote ya kijamii kwani nao wanahitaji faraja.

Huu ni mwendelezo wa mpango mkakati wa Jeshi la Polisi wa kuishirikisha jamii katika kuzuia na kutanzua uhalifu kwa kutoa elimu ya usalama kwa makundi yote.